Waziri Mkuu azungumzia ufukwe wa Coco Beach


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza manispaa ya Kinondoni kupanga mikakati wa kufanya usafi pembezoni mwa Bahari ya Hindi eneo la Coco Beach jijini hapa pamoja na kuimarisha ulinzi ili kuwavutia wawekezaji

Pia, ameitaka manispaa hiyo kuratibu na kuandaa shughuli za burudani katika fukwe hiyo ili zifanyike siku za Jumapili na Jumamosi kwa maelezo kuwa zitafanya eneo hilo kupendeza na kuwa kivutio nchini

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo asubuhi Jumatano Julai 25, 2018 baada ya kuwaongoza wananchi kufanya usafi katika fukwe hiyo, ikiwa ni kuadhimisha siku ya kumbukumbu ya mashujaa

“Eneo hili linatembelewa na watu wengi kutoka ndani ya nchi na nje ya nchi, hivyo ni lazima lilindwe na kuwa safi ili  kuwavutia wawekezaji,” amesema

Usafi huo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa Juni 29, 2018 akiwataka Watanzania kufanya usafi kwenye maeneo yao ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mashujaa ambayo huadhimishwa Julai 25, kila mwaka

Huku akiwa sambamba na mkewe, Majaliwa amefanya usafi kwa dakika 20

Alifika eneo hilo saa 2:10 asubuhi na kuungana na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaa pamoja na wananchi waliokuwa wakimsubiri

Katika maelezo yake, Majaliwa amesema pamoja na mipango ya manispaa ya kuboresha eneo hilo bado jitihada zinahitajika za kufanya usafi kwasababu ufukwe huo ni muhimu kwa wananchi wanaoenda kupumzika na kupata burudani

Alionyesha kutoridhishwa na usafi unaofanyika eneo hilo kwa sasa na kutaka vibanda vilivyopo pembezoni mwa ufukwe huo kuboreshwa ili viwe vya kisasa huku akiwataka Watanzania kugeuza usafi kuwa jambo la kufanya kila siku

“Mnajua eneo hili kila anayekuja alikuwa analipia gharama kubwa lakini Rais Magufuli aliagiza litumike kwa wote,” amesema

Baadhi ya viongozi walioshiriki kufanya usafi ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa
Waziri Mkuu azungumzia ufukwe wa Coco Beach Waziri Mkuu azungumzia ufukwe wa Coco Beach Reviewed by KUSAGANEWS on July 25, 2018 Rating: 5

No comments: