![]() |
Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani
Jafo(katikati) akitoa maelekezo kwa Mkandarasi anayejenga Soko la Kijichi
kuzingatia ubora na kujali muda wa kukamilisha mradi huo.
|
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa Mhe.Selemani Jafo ameendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Dar es
Salaam na leo ametembelea Manispaa ya
Temeka kukagua maendeleo ya mradi wa uboreshaji wa miundombinu unaotekelezwa
kupitia mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam (DMDP).
Akiwa katika ziara hiyo Mhe. Jafo ametembelea na kukagua
ujenzi wa masoko ya kisasa yanayojengwa katika Kata ya Kijichi na Mbagala Kuu, Kituo cha Mabasi madogo sambamba na Ujenzi
wa barabara za mitaa inazojengwa kwa kiwango cha Lami katika Kata hizo.
Akitembelea maeneo ya miradi Mhe. Jafo alisisitiza ubora
wa miradi hiyo pindi itakapokamilika na kuwataka Wakandarasi wajenzi
kukahikisha wanaongeza umakini na kuzingatia ubora katika kila hatua ya ujenzi
huku wakijali muda uliowekwa wa ukamilishaji wa miradi hiyo.
“Fedha za miradi hii
zipo zinasubiria kazi tu ikamilike lakini sio kukamilika chini ya
kiwango. Kinachotakiwa na nyie wakandarasi mnazingatia Mikataba mliongia
mwanzoni kabla hamjaanza kazi na kufikia viwango vile vilivyowekwa ili Fedha
itakayolipwa iendane na kazi iliyofanyika” alisema Mhe. Jafo.
Akiwa katika Soko la Kijichi Mhe, Jafo amesema ameridhishwa
na ujenzi unaondelea ila pia amewataka uongozi wa Temeke pamoja na Mkandarasi
kutoa ajira ndogondogo kwa vijana wa maeneo hayo ili nao waweze kujikwamua
kiuchumi.
Akizungumza katika ziara hiyo Mbunge wa Jimbo la Temeke Mhe.
Issa Mangungu amesema hatasubiria tena Mhe. Waziri Jafo aje kukagua miradi hii
ndio na yeye afike kwenye maeneo hayo bali ataweka ratiba katika kila wiki
kuhakikisha anapitia miradi yote kuona maendeleo ya ujenzi na kuhakiki ubora wa
miundombinu hiyo itakayoongeza thamani ya Manispaa ya Temeke kwa ujumla.
Akisoma taarifa ya Utekelezaji wa Miradi Mratibu wa Dmdp Manispaa ya Temeke Edward Haule
amesema kwa sasa wameanza
kutekeleza mradi huu katika Kata 8 kati ya 23 zinazohusika na katika maeneo yote
hayo wanaboresha miundombinu msingi
ambayo ni kichocheo cha ustawi wa jamii husika.
Katika Kata ambazo zimetembelewa leo na Mhe. Waziri Jafo
hususan ni Kata ya Kijichi kazi zinazoendelea ni ujenzi wa barabara 13 zenye
urefu wa Km 18.7, Soko moja lenye uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 200, kituo
kimoja cha daladala, mfumo wa maji utakaohudumia wakazi zaidi ya 300,000 na taa
za barabarani 700 kwa gharama ya Tsh
Bil. 22.
Aliongeza kuwa katika Kata ya Mbagala Kuu kazi
zitakazofanyika ni ujenzi wa barabara 12 zenye urefu wa Km 12, soko moja lenye
uwezo wa kubeba wafanyabiashara zaidi ya
290, kituo cha daladala, mfumo wa maji utakaohudumia wakazi zaidi ya 400,000 na
Taa za barabarani 600 kwa gharama ya Tsh Bil. 19.
Miradi hii itakayoleta manufaa makubwa kwa Manispaa ya
Temeke na kwa wananchi kwa ujumla
inategemewa kukamilika mapema mwezi Januari mwaka 2019.
JAFO AWATAKA TEMEKE KUKAMILISHA MIRADI YA DMDP KWA UBORA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 23, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment