Vigogo wa taasisi mbili za Ushirika mkoani Kilimanjaro,
wanaokabiliwa na kesi mbili za uhujumu uchumi, wataendelea kusota mahabusu huku
mmoja akikodi wakili kwa ajili ya kumtetea
Vigogo hao wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Kahawa mkoa
Kilimanjaro (KNCU) na kiwanda cha kukoboa kahawa Tanganyika (TCCCo),
wataendelea kukaa rumande hadi Agosti 7.
Mwenyekiti wa zamani wa KNCU, Aloyce Kitau ambaye
alipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Julai 9, 2018 hakuwa na wakili,
sasa amemkodi wakili Elikunda Kipoko kumtetea
Hayo yamebainika leo Jumanne Julai 24, 2018 wakati
kesi hiyo ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Moshi, Pamela Mazengo na wakili wa
Serikali mwandamizi, Tamari Mndeme kueleza kuwa upelelezi wa kesi hizo
haujakamilika
Wanaoshitakiwa pamoja na Kitau ni aliyekuwa makamu
mwenyekiti wa KNCU, Hatibu Mwanga anayetetewa na wakili Sawayael Shoo na Meneja
mkuu, Honest Temba anayetetewa na wakili Jullius Semali
Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Julai 2014 na Novemba
2017, kwa pamoja walitumia vibaya madaraka yao wakiwa viongozi wa KNCU na
kuisababishia KNCU, hasara ya Sh2.9 bilioni
Katika shitaka la pili, upande wa mashitaka unadai katika
kipindi hicho, washitakiwa kwa matendo ya makusudi, waliilipa kampuni ya
Oceanic Link kiasi hicho cha fedha na kuisababishia KNCU hasara ya Sh2.9
bilioni
Mbali na kesi hiyo, jana walifikishwa kortini kwa mara ya
pili, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TCCCo, Maynard Swai na Meneja mkuu wake,
Andrew Kleruu wanaokabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi.
Swai na Kleruu,
wanaotetewa na wakili Kipoko wakili, wanadaiwa kuwa kati ya Januari 2014 na
Desemba 2015, walitumia vibaya madaraka yao na kununua mtambo wa kukoboa
kahawa bila kufuata taratibu
Upande wa mashitaka unadai kuwa watuhumiwa walinunua
mtambo wa kukoboa kahawa kutoka kampuni ya Brazafric ya Brazil bila kufuata
taratibu na kuisababishia TCCCo hasara ya Sh1.67 bilioni
Kama ilivyokuwa katika kesi ya vigogo wa KNCU, wakili
mwandamizi wa Serikali, Tamari Mndeme aliomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa
kesi hiyo kwa kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika
Hakimu mkazi wa Moshi,Pamela Mazengo aliahirisha kesi hiyo
hadi Agosti 7 mwaka huu na kuamuru washitakiwa wote waendelee kusota rumande
katika gereza kuu la Karanga mjini Moshi
Vigogo KNCU, TCCCo kuendelea kusota mahabusu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 24, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment