Utafiti: Uongozi wa nyumba kumi kumi suluhisho bora la migogoro


Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) umebaini kuwa mfumo wa uongzi wa  nyumba kumi katika Serikali za mitaa ni suluhisho la migogoro kwa kuwa unawapa nguvu vijana kushiriki mapambano dhidi ya uhalifu

Utafiti huo uliofanyika katika Mikoa saba umebaini kuwa kupitia mpango huo ambao ulikuwapo tangu miaka ya 1970 na kuasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere unaweza kuongeza uhusishwaji wa vijana katika masuala ya kijamii

Akizindua Utafiti huo leo Agosti 23 , Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,S ayansi na Teknolojia Dk.Ave Maria Semakafu amesema jamii haipaswi kuwaona vijana kama chanzo cha migogoro na badala yake iwe ni mbadala wa matatizo

"Vijana ni sehemu kubwa ya watu duniani na wamekuwa waathirika wakubwa wa vita, ukatili, usalama na ulinzi lakini wanaweza kuwa njia ya utatuzi wa mambo haya,"amesema

Amesema wizara ya elimu imeanzisha mfuko wa kuwawezesha vijana kupitia sekta zisizo rasmi ili kuondoa wimbi la vijana wasio na ajira ili kupunguza uhalifu

Mtafiti Mkuu wa utafiti huo, Profesa Benadetha Killian amesema hali inaonyesha kuwa nyumba kumi imekuwa msaada mkubwa katika usuluhishi kwenye ngazi za chini

Amesema katika maeneo ambayo yamekumbwa na migogoro mikubwa kama Kibiti na Rufiji utafiti umebaini kuwa hakuna uongozi wa nyumba kumi ambao ungeweza kuleta suluhu za viashiria vya migogoro

"Mgogoro wa Kibiti umedumu kwa takribani miaka miwili lakini ukiangalia hakukuwa na Uongozi wa nyumba kumi ambao ni rahisi kufikiwa pale watu wanapohitaji msaada hasa usuluhishi,"amesema

Utafiti huo unapendekeza Serikali ya nyumba kumi kutumika kama taasisi rasmi ya usuluhishi kwa sababu ni rahisi kuwafikia viongozi wake kutokana na udogo wa eneo

"Mfumo wa nyumba kumi bado una nguvu na haujafa.Kupitia nyumba kumi unakuta vijana wanashiriki katika ulinzi shirikishi ambao unasaidia kupunguza uhalifu,"amesema Mtafiti huyo

Utafiti huo umefanyika katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka jana ukihusisha Mikoa ya Tanga,Kagera,Pwani,Mtwara,Arusha,Mwanza na Zanzibar

Utafiti: Uongozi wa nyumba kumi kumi suluhisho bora la migogoro Utafiti: Uongozi wa nyumba kumi kumi suluhisho bora la migogoro Reviewed by KUSAGANEWS on August 23, 2018 Rating: 5

No comments: