TLS chapinga marekebisho ya sheria yake


Chama cha Wanasheria nchini (TLS) kimepinga Marekebisho ya Sheria ya TLS yanayolenga kuwakataza watumishi wa Serikali na viongozi wa kisiasa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chama hicho kikieleza kuwa marekebisho hayo yanawabagua wanachama.

 Akizungumza leo Agosti 24 wakati wadau wa masuala ya sheria wakitoa maoni yao kwa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, mwakilishi wa TLS, Jebra Kambole alisema marekebisho hayo pia yanalenga katika kumfanya mwanachama mmoja kuwa na nguvu kuliko wengine

TLS ilikuwa ikitoa maoni kuhusu Muswada wa Sheria namba mbili wa mwaka 2018

“Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni mwanachama wetu, anapelekewa kanuni kwa ajili ya kupitisha ni wazi hapa mwanachama huyu anakuwa na nguvu kuliko wanachama wengine,”alisema

Alitaja sababu nyingine ya kupinga mapendekezo hayo ni pale Mwanasheria Mkuu wa Serikali AG atakapopewa mamlaka ya kupitisha kanuni, chama hicho hakitakuwa na uhuru wa kujiendesha

Mbunge wa Malindi (CUF) Ally Saleh alitaka TLS kiwashawishi kwa nini mkono wa Serikali usiingie katika chama hicho

Hoja ya Saleh iliungwa mkono na mwenyekiti wa kikao hicho, Dk Damas Ndumbaro ambaye alikitaka chama hicho wakati kinajibu swali hilo kutoa mifano ya bodi nyingine ambazo Serikali haitengenezi kanuni
“Pia mmesema kuna ubaguzi sasa ikitokea siku Rais anagombea uraisi je mtamruhusu? Tuchukue mfano Rais Magufuli ni mwanachama wa TLS na uchaguzi uko Februari mwakani mtamruhusu agombee? Kama sheria inaruhusu nani atamzuia?” Alihoji Dk Ndumbaro ambaye pia ni mbunge wa

Dk Ndumbaro ambaye pia ni mwanachama wa siku nyingi wa TLS alisema kumekuwa na mabadiliko ya majukumu ya TLS kutoka katika kushughulikia taaluma na kujiingiza katika siasa

Akijibu hoja hizo, Kambole alisema hawezi kuwa na jibu la moja kwa moja kuhusu upitishaji wa kanuni za uendeshaji kwa bodi nyingine lakini kuna tofauti kubwa kati yao na bodi nyingine za kitaaluma

“Huwezi kukuta daktari anakutana na daktari wa serikali lakini sisi katika mashauri huwa tunakutana na AG sisi upande huu mwingine. Lakini pia chama chetu hakina fungu lolote linalotoka Serikalini, ni michango ya wanachama wenyewe,”alisema

Alisema iwapo mwanachama anayelipa michango yake ataomba uongozi hata kama ni mtumishi wa Serikali atapigiwa kura sawa na wanachama wengine

Akizungumzia hoja hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria Palamagamba Kabudi alisema sehemu ya 14 ya sheria hiyo inapendekeza kurekebisha Sheria ya TLS, Sura ya 307

Alisema marekebisho hayo yanalenga kuweka vigezo ambavyo vitatumika kwa wajumbe wa baraza na taratibu za kuzifuata wakati wa utungaji wa kanuni zinazosimamia chama hicho

“Kwa ufupi mapendekezo ya marekebisho ya sheria hii yana lengo la kuweka masharti ya kumtaka Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuzipitisha kanuni zinazotungwa na chama kabla ya kuchapishwa. Pia kanuni hizo zitachapishwa kwenye Gazeti la Serikali,”alisema

TLS chapinga marekebisho ya sheria yake TLS chapinga marekebisho ya sheria yake Reviewed by KUSAGANEWS on August 24, 2018 Rating: 5

No comments: