Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli ametuma salamu za pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Filipe
Jacinto Nyusi, wanachama wa chama cha FRELIMO na wananchi wote wa Msumbiji
ambao kesho tarehe 25 Julai, 2018 wanaadhimisha miaka 50 ya Mkutano wa Pili wa
FRELIMO
Pamoja na salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amemtuma Rais
Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa na Makamu Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM)-Bara Ndg. Philip Japhet Mangula kumwakilisha katika
sherehe za maadhimisho hayo zitakazofanyika Matchedje katika jimbo la Niassa.
Katika salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amewatakia heri
wananchi wote wa Msumbiji na kuwapongeza kwa mafanikio waliyoyapata ikiwemo
kudumisha uhuru wao, na kwamba Tanzania inajivunia uhusiano wa kidugu,
kihistoria na ujirani mwema na nchi hiyo
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
CCM na Watanzania wote naungana nawe Mhe. Rais Nyusi na wananchi wote wa
Msumbiji katika kusherehekea siku hii muhimu, siku hii inatukumbusha jukumu
muhimu tulilonalo la kuulinda na kuutetea uhuru ambao waasisi wa Mataifa yetu
yaani Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Samora Moises
Machel wa Msumbiji waliupigania” amesema Mhe. Rais Magufuli
Amemhakikishia Mhe. Rais Nyusi kuwa Tanzania itaendelea
kudumisha na kukuza uhusiano wake na Msumbiji katika ngazi ya Serikali na vyama
vya CCM na FRELIMO, na pia kuimarisha ushirikiano hasa katika masuala ya uchumi
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa wananchi wa
Tanzania na Msumbiji kuendelea kutumia fursa za maendeleo zilizopo na kudumisha
udugu wao.
Raisi Magufuli Atuma salamu za pongezi kwa Raisi wa Msumbiji
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 24, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment