Na Rashid Nchimbi
Kitendo cha Mkuu wa Jeshi la Polisi
Nchini IGP Simon Sirro kumpandisha Cheo askari Polisi Fabian Nelson kutoka
Konstebo hadi Koplo baada ya kuibuka mshindi wa mbio za mita 5,000 katika
mashindano ya EAPCCO yaliyomalizika hivi karibuni jijini Dar es salaam kimetoa
faraja kubwa kwa Shirikisho la Riadha nchini.
Akiongea katika hafla ya kuwapongeza
askari Polisi ambao walishiriki michezo ya Riadha na Taekwondo iliyoandaliwa na
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi
Ramadhani Ng’anzi katika ukumbi wa Bwalo la Maofisa uliopo jijini hapa,
Katibu wa Shirikisho la Riadha nchini Bw.Wilhelmi Gidabuday alisema kwamba
anampongeza sana Mkuu wa Jeshi hilo nchini pamoja na Jeshi hilo kwa ujumla kwa
uamuzi walioufanya.
Alisema kwamba kitendo hicho
kimeonyesha Jeshi hilo linatambua na kuthamini mchango wa askari wake ambao
wanaliwakilisha Taifa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa hali ambayo
itaendeleza hamasa.
“Kwa niaba ya Rais wa Shirikisho la
Riadha nchini Mheshimiwa Anthony Mataka nichukue nafasi hii kumpongeza Mkuu wa
Jeshi la Polisi nchini baada ya kutoa motisha kwa kijana wake (Askari Polisi)
kwa kumpandisha cheo hali ambayo imetufariji sana na ni tafsiri sahihi kwamba
ili kuiletea sifa nchi yetu katika michezo yatupasa tushirikiane”. Alisema
Gidabuday
Aliahidi Shirikisho hilo kuendeleza
ushirikiano kwa Jeshi hilo kwa kipindi chochote ambacho watakuwa katika
mashindano ya Riadha na kuliomba Jeshi hilo kuendelea kutoa nafasi za ajira kwa
wanamichezo ili waweze kuendelea kuliletea sifa Jeshi hilo na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mnadhimu wa Jeshi la
Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Yusuf
Ilembo ambaye alimwakilisha Kamanda wa Polisi, alisema kwamba Jeshi hilo
liliandaa hafla hiyo kama njia mojawapo ya kuwapongeza na kuwahamasisha
askari wanamichezo ili waendelee kufanya vizuri katika mashindano
mbalimbali.
Aliwataka wanamichezo hao
kutobweteka na ushindi walioupata badala yake wanatakiwa kuongeza juhudi ili
waweze kupata mafanikio zaidi na kuahidi kuendelea kuwaunga mkono kwa hali na
mali ili waweze kufanya vizuri katika mashindano mengine.
Mwanariadha Fabiani Nelson alitumia
dakika 13:45:99 na kuvunja rekodi iliyowekwa na mshindi wa mwaka jana katika
mashindano hayo yaliyofanyika kwa mara ya kwanza Kampala nchini Uganda ambapo
askari Polisi wa Uganda Stephen Diott alishinda baada ya kutumia dakika
14:02:11.
Mashindano ya shirikisho la Majeshi
ya Polisi Ukanda wa Afrika Mashariki na kati yalifunguliwa rasmi tarehe 06
Agosti mwaka huu ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim
Majaliwa na kufungwa tarehe 12 Agosti ambapo Tanzania ilishika nafasi ya pili
katika ushindi wa jumla ambapo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Kenya na Uganda
ilishika nafasi ya Tatu.
MOTISHA YA IGP KWA ASKARI YAMUIBUA GIDABUDAY
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 24, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment