Utafiti wamtaja Makamu Rais Kenya kuongoza kwa rushwa


Naibu Rais wa Kenya, William Ruto ametajwa kuwa mwanasiasa anayeongoza kwa vitendo vya rushwa ikiwa ni maoni yaliyotolewa na wananchi waliohojiwa kwenye utafiti uliofanywa na taasisi ya utafiti ya Ipsos Synovate ambayo yanabainisha kwamba asilimia 33 ya Wakenya wanasema anasifika zaidi kwa vitendo hivyo akifuatiwa na Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru mwenye asilimia 31

Utafiti huo ulifanywa katika kaunti 45 kwa kuhusisha washiriki 2,000

Matokeo yanaonyesha asilimia 51 ya Wakenya wana imani na namna Rais Uhuru Kenyatta anavyopambana kudhibiti vitendo vya rushwa huku asilimia 32 wakiitaja rushwa kwamba ni tatizo sugu kwa Taifa hilo

Ruto, Waiguru wajibu

Akijibu tuhuma hizo, msemaji wa makamu wa Rais, David Mugonyi alisema utafiti huo umefadhiliwa na baadhi ya wanasiasa ukilenga kumchafua bosi wake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2022

“Wapo wanasiasa wanaoamini wanaweza kufanikiwa kwa mbinu chafu kama hizi za kuchafuana na kumzuia Ruto ashindwe kugombea urais kama anavyotarajia. Matokeo ya utafiti hayaonyeshi uhalisia, unapimaje mtazamo wa watu?” alihoji msemaji huyo

Kuthibitisha mtazamo wake, alisema hata takwimu zilizowasilishwa zimekaa kisiasa hivyo kuwa vigumu kwa mtu wa kawaida kuziamini

“Katika kipindi ambacho watu wanawaza kubadili Katiba kumzuia makamu wa rais kugombea nafasi ya juu zaidi haishangazi yanapotolewa matokeo ya utafiti kama huu,” alisisitiza

Msemaji huyo hakuwa peke yake kupinga utafiti huo, Waiguru pia alisema hajawahi kufikishwa mahakamani kwa tuhuma yoyote inayohusiana na rushwa hivyo akashangazwa na kuwekwa juu katika utafiti huo

“Ipsos inatumika kisiasa kuwachafua baadhi ya watu hasa wanaoogopwa kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2022. Wameona Kaunti ya Kirinyaga inasonga kimaendeleo na wanahaha,” alisema Waiguru

Licha ya Ruto na Waiguru, kwenye orodha hiyo pia yumo Aden Duale, kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa ambaye amepigiwa kura nyingi na wananchi walioshiriki utafiti huo

“Tuhuma za rushwa hazitakiwi kupimwa kwa maoni ya mtu, bali ushahidi. Huwezi kuwatuhumu watu kwa maoni ya mamluki,” alisema Duale

Utafiti wamtaja Makamu Rais Kenya kuongoza kwa rushwa Utafiti wamtaja Makamu Rais Kenya kuongoza kwa rushwa Reviewed by KUSAGANEWS on August 23, 2018 Rating: 5

No comments: