Chadema wakata rufaa NEC

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Mara kimekata rufaa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kupinga kuenguliwa kwa mgombea wao wa udiwani katika kata ya Manchira wilayani Serengeti

Katibu wa Chadema mkoa wa Mara , Chacha Heche amesema leo Julai 18, 2018 kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kufanya kikao na kujiridhisha kuwa msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo alikiuka kanuni za uchaguzi

Amesema moja ya sababu iliyomwondoa ni kuwa aliwahi kufungwa kwa kosa la mauaji, madai ambayo alisema si ya kweli

"Mgombea wetu Timani Shaweshi hakuwahi kufungwa bali alikaa mahabusu kwa zaidi ya miaka mitano kwa tuhuma za mauaji akaachiwa baada ya kukosekana kwa ushahidi na vielelezo," amesema Heche

Pia, amesema barua ya pingamizi ilipelekwa kwa katibu wa chama wakati mgombea aliweka anuani yake

Heche amesema hata alipowasilisha majibu ya pingamizi hapakuwa na mhusika wa tume licha kwamba ulikuwa ni muda wa kazi na kulazimika kuwasiliana na NEC na kuagizwa wapeleke rufaa moja kwa moja

"Tulishatuma maana kuna makosa ya makusudi aliyofanya msimamizi wa uchaguzi jimbo, maana alitoa barua ya kumuengua mapema kabla ya muda wa rufaa na kumpa katibu wa chama badala ya mgombea," amesema

Msimamizi wa uchaguzi huo, Juma Hamsini amesema mgombea huyo hakusaini rejesta kwa mjibu wa sheria, ikiwemo kutojaza kikamilifu fomu yake

"Kuna fomu mbili alitakiwa kujaza moja kwenda kwa anayempinga na kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo. Yeye hakufanya hivyo," amesema Hamisi

"Kwanza alidanganya tume kuwa hajawahi kushitakiwa lakini baada ya kuwekewa pingamizi akakiri kuwa alishitakiwa na kuachiwa kwa sababu hizo alipoteza sifa za kugombeana na hivyo kumtangaza Charles Muyuga (CCM) kuwa diwani mteule," amesema

Hata hivyo, Heche amesema kutokutengenezwa kamati za rufaa ambazo ziko kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ambayo hutumika kama mahakama kusikiliza pande zote ni chanzo cha matatizo mengi katika chaguzi

Katika Jimbo la Serengeti kata mbili za Manchira na Ikoma zilitakiwa kufanya uchaguzi wa marudio baada ya waliokuwa madiwani wake kupitia Chadema kujiuzulu na kuhamia CCM.

 Katika kata ya Ikoma, Michael Kunani wa CCM amepita bila kupingwa kutokana na mgombea wa Chadema, Kennedy Josephat kushindwa kurejesha fomu ya uteuzi kwa kile kinachodaiwa katibu wa chama aliyejiuzulu kuhujumu chama


Chadema wakata rufaa NEC Chadema wakata rufaa NEC Reviewed by KUSAGANEWS on July 18, 2018 Rating: 5

No comments: