Watu kukata tamaa ya maisha, wivu wa mapenzi na ulevi ni
miongoni mwa sababu za watu 65 kujiua katika kipindi cha miaka miwili mkoani
Geita
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kila mwaka
zaidi ya watu 800,000 hujiua duniani
Katika ripoti yake, WHO inasema kwamba kitendo cha watu
kujiua hutokea katika rika zote bila kujali umri na kwa mwaka 2015 pekee,
kujiua kulishika nafasi ya pili kwa vifo vyote duniani hasa vya vijana wa umri
wa kati ya miaka 15-29
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, kamanda wa
Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema watu 65 walijiua mkoani humo
kuanzia mwaka 2017 hadi Julai 2018
Alisema mwaka 2017 watu 43 walijiua, wengi wakiwa ni kwa
kujinyonga. Alisema tangu Januari hadi Julai mwaka huu, watu 22 wamejiua
Mwabulambo alisema hayo alipokuwa akizungumzia tukio la hivi
karibuni la mfanyabiashara wa madini kujiua kwa kujipiga risasi akiwa kwenye
nyumba ya kulala wageni ya Flamingo eneo la Buseresere wilayani Chato
Kamanda huyo alisema takwimu zinaonyesha wilaya za Chato na
Geita zinaongoza kwa matukio hayo katika kipindi hicho yakiwa 24. Matukio ya
watu kujiua wilayani Chato mwaka jana yalikuwa 18 na mwaka huu yamefikia sita,
wakati Geita ikiwa na matukio 10 mwaka huu tofauti na 14 ya 2017
Mwabulambo alisema Mbogwe ina matukio tisa huku matano
yakiwa ya mwaka jana na manne mwaka huu, ikifuatiwa na Bukombe ambako watu
watano wamejiua kati ya hao wanne mwaka 2017 na mmoja mwaka huu. Wilaya ya
Nyang’wale ina matukio matatu, mawili yakiwa ya 2017 na moja mwaka huu
Kamanda alisema matukio ya watu kujiua kwa wivu wa mapenzi
takwimu zinaonyesha mwaka jana yalikuwa matano na Januari hadi Julai yako sita
Alisema matukio ya watu kujiua kwa kukata tamaa ya maisha
mwaka 2017 yalikuwa saba na sasa yako matatu
Kamanda Mwabulambo alisema watu wanne walijiua kutokana na
magonjwa ya akili, matukio mawili mwaka jana na mawili mwaka huu
Alisema matukio yanayohusisha ulevi yalitokea mawili 2017 na
kuanzia Januari hadi Machi hakuna lililotokea
Kuhusu matukio ya watu kujiua kwa sababu nyingine, alisema
yalikuwa 38, kati ya hayo 27 yalitokea mwaka jana na mwaka huu yako 11
Kamanda Mwabulambo alisema mtu anapofikia uamuzi wa kujiua
ni wa kuonewa huruma huku akiiomba jamii kuwasaidia kabla ya kufikia hatua ya
kujitoa uhai. Alisema watu wa aina hiyo wanahitaji ushauri wa kisaikolojia
Pia, aliitaka jamii kuwa karibu na ndugu zao wanapowaona
wana msongo wa mawazo
Sababu tatu za watu 65 kujiua Geita kwa miaka miwili
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 23, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment