Mkurugenzi wa Kampuni ya Halihalisi inayochapisha magazeti
ya Mawio, Mwanahalisi na Mseto, Saed Kubenea amesema watarudi Mahakama ya
Afrika Mashariki kuomba kibali cha kuchapisha gazeti la Mseto baada ya Serikali
kutoondoa zuio la uchapishaji
Mahakama hiyo Juni 21, 2018 ilitoa amri kwa Serikali
kuhakikisha inachukua hatua stahiki ili gazeti hilo lirudi mtaani ikisema
lilifungwa kinyume cha sheria
Gazeti hilo lilifungiwa Agosti 10, 2016 kwa miezi 36
ikielezwa ni kwa kuandika habari za upotoshaji, uchochezi na uongo,
zisizozingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari
Kubenea akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili
Julai 22, 2018 amesema Serikali sasa inapaswa itoe ushirikianao kwa Mahakama
ili usikilizaji wa kesi za madai na jinai ufanyike kwa haraka kuliko
kucheleweshwa bila sababu za msingi
"Tungekuwa tuna mitambo yetu tungekuwa tumechapisha
tangu siku ambayo Mahakama imetengua agizo hilo lakini nashindwa kwa sababu
wachapishaji wanahitaji hati ya usajili wa gazeti kabla ya kuchapishia,”
amesema Kubenea
“Lakini hicho kibali tutakachopewa na Mahakama kitatumika
kama kigezo cha sisi kuchapisha na kuuza gazeti," ameongeza Kubenea ambaye
pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema).
Wakili kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
Fulgence Massawe amesema kitendo cha kuchelewa kutengua uamuzi wa kufungiwa kwa
gazeti hilo ni ukiukaji wa sheria ambao unapaswa kuangaliwa
"Siyo kwamba Serikali haina taarifa, siku hukumu
inasomwa walikuwa na mawakili wa upande wa Serikali ambao walisikia na kuahidi
kutekeleza maagizo," amesema Massawe na kuongeza
“Serikali tayari imeandaa notisi ya rufaa kupinga hukumu
hiyo na itaiwasilisha Jumatatu lakini jambo hilo halizuii kuanza kwa
utekelezaji wa hukumu iliyotolewa,” amesema
Kubenea kurudi mahakamani kupigania gazeti lake
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 22, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment