Obama viongozi waache ubabe


Afrika Kusini . Rais mstaafu wa Marekani Barack Obama amesema viongozi wa sasa wanatawala kwa ubabe huku wakiikandamiza demokrasia na kuuweka ulimwengu njia panda

Amewataka viongozi hususan wanasiasa kuyafanyia kazi mawazo ya aliyekuwa kiongozi wa Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela ambaye alipinga ubaguzi wa rangi kwa nguvu zake zote

Amesema hayo jana  alipokuwa akihutubia katika mhadhara wa kila mwaka wa Nelson Mandela nchini Afrika Kusini ambao huandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya kukumbuka kuzaliwa kwa kiongozi huyo wa zamani.

 ‘’Enzi hizi ni za watawala wababe,  hivyo hawaipi uzito kabisa demokrasia kwani wanaikandamiza,” amesema Obama.

 Huku akionekana kumkosoa mrithi wake Donald Trump, Obama amesema watawala wenye nguvu wanahujumu karibu kila taasisi ya Serikali ambayo huleta maana kwa demokrasia

Obama amesema kiongozi huyo aliyepambana dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini mwake  alikuwa mtu shujaa kweli na anayetakiwa kukumbukwa katika historia

Ametoa  wito kwa watu kujifunza mengi zaidi kutoka kwa uongozi wake na kujenga jamii ya kuvumiliana ambapo demokrasia  na  jamii vinathaminiwa na kusema kwamba vijana wanatakiwa kutekeleza mchango muhimu katika kuangusha watawala wa kiimla.

 Obama amesema kuna kizazi cha watu ambao wamekulia na kulelewa katika ulimwengu uliojaa uhuru zaidi na wa kuvumiliana
"Ni lazima tuanze kwa kukubali kwamba sheria zote ambazo huenda zilikuwapo kwenye vitabu …. Miundo ya zamani ya hadhi na mamlaka na unyanyasaji vyote viliangamizwa, lakini havikuangamizwa kabisa," amesema

Obama amesema Marekani changamoto dhidi ya utandawazi mwanzoni zilitoka kwa wanasiasa wa mrengo wa kushoto na kisha zikaanza kutokea kwa wanasiasa wa mrengo wa kulia

Ahadi  hewa Amesema madhara ya kudorora kwa uchumi wa dunia mwaka 2008  na kutoaminika kwa wasomi na watawala  ndiyo hasa chanzo cha ahadi zilizotolewa kwa watu kuwa hewa tu
"Siasa za kuwatia watu hofu na kutoridhika na kuwa na misimamo mikali zilianza kuwavutia watu. Na siasa za aina hiyo sasa zinashika kasi," amesema Obama

Amesisitiza kwamba anapenda aeleweke kwa watu yeye hasemi hayo kwa lengo la kuwatisha watu bali anachokielezea ni ukweli.
 "Viongozi wenye nguvu kuu kisiasa wameanza kuchipuka...wale walio madarakani hujaribu kuhujumu kila taasisi au utamaduni unaoipatia demokrasia maana," amesema

Obama pia amesema watu wanatakiwa kuachana na mtazamo wa kusaidiwa tu na badala yake walio na mali na mamlaka wafikirie kuwekeza zaidi katika jamii zilizotengwa

Inaonekana ni kama tunaelekea kwenye siasa za kukaripiana, mapambano ya kuhakikisha haki za msingi bado hayajakamilika kwa kweli. Ni lazima tuwe macho dhidi ya watu wanaojaribu kujitukuza kwa kuwashusha hadhi wengine," amesema

Mandela ameongoza kampeni dhidi ya sera za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini na kufungwa miaka 27 gerezani

Alikuwa rais wa kwanza mweusi mnamo mwaka 1994 baada ya kushinda uchaguzi wa kwanza wa demokrasia wa nchi hiyo, na ambao watu wa kila rangi walikubaliwa kushiriki. Alifariki dunia mwaka wa 2013 akiwa na miaka 95

Obama amemsifu Mandela kwa kujaribu kumaliza ubaguzi wa rangi kupitia majadiliano na kufikia upatanisho miongoni mwa watu wa kila rangi
Obama viongozi waache ubabe Obama viongozi waache ubabe Reviewed by KUSAGANEWS on July 18, 2018 Rating: 5

No comments: