Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira
(NEMC), Heche Suguta amewaonya wakandarasi wanaosafisha mto Mbezi na matawi
yake kutojikita kwenye biashara ya kuuza mchanga na kusahau jukumu lao la
msingi
Kampuni tatu zilizoshinda kandarasi ya kusafisha mto huo
kufuatia mafuriko yaliyoyokea Oktoba mwaka jana ni pamoja na Othyblue
International, Benson na Carrebean
Akizungumza katika mkutano ulioitishwa kati ya mitaa ya
Mbezi A, Ukwamani na Mzimuni wilayani Kinondoni leo Agosti 23 Heche amesema
NEMC itaangalia mkataba wa wakandarasi hao
"Wengi mmesema kazi iendelee ila kuwe na usimamizi
mzuri. Hizi kazi zinafanyika kwa nyaraka, tutaangalia mpango kazi wao. Je,
wanafuata sheria? Mbona wanachimba mchanga tu?" amehoji Heche.
Licha ya baadhi ya wananchi kuridhia usafishwaji huo,
wamekosoa uchimbaji wa mchanga na kutotekelezwa kwa makubaliano
"Nia ya serikali kuleta tingatinga ni kusafisha mto,
kwa hiyo uchimbaji wa mchanga sasa basi na mchanga uliolundikwa katikati
uondolewe," amesema May Maumba ambaye ni mkazi wa mtaa wa Mzimuni.
Naye Joseph Mfaume amesema licha kazi nzuri zinazofanywa na
wakandarasi hao, wananchi wanashindwa kuwaelewa kwa sababu ya kukosa mpango
kazi
Mkandarasi wa kampuni ya Othyblue International, Heri
Mohammed amrsema malalamiko ya wananchi hao yana sura ya kisiasa na kiuchumi
"Wengi wanaopinga kazi hii ni wanachama wa Chadema na
wanaounga mkono ni CCM. Halafu kuna watu walikosa tenda ya kazi hii, ndio
wanahamasisha wananchi kupinga kazi yetu," amesema Mohammed
Mwakilishi wa Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu, Mshube Wilson
amewataka wananchi hao kupeleka malalamiko yao kwenye kamati ya mazingira ya
kata badala ya kuwasumbua wakandarasi wawapo kazini
NEMC yawaonya wakandarasi wanaosafisha mito Dar
Reviewed by KUSAGANEWS
on
August 23, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment