Washtakiwa watano waliomuua kwa makusudi mfanyabiashara
tajiri wa madini Mirerani mkoani Manyara na Arusha, Erasto Msuya, wamehukumiwa
kunyongwa huku maelezo yao ya kukiri kosa yakiwachangia adhabu hiyo.
Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa jijini
Arusha, aliuawa kwa kupigwa risasi na bunduki ya kivita ya Sub Machine Gun
(SMG), Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai
Katika eneo la tukio kuliokotwa maganda ya risasi za SMG 22,
huku gari yake aina ya Range Rover namba T800 CKF, bastola zake na simu zake
mbili zikikutwa eneo la tukio
Watu hao waliohukumiwa kunyongwa ni mshtakiwa wa kwanza,
Sharifu Mohamed; mshtakiwa wa tatu, Mussa Mangu; mshtakiwa wa tano, Karim
Kihundwa, wa sita Sadik Jabir na wa saba, Ally Majeshi
Hata hivyo, Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama Kuu alimuachia
huru mshtakiwa wa pili, Shwaibu Jumanne maarufu kwa jina la Mredii, kutokana na
kukosekana kwa ushahidi wa kumtia hatiani kwa kosa la mauaji
Akichambua ushahidi dhidi ya washtakiwa hao, Jaji Maghimbi
alisema mahakama imezingatia maelezo ya kukiri kosa na ya ungamo ya washtakiwa
wanne na pia ushahidi huru kuunga mkono
Maelezo ya kukiri kosa ambayo yalipokewa mahakamani na
kusomwa yakieleza mpango mzima wa mauaji hayo na ushiriki wa kila mmoja ni ya
Sharifu, Mangu, Karim, Sadick na Majeshi
Awali kesi hiyo ilipofunguliwa Mahakama ya Hakimu Mkazi
Moshi mwaka 2013, ilikuwa na washtakiwa wanane, akiwemo mfanyabiashara mwingine
tajiri, Joseph Mwakipesile au Chussa
Hata hivyo Aprili 16, 2014, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP),
alimfutia mashtaka mfanyabiashara huyo akitumia kifungu Na 91 cha Sheria ya
Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) ya 2002
Mei 14, 2018, Jaji Maghimbi alimuachia huru mshtakiwa wa
nne, Jalila Zuber baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 32 wa mashtaka na
vielelezo 26, na kumuona hana kesi ya kujibu
Alichoeleza mshtakiwa wa kwanza Katika maelezo yake ya
kukiri kosa yaliyoandikwa na Inspekta Damian Chilumba, mshtakiwa wa kwanza,
Sharifu Athman, alieleza mpango mzima ulivyofanyika hadi kuuawa kwa Msuya
“Mwishoni mwa mwezi Julai 2013 nilimtembelea Chussa na
akaniambia Sharifu naomba uniangalizie shughuli zangu za madini zisikwame na
ikibidi kugharamia shughuli za uendeshaji,”
“Wakati najiandaa kuondoka Chusa aliniomba nimsogelee ana
jambo nyeti ambalo hataki watu wengine wasikie,”ananukuliwa mshtakiwa huyo wa
kwanza akisema katika maelezo hayo
Akinukuu alichoambiwa, shahidi huyo alidai, “unajua mateso
yote haya ninayoyapata yanatokana na Msuya. Msuya ndiye amehonga niunganishwe
kwenye kesi ya mauaji wakati sikuhusika,”
“Kwa sauti ya chini Chusa aliniambia unajua wewe ni rafiki
yangu nisaidie kumuondoa duniani Msuya. Nilipigwa na butwaa. Kasema fanya
ufanyavyo ndani ya siku chache Erasto Msuya afe.”
Mshtakiwa huyo katika maelezo hayo anadaiwa kumweleza Chussa
kuwa asingeweza kumuua Msuya kwa kuwa hana ugomvi naye na ni mfanyabiashara
mwenzake, kauli iliyoonekana kumuudhi Chusa
“Alibadilika na kuonyesha hasira akaniambia kama umeshindwa
basi nikitoka nitafanya mwenyewe. Baada ya kutafakari nikaona nikimwacha afanye
mwenyewe angeniua kwa sababu alishaniweka wazi
“Siku nyingine nilienda kumtembelea aliniuliza tena na
kuniambia au rafiki yangu unataka kunisaliti? Nilimuuliza anataka nifanyeje
hiyo kazi, akasema niwe mfadhili wa kazi yote akitoka atanirudishia”. Katika
maelezo hayo, mshtakiwa anadaiwa kueleza kuwa Chusa alienda mbali na kumweleza
kuwa kuna kijana anaitwa Mredii (Shaibu Jumanne, mshtakiwa wa pili) ametoka
gerezani ashirikiane naye
“Mimi na Mredii tulionana Mirerani nikamuuliza kama amepewa
maelekezo yoyote na Chussa, akasema ni kweli ana maelekezo ya kutekeleza mpango
mzima wa mauaji,” anadaiwa kueleza hivyo Sharifu
“Tuliondoka kwenda Babati na kuonana na Chussa na lengo la
kwenda ni kutaka anithibitishie Mredii aliyemtuma kwangu ndio huyo, naye
akathibitisha ndio amemwagiza kutekeleza mauaji hayo
“Mredii aliniambia ngoja atafute watu wa kazi anaowajua na
ataleta gharama za kazi nzima. Baada ya siku mbili Mredii alikuja Arusha na
kuniambia tayari ameshapata mtu mmoja
“Nilienda nikakutana nao na Mredii akanitambulisha huyo mtu
mwingine kuwa ni Ally Majeshi (mshtakiwa wa saba). Ally Majeshi aliniambia
kikosi kitahitaji kuwa na watu wanne.”
Katika maelezo hayo, mshtakiwa huyo anadaiwa kueleza kuwa
Majeshi ndiye aliyetoa wazo la kusajiliwa kwa laini mpya na kununua pikipiki
mbili na baada ya hapo ndio watafute silaha
Kwa mujibu wa maelezo hayo, mshtakiwa huyo anadaiwa kueleza
kuwa Majeshi alifanya mawasiliano na watu wengine wawili na siku iliyofuata
alikutana nao Shamoo Guest House
“Siku iliyofuata tulikutana Shamoo Guest House
(inayomilikiwa na Sharifu) na ndipo nilitambulishwa kwa Sadik (Jabir-mshtakiwa
wa sita) na Karim (Kihundwa - mshtakiwa wa tano), ”anadaiwa kueleza Sharifu
“Walisema wanahitaji usafiri na nikawapa gari yangu aina ya
Toyota Landcruicer LX pamoja na dereva wangu Mussa (Mangu-mshtakiwa wa tatu)
wakaenda Namanga kutafuta silaha
“Zilitengenezwa laini mpya sita na kununuliwa simu mpya sita
zilizosajiliwa kwa jina la Adam Leani. Ally Majeshi ndio aligawa simu hizo.
Zililetwa pikipiki King Lion nyeusi na Toyo nyekundu
“Mredii, Sadick na dereva wangu ndio waliokwenda Namanga kwa
ajili ya kukodi silaha, lakini siku hiyo haikupatikana ilibidi walale. Siku
iliyofuata niliwapelekea Sh4 milioni za kukodi silaha. Siku hiyo walileta SMG
na ilipelekwa nyumbani kwangu nikaihifadhi hadi siku ya tukio. Siku moja kabla
ya tukio yaani tarehe 6/8 tulikutana wote Shamoo Guest House kukamilisha
mipango
“Siku hiyo tulikubaliana tutumie mbinu ya kufanya biashara
ya madini ili kumvuta marehemu. Ally Majeshi aliniambia nitoe jiwe moja (la
Tanzanite) ili aende kufanya biashara na Erasto
“Jioni alienda na jiwe lile wakakubaliana kufanya biashara
siku inayofuata (tarehe 7.8.2013, siku ya mauaji) maeneo ya Bomang’ombe.
Alimwambia lile jiwe wako wawili na mdogo wake.”
Katika maelezo hayo, mshtakiwa anadaiwa kueleza kuwa siku ya
mauaji, pikipiki aina ya King Lion nyeusi iliwabeba Mredii na Sadick wakati
aina ya Toyo ilimbeba Karim na Majeshi
“Majeshi alishukia eneo la Kia-Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Kilimanjaro (makutano ya barabara). Mimi nilikuwa na Suzuki na nilibaki na
Jalila (Jalila Zuberi -mshtakiwa wa nne) ila hakutumika sana. Waliogopa kama
wangemwacha angetoa siri
“Mimi (Sharifu) ndiye nilibeba silaha hiyo kuelekea hadi Kia
lakini tulipofika eneo la King’ori nilikabidhi silaha ile kwa Sadik aliyekuwa
anatumia Toyo (pikipiki) nyekundu,” anadaiwa kueleza
“Niliwaambia watakapomaliza kazi ya mauaji wasichukue
chochote kwani hayo ndio yalikuwa maelekezo ya Chusa. Kaburu alinipigia simu
baadaye na kuniambia kazi ya mauaji imekamilika
“Kaburu ndiye mtu wa karibu na Chusa na ndiye alikuwa
akimhudumia wakati akiwa amelazwa kule Babati na kuna wakati alikuwa akilala
naye na alikuwa akijua mpango mzima wa mauaji.”
Mshtakiwa katika maelezo hayo ananukuliwa akieleza kuwa
Kaburu ndiye aliyekuwa akifuatilia kila hatua ya mipango ya mauaji na yeye
(mshtakiwa) alikuwa akimpa taarifa ili naye ampe Chusa
“Baada ya tukio la mauaji kukamilika tulikutana wachache.
Tulikutana na Mredii na Sadick maeneo ya Hoteli ya City Link na tukajadiliana
kuhusu malipo yao na tathmini ya kazi nzima,” anadaiwa kueleza
Mshtakiwa anadaiwa kueleza kuwa washtakiwa hao walitaka
walipwe pesa zao zote hivyo siku hiyo aliwalipa Sh10 milioni, lakini kabla ya
siku hiyo alikuwa tayari amewapa malipo ya awali ya Sh6 milioni
“Baadaye Majeshi na Sadik walirudi wakataka niwapeleke
Babati. Niliendesha gari kwenda Babati na tulifika saa 3:00 usiku,” mshtakiwa
anadaiwa kueleza hayo katika maelezo yake hayo
“Nilipofika Babati nikaenda moja kwa moja kwa Chusa
(hospitalini alikokuwa amelazwa chini ya ulinzi ) na nikamweleza kukamilika kwa
kazi ya kumuua Msuya na Chusa alifurahi sana.”
Katika maelezo hayo, mshtakiwa ananukuliwa kuandika
uthibitisho wa maelezo hayo kwa mkono wake na kuweka saini na dole gumba
akisema ameyatoa kwa hiari bila kushurutishwa
Alichokiri mshtakiwa wa tatu
Akisoma maelezo ya Mangu, Januari 19, 2016, shahidi wa nane,
Inspekta Herman Mtungi, mshtakiwa anadai kwa aonavyo yeye, kwa asilimia 100
mauaji hayo yalipangwa na kutekelezwa na Sharifu
Katika maelezo yake hayo, Mangu ananukuliwa akisema
anakumbuka Jumamosi moja ambayo hakumbuki tarehe, Sharifu alipeleka majina kwa
mtu aliyemtaja ni Adamu ili akasajili laini za simu
Mshtakiwa huyo anaeleza kuwa alimpelekea Adamu majina hayo
na ilipofika saa 12:00 jioni alimpigia simu ili amfuate kwamba laini hizo
tayari zilikuwa zimesajiliwa
“Nilipomfuata nilimkuta kwa dada mmoja anayesajili simu na
alinikabidhi laini mbili za Airtel na nilizipeleka nyumbani kwa Sharifu na
kumkabidhi,” yanasomeka maelezo hayo
Katika maelezo hayo, Mangu ananukuliwa akisema anakumbuka
Julai 29, 2013 alipigiwa simu tena na Sharifu na kumwelekeza aende kwa Adamu
akamchukulie laini nyingine mbili
Agosti 3, 2013, Mangu katika maelezo hayo anadaiwa kumwambia
Inspekta Herman kuwa alipigiwa simu na mshtakiwa wa kwanza na alipomfuata
alimkuta akiwa na gari aina ya Toyota Noah
Ndani ya gari hilo kulikuwa na vijana wawili ambapo alimtaka
aende na Adamu kumsaidia kununua pikipiki mbili, na pikipiki hizo walizinunua
kwa Sh3.4 milioni na kuzipeleka kwa Sharifu
Pikipiki hizo zilisajiliwa kwa jina la Motii Ndoole ambalo
ni jina lililotumika pia kusajili laini za simu ambazo Adamu aliagizwa
azisajili na baadaye kukabidhiwa kwa mshtakiwa huyo wa kwanza
Mshtakiwa huyo katika maelezo hayo anadai katika siku ya
Jumanne ambayo tarehe haikumbuki, bosi wake alimwita katika hoteli yake ambako
alimkuta na vijana watatu wakifanya mazungumzo
“Alitoka ndani akiwa ameongozana na watu watatu
nisiowafahamu. Mimi ndio niliendesha ile Noah, wale vijana watatu wakawa
wanaulizana nani akafanye naye biashara (Msuya), ” anaeleza Mangu.
“Nilimuuliza Sharifu (mshtakiwa wa kwanza) wanaenda kufanya
biashara gani, akasema wanaenda kumuuzia mawe (madini ya Tanzanite) Erasto
Msuya.”
Katika maelezo hayo, Mangu ananukuliwa akidai Agosti 7,
2013, mshtakiwa alikuja akiwa na gari aina ya Suzuki Vitara ndani yake kulikuwa
na wale vijana aliowakuta na bosi wake jana yake.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, Mangu anadai bosi wake
alimwelekeza aendeshe hiyo Suzuki Vitara kuelekea Moshi, lakini akawa anaongea
na watu kwenye simu kuwa wamsubiri King’ori.
“Tulipofika King’ori,
Sharifu alinielekeza nisimame mahali walipokuwa wamesimama vijana wawili ambapo
niliwatambua wawili kuwa ni wale niliokutana nao jana yake,” anaeleza Mangu
Mangu katika maelezo hayo, anadaiwa kumweleza Inspekta
Ngurukizi kuwa watu hao wanne walikuwa na pikipiki mbili ambazo walizinunua
jana yake na kuzipeleka nyumbani kwa Sharifu.
“Tulianza safari gari yetu ikiwa mbele huku pikipiki zikiwa
nyuma. Tulielekea hadi kwenye miti ya mijohoro (Wilaya ya Hai), Sharifu
aliniambia nisimamishe gari,” ananukuliwa Mangu
Anadai katika maelezo hayo kuwa, baada ya kusimamisha gari,
ilikuja pikipiki nyekundu ambayo ni moja kati ya zile walizonunua ambapo
aliwaambia, “biashara ifanyikie hapa.”
Anaeleza kuwa wao walirudi Arusha na kuwaaacha wale vijana,
lakini alipokuwa kijiweni siku hiyo hiyo saa 8:10 mchana alisikia taarifa kuwa
Erasto amekufa kwa kupigwa risasi Kia
Katika maelezo hayo, mshtakiwa huyo anadai alipata picha
vijana wale ndio waliofanya mauaji hayo kwa vile eneo la mauaji ndilo bosi wake
aliwaambia wale vijana wafanyie biashara hapo
Pia, anadai anaamini ndio waliohusika na mauaji hayo kwa
vile jana yake, bosi wake alimweleza kuwa vijana wale wanakwenda kufanya
biashara na Erasto na asubuhi yake aliona mfuko ukiwa na bunduki
Katika maelezo ya nyongeza aliyoyaandika polisi, Mangu
anadai Agosti 4, 2013, Sharifu alimwelekeza awapeleke watu ambao aliwatambua
baadaye kwa majina ya Mredii na Msoja hadi Namanga
“Nili-pack (egesha gari) upande wa Kenya. Mredii na Msoja
walienda nisikokujua hadi saa mbili usiku waliporudi na kuniambia itabidi
tulale Namanga kwa vile walichokifuata hawajakipata,” anasema mshtakiwa huyo
katika maelezo yake
Siku iliyofuata saa 4:00 asubuhi, Mredii alimpigia simu
kwamba awafuate upande wa Kenya na alipowakuta walimwambia ampigie simu Sharifu
kumjulisha kuwa ‘mzigo’ umepatikana
Hata hivyo, Mangu ananukuliwa akisema alikataa kumpigia simu
bosi wake na ndipo Mredii alipiga simu Sharifu na baadaye alimsikia akisema
atatuma pesa kwa M-Pesa na ameikagua ni nzuri na inapiga
Mangu anadaiwa kukataa kubeba mzigo huo na ndipo Mredii
akampigia simu Sharifu aje mwenyewe kuubeba na wakati wanasubiri pale, alikuja
Msomali mmoja akawa anazungumza nao. “Sharifu alikuja baada ya saa tatu. Mredii
na yule Msomali wakapanda kwenye gari la Sharifu. Nilihisi walichofuata Namanga
ilikuwa ni bunduki, lakini sikujua ni ya aina gani,” anaeleza Mangu
Mshtakiwa wa tano alivyofyatua risasi
Katika maelezo yake ya ungamo (extra judicial statement), ya
mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa yaliyoandikwa Septemba 16, 2013, mshtakiwa
huyo alieleza namna alivyomfyatulia risasi Bilionea Msuya
Maelezo hayo yaliandikwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya
Mwanzo Moshi, Ponsian Claud aliyekuwa shahidi wa 12 na yalipokewa kama kielelezo
na kusomwa mahakamani
Katika maelezo hayo, shahidi huyo alidai mshtakiwa aliyatoa
kwa hiari na kwa ridhaa yake, akieleza alifika eneo la tukio na mshtakiwa wa
sita, Sadick Jabir wakiwa na pikipiki
Mshtakiwa anadaiwa kumweleza mlinzi huyo wa amani kuwa ndiye
aliyefyatua risasi kwa kutumia bunduki aina ya SMG akishirikiana na mtu
aliyemtaja kwa jina moja la Sharifu na kumuua Erasto
Halikadhalika katika maelezo hayo ya ungamo, mshtakiwa
anadaiwa kueleza kwa hiari yake kuwa katika kutekeleza mauaji hayo,
alishirikiana na watu wengine watatu ambao ni Sharifu, Mredii na Sadik
KESI MAUAJI YA BILIONEA MSUYA: Hivi ndivyo mipango ya mauaji ilivyosukwa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 25, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment