NEC yawalima barua Chadema


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeiandikia barua Chadema ikitaka utambulisho wa mawakala watakaosimamia uchaguzi wa marudio wa jimbo la Buyungu na Kata 77 Agosti 12, 2018

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 18, 2018 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila amesema barua hiyo inawaelekeza wakala atatambulishwa kwa msimamizi wa uchaguzi kwa barua ya chama, picha mbili za pasapoti na kitambulisho chochote chenye picha

Hata hivyo, Kigaila amekosoa uamuzi huo wa Tume kwa madai hawajapewa mwongozo wowote wa mawakala siku ya kupiga kura, jambo linaloweza kusababisha sintofahamu kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa jimbo la Kinondoni

"Kwenye uchaguzi uliopita wa Kinondoni mawakala wetu waliambiwa hawana utambulisho wowote kutoka Tume, jana wametuandikia barua wanatoa masharti lakini hawasemi siku ya uchaguzi itakuwaje, mawakala watatambuliwa vipi," amesema Kigaila

Kigaila amesema Tume hiyo haijayafanyia kazi malalamiko ya Chadema licha ya kuandikiwa barua na Katibu Mkuu wake, Dk Vincent Mashinji kukutana na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk Athumani Kihamia

Amesisitiza wataendelea kupigania haki ya wagombea wa chama hicho na wanakwenda kushinda kwenye uchaguzi huo

"Mkurugenzi ametuambia ili kuepusha makosa yaliyofanyika kwenye uchaguzi wa Kinondoni mawakala waje na vitambulisho. Kumbe wanatambua Uchaguzi wa Kinondoni ulikuwa na kasoro lakini hawajamchukulia hatua zozote msimamizi wa uchaguzi wa Kinondoni kwa kuharibu uchaguzi," amesema

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi amewataka polisi kufanya kazi zao badala ya kuingilia uchaguzi kwa kuwakamata wagombea wa Chadema

"Kuna kata 18 ambazo wagombea wa Chadema wameenguliwa. Mpaka sasa kuna maeneo watu wetu wamekataliwa rufaa zao, kwa mfano Rombo. Tumeandika malalamiko yetu kwa Tume," amesema Munisi.

NEC yawalima barua Chadema NEC yawalima barua Chadema Reviewed by KUSAGANEWS on July 18, 2018 Rating: 5

No comments: