Mahakama Kuu imekataa maombi ya
aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kufungua shauri la
maombi ya kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai
uliosababisha ubunge wake kukoma.
Imesema mwanasheria mkuu huyo wa
Chadema hakupaswa kuwasilisha maombi hayo, alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi
wa ubunge katika jimbo hilo.
Akisoma uamuzi huo wa mahakama leo
Jumatatu Septemba 9, 2019 Jaji Sirillius Matupa amesema kama maombi yake
yakikubaliwa yatasababisha uvunjaji wa katiba kwa kuwa italazimika kuwa na
wabunge wawili kwenye jimbo moja.
Lissu alifungua maombi chini ya hati
ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai ambaye amempa mamlaka ya
kisheria kumwakilisha, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa
ubunge wake.
Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka
2019, dhidi ya Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu
aliomba kibali cha kufungua shauri kupinga taarifa ya Spika ya kukoma kwa
ubunge wake na mahakama iteunge taarifa hiyo.
Lissu yuko nchini Ubelgiji, kwa
ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa
hawajajulikana, tangu Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa, katika makazi yake,
jijini Dodoma akitokea bungeni.
Juni 28, 2019, wakati akiahirisha
mkutano wa 15 wa Bunge, Spika wa Bunge Job Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge
wa Lissu, huku alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya
Katiba ya Nchi.
Alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni
kutokuhudhuria vikao vya bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa
maandishi mahali aliko na kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
BREAKING: Mahakama Yatupilia Mbali Maombi ya Tundu Lissu Kupinga Kuvuliwa Ubunge
Reviewed by KUSAGANEWS
on
September 09, 2019
Rating:
No comments:
Post a Comment