Wabunge 19 Chadema kulinda kura za uchaguzi

Ili kuepuka kile ilichodai kuwa ni hujuma nyakati za uchaguzi, Chadema imepanga kuwatumia wabunge wake 19 kuwa mawakala katika Kata ya Kizota jijini Dodoma

Wabunge hao watatumika katika Kata ya Kizota jijini Dodoma kwenye uchaguzi utakaofanyika Septemba 16, ukihusisha pia kata 23 na majimbo mawili ya ubunge. CCM imeshatangazwa mshindi katika kata tatu na jimbo moja la Korogwe

Majimbo yatakayohusika katika uchaguzi huo mdogo ni Monduli la Arusha na Ukonga jijini Dar es Salaam baada ya waliokuwa wabunge wake kupitia Chadema, Mwita Waitara (Ukonga) na Julius Kalanga (Monduli) kutimkia CCM kisha kupitishwa tena CCM kuwania nafasi hiyo

Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kampeni zilianza Jumatatu Agosti 21. Hata hivyo, si CCM wala Chadema inayoshirikiana na ACT-Wazalendo waliozindua kampeni

Jana, Katibu wa Chadema Kanda ya Kati, Iddi Kizota akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma muda mfupi baada ya mgombea wa chama hicho, Omary Bangababo kurudisha fomu ya kugombea udiwani alisema watawatumia wabunge kusimamia upigaji na kuhesabu kura

Alisema wamefikia uamuzi huo baada ya baadhi ya mawakala wanaowekwa vituoni kujiondoa siku ya kupiga kura

“Ikiwezekana tutatumia hata wabunge na ukiangalia uchaguzi unafanyika Septemba 16, 2018 kipindi ambacho Bunge linaendelea na vikao vyake basi wabunge 19 tutaweza kuwapata,” alisema Kizota

“Katika kata yetu ya Kizota tuna vituo vya kupigia kura 19 hivyo hao wabunge 19 ni kwa ajili ya kuwa mawakala kwenye vituo vya kupigia kura,” aliongeza

Bangababo alisema ameamua kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo ili kuwatumikia wananchi ikiwa ni pamoja na kutatua kero ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kizota ya kutokuwa na maabara

Awali, Mtendaji Kata ya Kizota, Loyce Mrefu alisema wawakilishi wote wa vyama sita waliochukua fomu kwa nafasi hiyo ya udiwani walirejesha

Waliorudisha fomu ni Jamali Ngalya (CCM), Salum Salum (CUF), Omary Bangababo (Chadema), Jacklin Msajila (UPDP), Aziz Abbas (NCCR- Mageuzi) na Peter Malya (NLD).

Wakati hayo yakiendelea Kizota, rufaa ya mgombea ubunge wa Korogwe Vijijini (Chadema), Asia Saguti aliyeiwasilisha juzi kwa msimamizi wa uchaguzi imepokewa

Saguti pamoja na viongozi wa Chadema wamekata rufaa NEC wakipinga kutokupokewa kwa fomu za kugombea

Alipoulizwa jana kuhusu rufaa hiyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Athumani Kihamia alisema, “NEC inaendelea na taratibu zake na hatuwezi kujibizana na vyama au chama kimojakimoja katika vyombo vya habari, tutakapokamilisha, tutatoa taarifa ya pamoja.”

Vyama vinane ambavyo wagombea wake wamepitishwa katika Jimbo la Monduli vimeanza kampeni huku mchuano mkali ukitarajiwa kuwa kati CCM na Chadema sanjari na Ukonga

Mchuano huo utakuwa mkali zaidi baada ya ACT Wazalendo kushirikiana na Chadema na kuwaachia kusimamisha wagombea kwenye majimbo hayo

Mwenyekiti wa Uchaguzi wa ACT Wazalendo, Mohamed Babu alisema jana kwamba wanatarajia kuzindua kampeni za udiwani katika kata 10 kati ya 23 zinazorudia uchaguzi

Kuhusu kushirikiana na Chadema, Babu alisema, “Mazungumzo yanaendelea na yanavyoelekea, tutawaachia wenzetu Chadema Monduli na Ukonga na wao watatuachia katika hizo kata 10.”

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema vikao vya uzinduzi vinaendelea chini ya mwenyekiti wa kampeni wa Jimbo la Ukonga, Frederick Sumaye ambaye pia ni waziri mkuu mstaafu

Mrema alisema Monduli ambako aliyewahi kuwa waziri mkuu, Edward Lowassa ataongoza timu ya kampeni lakini hawajajua watazindua lini, “Ukonga tutazindua kampeni zetu Jumamosi (kesho) katika viwanja vya Mzambarauni.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kate Kamba alisema, “Ratiba bado haijatoka.”

Alipoelezwa kwa mujibu wa ratiba ya NEC, tayari kampeni zimekwisha kuanza, Kamba alisema, “Hilo unasema wewe, lakini hatujakaa vikao, labda nitafute kesho (leo) au keshokutwa (kesho).

Jimbo la Monduli ofisa uchaguzi Meleji Kuresoi alisema NEC imetoa ratiba kwa vyama vyote na “tayari vyama vyote vimeridhia na kuanza kampeni.”

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Loota Sanare alitamba kuwa tayari chama chake kimeshinda uchaguzi huo kwani kinakubalika Monduli, jimbo ambalo liliongozwa na Lowassa miaka 20 kuanzia 1995 hadi 2015.

 “Monduli wamejua makosa waliyofanya sasa wameona kazi nzuri za Serikali na wanaiunga mkono” alisema Sanare

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Arusha, Aman Golugwa alitaka uchaguzi uwe huru na haki na wana uhakika wa ushindi asubuhi

Wabunge 19 Chadema kulinda kura za uchaguzi Wabunge 19 Chadema kulinda kura za uchaguzi Reviewed by KUSAGANEWS on August 24, 2018 Rating: 5

No comments: