Wakili Jeremiah Mtobesya amejitoa kuwawakilisha katika kesi
viongozi tisa wa Chadema, akiwamo mwenyekiti Freeman Mbowe akisema anaona haki
haitatendeka.
Mtobesya alijiondoa katika kesi hiyo iliyopo Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri
Alifikia uamuzi huo baada ya Mahakama kutoa uamuzi wa
kutupilia mbali maombi ya wateja wake ya kutaka kesi hiyo ya jinai namba
112/2018 iahirishwe ili kusubiri kusikilizwa maombi na rufani iliyopo Mahakama
ya Rufaa.
Washtakiwa
wamewasilisha katika Mahakama ya Rufaa maombi wakitaka kesi ya msingi iliyopo
Kisutu isitishwe usikilizwaji hadi rufaa ya kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu wa
kutupilia mbali maombi ya marejeo namba 126/2018 itakaposikilizwa na uamuzi
kutolewa
Katika Mahakama Kuu, washtakiwa waliiomba irejee mwenendo wa
kesi na uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Jana, baada ya Hakimu Mashauri kuyatupilia mbali maombi ya
washtakiwa aliamuru wasomewe maelezo ya awali ya kesi inayowakabili
Wakili Mtobesya alieleza kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya
kutajwa na uamuzi ulitolewa
Alisema hakubaliani na ombi la upande wa mashtaka la
kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali
Wakili Mtobesya aliieleza Mahakama kuwa anajiondoa katika
kesi kwa sababu anaona kwa namna mwenendo wa kesi unavyokwenda haki
haitatendeka
Kwa kauli hiyo, Mtobesya alibeba begi lake na kuondoka ndani
ya ukumbi namba moja wa Mahakama ambako kesi ilikuwa ikiendeshwa
Aliwaacha washtakiwa wakiwa hawana wakili mahakamani kwa
kuwa wakili mwingine anayewawakilisha, Peter Kibatala hakuwapo
Hakimu Mashauri aliwaeleza washtakiwa kwa kuwa hawakuwa na
wakili mwingine mahakamani, anaahirisha kesi hadi Agosti 27 watakaposomewa
maelezo ya awali
Hakimu Mashauri katika uamuzi wa kutupilia mbali maombi ya
washtakiwa, alisema kifungu cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai
kilichotumika kuwasilisha maombi hayo, hakiipi Mahakama mamlaka ya kuahirisha
kesi kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa
Alisema hata kama kifungu hicho kingekuwa kinaipa Mahakama
mamlaka ya kufanya hivyo, basi isingefanya hivyo kwa sababu ilishatoa uamuzi
mara kadhaa kutokana na maombi mbalimbali ya utetezi na kuyatupilia mbali,
hivyo haiwezi kula matapishi yake
Baada ya uamuzi kutolewa, wakili wa Serikali mkuu, Faraja
Nchimbi alisema kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa, na kwa kuwa uamuzi
umeshatolewa aliiomba Mahakama iridhie washtakiwa wasomewe maelezo ya awali.
Ombi hilo lilipingwa na Mtobesya
Hakimu Mashauri alisema ni kweli kesi ilipangwa kwa ajili ya
kutajwa kusubiri uamuzi ambao alishautoa, hivyo haoni haja ya kuahirisha
kusomwa kwa maelezo ya awali
Alisema usomaji wa maelezo hayo hauhitaji maandalizi, hivyo
aliamuru upande wa mashtaka kuwasomea washtakiwa hao
Wakili Kibatala alipowasilisha maombi awali, alidai Mahakama
hiyo ina mamlaka ya kuiahirisha kesi ya jinai namba 112/2018 kwa kipindi
kisichozidi siku 15 iwapo mshtakiwa atakuwa ndani na kisichozidi siku 30 iwapo
mshtakiwa au washtakiwa watakuwa nje kwa dhamana
Wakili Nchimbi alidai kuwa maombi hayo ya utetezi yanakosa
baraka za kisheria na hata miguu ya kisheria ya kusimama mbele ya Mahakama hiyo
Aliiomba Mahakama itupilie mbali maombi yaliyowasilishwa na
upande wa utetezi kwa sababu yanakosa msingi wa kisheria
Alidai maombi ya upande wa utetezi yanalenga kuchelewesha
kesi na hakuna kipya kilichowasilishwa mahakamani. Mbali na Mbowe washtakiwa
wengine katika kesi hiyo ya jinai ni naibu katibu mkuu wa Chadema –Zanzibar,
Salum Mwalimu na naibu katibu mkuu –Bara, John Mnyika ambaye pia ni mbunge wa
Kibamba.
Wengine ni wabunge wa
Tarime Vijijini, John Heche; Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda),
Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Esther Matiko (Tarime Mjini) na katibu
mkuu wa chama hicho, Dk Vincent Mashinji
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama,
kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya
kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai
Washtakiwa wanadaiwa
kutenda makosa hayo kati ya Februari Mosi na Februari 16 jijini Dar es Salaam
Wakili aeleza sababu za kujitoa kesi ya Mbowe
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 23, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment