Nyumba ya ‘Polisi’ yafungwa pingu

Chumba kimoja cha biashara kati ya viwili vilivyokodishwa na askari wa Jeshi la Polisi eneo la Sinza Afrikana wilayani Kinondoni kilifungwa kwa muda kwa kutumia pingu baada ya kuibuka mgogoro kati ya askari huyo na mwenye nyumba

Hata hivyo, si askari huyo wala mmiliki anayejua pingu hizo za kudhibitia wahalifu zilifungwa na nani mlangoni baada ya wote kuhojiwa na gazeti hili jana

Mlango wa chuma wa chumba hicho ulifungwa kwa pingu baada ya mpangaji anayejulikana kwa jina la Glory Masawe kuingia katika mzozo na Jerome Kaale, mmiliki wa vyumba hivyo vya biashara vinavyojulikana zaidi kwa jina la fremu

Mpangaji huyo ambaye ni askari alikuwa akidai arejeshewe fedha zake baada ya kutaarifiwa na Manispaa ya Kinondoni kuwa eneo hilo halitakiwi kufanyiwa biashara na mzozo ulipozidi, chumba hicho kikafungwa kwa pingu na baadaye Julai 9 askari huyo aling’oa milango, madirisha na mita ya umeme, katika kile kilichoonekana kuwa ni kutaka kufidia fedha zake ambazo ni Sh1.8 milioni za pango

“Kabla ya kuja kung’oa milango, madirisha na mita ya umeme mwezi Mei mlango ulifungwa kwa pingu,” alisema Kaale jana

Alisema walisaini mkataba Desemba Mosi mwaka jana na umeisha Juni Mosi mwaka huu

“Kama aliambiwa hivyo (kuwa eneo halitakiwi kufanyia biashara)ilibidi afuate taratibu za kuvunja mkataba, lakini alikaa hadi mkataba umeisha leo (ndio) anadai pesa yake. Kwa nini?” alihoji Kaale
“Ni makubaliano tu si kutumia nguvu na uonevu. Mfano mwanzoni mwa mwezi Mei nilikuja hapa asubuhi nikakuta mlango umefungwa na pingu. Baada ya kuuliza kwa nini anaweka vitu vya hatari kama hivyo, naambiwa hainihusu.”

Lakini Glory alikana kuwa ndiye aliyefunga pingu hizo mlangoni

“Sijawahi kufanya hivyo. Ndiyo kwanza nalisikia hilo leo mimi sijawahi kabisa,” alisema Glory alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu suala hilo

Msaidizi wa mkuu wa kituo wa polisi kituo cha Mabatini wilayani Kinondoni, Rijuo Said alisema kesi hiyo ipo kituoni, lakini haikuwa kazi ya polisi na kushauri suala hilo lishughulikiwe na uongozi wa Serikali za Mitaa

“Walivyokuja hapa nikawasikiliza lakini nikasema kuwa hili mbona linaweza kushughulikiwa huko,” alisema Said.

 “Kimsingi hatupendi sana kuingilia malalamiko ya madai. Ingekuwa jinai tungelishughulikia sisi, hata kama kuna vitu vingine ambavyo atahitaji msaada tunaweza kumsaidia.” Alisema

Katibu wa soko la Sinza2 lililopo Afrika Sana, Honest John alisema mpangaji huyo alifika Julai 9 na gari, akidai anataka aondoke na milango kwa kuwa anamdai mwenye fremu

Alisema pamoja na kumshauri atafute suluhisho na mwenye nyumba, hakukubali akaendelea na mpango wake


Nyumba ya ‘Polisi’ yafungwa pingu Nyumba ya ‘Polisi’ yafungwa pingu Reviewed by KUSAGANEWS on July 23, 2018 Rating: 5

No comments: