MARA kwa mara familia nyingi zinalalamikia gesi kumalizika
mapema kuliko walivyotarajia na wakati mwingine mtungi wa kilo 30 unadaiwa
kutumiwa kwa siku chache
Hivi karibuni Gazeti dada la Financial Times, lilifanya
uchunguzi kwa wateja wa gesi jijini Dar es Salaam na kuelezwa wajanja
wanavyopunguza nishati hiyo kwa kuchakachua uzito wa nishati hiyo
Mbinu zinazotumiwa kuiba gesi kutoka kwenye mitungi
zilielezwa kuwa ni za kizamani na mojawapo ni kutumia mipira inayochomekwa
kwenye mtungi uliojaa na ulioko tupu
Mpira wa kusukuma hukandamizwa kwenye mtungi uliojaa ili
kuivuta na kuiingiza kwenye mtungi ulio tupu, hivyo kuhamisha kiasi cha gesi
kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
Wateja huuziwa uzito pungufu kwa kuwa wengi hawawezi
kutofautisha mitungi hiyo, tena wana imani kuwa imejaa, kumbe
imechakachuliwa.
Kiuchumi, inaelezwa kuwa ni tatizo linalowasababishia
wateja hasara ya mamilioni ya fedha kila mwaka na pia kuwaneemesha baadhi ya
wauzaji wasio waadilifu
Baadhi ya wateja waliliambia gazeti hili kuwa wananunua gesi
kutoka maduka ya mitaani, kwa mawakala, au kutoka kwenye vituo vya mafuta
au kwa wauzaji wanaosambaza mitaani na magari, lakini kinachowashangaza
ni kuambulia nusu mtungi bila kugundua wakati wanaponunua
Wateja wengi wa gesi walidokeza kuwa wanashangaa
wanaitumia kwa muda mfupi na kwamba wanaumia zaidi kwa vile ni waangalifu
na wanajitahidi kuiokoa kwa vile hutumia kuni kupikia vyakula vinavyohitaji
moto mwingi kama maharage, nyama na makande
Christina Komba, mteja aliyezungumza na FT alisema: “Nanunua
mtungi wa kilo 30 kwa ajili ya familia yangu yenye watu watatu.
Awali ulikaa hata kwa miezi miwili kwa sababu ninatumia mkaa
pia. Lakini kwa siku za karibuni nashangaa mtungi haumalizi hata wiki mbili
Haitham Fadhili, aliunga mkono maelezo ya Christina akisema:
“Kwa mara ya kwanza nilidhani mpira wa gesi umetoboka na gesi inavuja. Nikaanza
pia kuhisi msaidizi wangu wa ndani anaitumia bila uangalifu, lakini nikaja
kusikia na wenzangu wanalalamikia hayo hayo
KAULI <b>YA EWURA
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji
(Ewura), inaeleza kuwa inaelewa kuhusu uwezekano wa kuwapo wizi wa gesi
unaoweza kufanyika kwa kuwapunja wateja na inachukua hatua za kuudhibiti
“Tatizo si kubwa kihivyo, tangu mwaka jana tunajihusisha
kikamilifu na udhibiti wa nishati hii. Na hili ni eneo letu jingine la
kipaumbele baada ya kusimamia na kudhibiti sekta ya mafuta,” alisema Meneja
Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo
Kaguo anaeleza kuwa walishagundua maeneo mengi yanajaza
mitungi ya gesi kwa kuchakachua na yako Dar es Salaam, akisema hii ni kwa
sababu biashara hiyo inaongezeka kwa kasi kubwa
Kwa mujibu wa takwimu za Ewura, matumizi ya gesi
kupikia yameongezeka kwa kiwango cha juu wakati utumiaji wa mafuta ya taa
ukipungua, hivyo kuibuka matapeli wa kuibia wateja gesi inapojazwa kwenye
mitungi
Ripoti ya mdhibiti huyo ya mwaka 2017 kuhusu ununuzi wa gesi
inaeleza kwamba Tanzania iliagiza takribani tani 107,263 za nishati hiyo
mwaka 2017 ilikinganishwa na tani 90,296 mwaka 2016
KUDHIBITI
Ewura inaeleza kwamba utapeli huo unafahamika na kwamba
katika jitihada za kuwadhibiti wahusika ilifunga kituo cha kuuza nishati
kilichoko Kibaha, mkoani Pwani baada ya kuwakurupusha baadhi ya
wafanyakazi wake wakiiba gesi kutoka kwenye mitungi
“Katika kituo cha Kalanguti huko Maili Moja, Kibaha
ilibainika kuwa muuzaji alikuwa anahifadhi mitungi ya gesi kwenye stoo ya chuma
chakavu na kwamba wanachakachua mitungi hiyo,” kwa mujibu wa Ewura
Ewura ilisema mawakala wa gesi wanatakiwa kuwa na mizani ya
kupima uzito wa mitungi wanapowauzia wateja ili kuepusha upungufu huo
Na wateja nao wanashauriwa kuwa na mizani ya kupima uzito
wanaponunua ili wasitapeliwe. Aidha, wanashauriwa kununua kwa mawakala na
wauzaji wenye vibali na si vichochoroni
Hata hivyo, wateja wengi hawafahamu kutofautisha uzito wakati
mtungi umejaa na ulioko tupu
Kaguo alisema Ewura imetoa na kusimamia maelekezo mbalimbali
kama kuhakikisha mitungi imefungwa kikamilifu, ina uzito unaotajwa, kama imejaa
imewekewa lakiri (seal) na inapimwa uzito inapouzwa na mteja anaweza kuhakiki
taarifa zote bila usumbufu
“Wateja wawe makini wanaponunua gesi kuhakikisha kuwa
mitungi yote ina vigezo vinavyoelezwa na Ewura kama kuonyesha uzito sahihi,
imefungwa na kubanwa, ina lakiri, kama wana shaka wanapima uzani na kunapokuwa
na hitilafu wawasiliane na mamlaka hiyo ya udhibiti,” anasema Kaguo
Uchunguzi wabaini Jinsi wajanja wanavyochakachua Gesi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 25, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment