Watu watano wamehukumiwa kunyongwa mapema wiki hii baada ya
kupatikana na hatia ya kumuua mfanyabiashara tajiri wa Mirerani, Erasto Msuya
Je, wajua kinachofuata baada ya hukumu hiyo? Ni hukumu
kutekelezwa?
Pengine hujawahi kufikiria ni nini hufuata na pengine
unaweza kuwa mmoja wanaoamini kuwa kinachofuata ni utekelezaji wa hukumu
Katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika Juni 28, Jaji
mstaafu Thomas Mihayo alieleza umuhimu wa hukumu za aina hiyo kubaki kwenye
sheria, akisema kuna mauaji mengine yanatia uchungu na pia kuzungumzia mambo
mengine yanayoendelea katika nyanja ya sheria nchini
Pia akaeleza nini hufuata baada ya mahakama kuhukumu kifo.
Alisema mtu anapohukumiwa kunyongwa hadi kufa, Rais ndiye anayesaini
utekelezwaji wa hukumu hiyo
“Lakini kunakuwa na automatic appeal (rufaa ya moja kwa moja
bila ya mtuhumiwa kuomba),” alisema Jaji Mihayo
Alisema baada ya hapo kamati maalumu inakuwapo kwa ajili ya
kuangalia mwenendo wa maisha ya nyuma ya aliyehukumiwa ili kumshauri jaji
aliyetoa hukumu aone nini kifanyike
“Kamati hiyo inakuwa na baadhi ya viongozi wa juu wa ulinzi
na usalama ili kuona kama inaweza kumshauri jaji abadili uamuzi wake, lakini
akiona haifai anasema acha sheria ichukue mkondo wake,” alisema Jaji Mihayo
Wakili wa kujitegemea John Mallya alisema iwapo jaji
atasimamia uamuzi wake, basi hukumu hiyo itapelekwa kwa Rais kwa ajili ya
kusainiwa ili adhabu ya kunyongwa iweze kutimizwa
Mallya alisema Rais akisaini, hukumu hupelekwa kwa mnyongaji
wa Taifa kwa ajili ya kutekeleza kilichoamuliwa.
“Yeye atapanga siku
gani ya kunyonga na anatakiwa amtaarifu mnyongwaji siku 90 kabla ya kutekeleza
adhabu hiyo,” alisema
Alisema baada ya mnyongwaji kupewa taarifa, ana haki ya
kusema kile anachotaka kabla ya siku hiyo kufika
“Ana haki ya kusema kama anahitaji kiongozi wake wa dini kwa
ajili ya kutubu dhambi, au aitiwe ndugu zake au chochote,” alisema
Alisema siku ikifika aliyehukumiwa hunyongwa kwa kutumia
kitanzi hadi anakufa
“Akishakufa ndugu watataarifiwa waje kuchukua mwili kwa
ajili ya kuzika au vinginevyo itakavyokuwa,” alisema Mallya
Hata hivyo, pamoja na adhabu hiyo kuwapo nchini, marais
wamekuwa hawasaini hukumu hizo, akiwamo wa sasa Dk John Magufuli ambaye hivi
karibuni aliamua kuwasamehe wafungwa 61 waliokuwa wakitumikia adhabu hiyo
Hata hivyo, Jaji Mihayo alisema kutotekelezwa kwa adhabu ya
kifo si sababu ya kuitoa kwenye sheria
“Kuna marais ambao hawapendi kutoa adhabu hiyo hivyo si
lazima,” alisema
“Lakini kunawaumiza wafungwa wa adhabu hiyo (kwa kuwa)
wanakaa muda mrefu kusubiri na ndiyo maana Rais wa sasa ameamua kuwasamehe kwa
kuwa wanateseka kuwa na ile adhabu kichwani.”
Jaji huyo mstaafu alisema Rais anaweza kusamehe adhabu
yoyote inayotolewa na ndiyo maana wakati mwingine anaweza kupunguza ile ya
kunyongwa na kuwa ya kutumikia kifungo cha maisha jela
Kinachofuata waliohukumiwa kwa kumuua bilionea Msuya
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 27, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment