Kwamba tarehe 25.07.2018 majira ya
saa 03:00hrs usiku katika mtaa wa Nyakabungo “A” kata ya Isamilo wilaya ya
Nyamgana jiji na mkoa wa Mwanza, nyumba mbili mali ya Selina Francis, @ mama
Mkapa, miaka 50, mkazi wa mtaa Nyakabungo na Abdalah Mwita @ Machela,
zimechomwa moto na kundi la wananchi waliojichukulia sheria mkononi baada ya
kuona watoto wa wahanga tajwa hapo juu wakijihusisha na uhalifu hapo mtaani
mara kwa mara kwani watoto hao wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa
mahakamani lakini wamekua wakiachiliwa kwa dhamana kisha kurudia tena kutenda uhalifu
kitendo ambacho kimekuwa kero kubwa kwa wananchi wa eneo hilo.
Vilevile nyumba moja mali ya Manka
Francis James @Mushi, iliharibiwa vibaya na kundi hilo la wananchi kwa kuvunjwa
milango na madirisha na kuharibiwa vitu mbalimbali vilivyokuwemo ndani kwa kumtuhumu
mwanamke huyo kuwa anashiriki katika kuficha wezi na vibaka pamoja na
kujihusisha na utapeli kwa wananchi wa mtaani hapo na Mwanza kwa ujumla kwa
kuwauzia dhahabu bandia, kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Inadaiwa kuwa wananchi wa mtaa tajwa
hapo juu wamekuwa wakimlalamikia na kumtuhumu mtoto wa Mama Selina Francis
aitwaye Mkapa Mwabe pamoja na mtoto wa mzee Abdalah Mwita aitwaye Emmanuel
Mwita @ Mwita kuwa ni wezi/vibaka mtaani hapo.
Vilevile wakimtuhumu Manka Fransis
James @ Mushi kwa kushiriki kuwaficha wezi na vibaka nyumbani kwake pindi
wanapotenda uhalifu mtaani na kuwatapeli wananchi kwa kuwauzia dhahabu feki.
Inasemekana kuwa kutokana na tuhuma
hizo ndipo tarehe na majira tajwa hapo juu kundi la wananchi waliojawa na
hasira kutokana na vitendo vya waanga walikwenda na kuvamia nyumba ya bwana
Abdalah Mwita pamoja na nyumba ya mama Selina Francis ambapo waliwakuta watoto
wadogo, wenye nyumba hawakuwepo kisha waliwatoa watoto nje na kuchoma nyumba
hizo moto.
Aidha inadaiwa kuwa baada ya hapo
kundi hilo la wananchi lilikwenda kwenye nyumba ya Manka Francis pia walikuta
watoto mwenye nyumba hakuwepo kisha waliwatoa watoto nje na walivunja
madirisha na milango na kuharibu vitu mbalimbali vilivyokuwepo katika nyumba
hiyo wakiwa wanataka……
Baada ya hapo raia wema walitoa
taarifa kituo cha polisi ambapo askari waliokuwa doria walifika haraka eneo la
tukio na kukuta tayari wahalifu hao wamekimbia.
Msako mkali wa kuwatafuta wale wote
wanaotuhumiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika uhalifu huo bado
unaendelea.
Pia msako na ufuatiliaji wa vijana
wanaotuhumiwa kufanya uhalifu mtaani hapo pamoja na wazazi wao bado
unaendelea.
Pia hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa
au kupoteza maisha katika tukio hilo, aidha thamani halisi ya vitu vyote
vilivyoharibiwa katika uhalifu huo bado haujafahamika.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza
Naibu Kamishina wa polisi Ahmed Msangi anatoa onyo kwa watu wote wenye tabia za
kujichukulia sheria mkononi kuacha mara moja kwani ni kosa kisheria na wale
wote waliohusika endapo watabainika hatua kali za kisheria zitachuliwa dhidi
yao.
Sambamba na hilo pia anawataka
wananchi watambue kwamba dhamana ni haki ya mtuhumiwa endapo tu kama kesi
anayohumiwa nayo inadhaminika hivyo wananchi waache tabia ya kujichukulia
sheria mkoni pindi watuhumiwa wanapofikishwa mahakamani na kuachiliwa kwa
dhamana kwani ni hitaji la kisheria wakati shauri linaendelea mahakamani.
Aidha anawaomba wananchi kuendelea
kutoa taarifa mapema za wahalifu ili waweze kukamatwa na kufikishwa katika
vyombo vya sheria.
IMETOLEWA NA:
DCP: AHMED MSANGI
KAMANDA WA POLISI (M) MWANZA.
DCP: AHMED MSANGI
KAMANDA WA POLISI (M) MWANZA.
Nyumba Mbili Zachomwa Moto Jijini Mwanza Na Wananchi Wenye Hasira Kali....RPC Msangi Atoa Onyo
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 25, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment