JAFO AWATAKA TEMEKE KUKAMILISHA MIRADI YA DMDP KWA UBORA

Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo(katikati) akitoa maelekezo kwa Mkandarasi anayejenga Soko la Kijichi kuzingatia ubora na kujali muda wa kukamilisha mradi huo.
Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo(katikati) akisoma ramani ya  ujenzi wa Stendi ya Mabasi Madogo yenye uwezo wa kuegesha  mabasi  madogo 50 kwa wakati mmoja kinachojengwa kupitia Mradi wa Dmdp.
 
Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo(katikati) akikagua ujenzi wa Soko la Kijichi lenye uwezo wa kubeba  wafanyabiashara 200 linajengwa kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam (Dmdp) chini ya OR TAMISEMI.   

Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo(katikati) akisalimiana na Mbunge wa Temeke Mhe. Issa Mangungu(kulia) wakati wa ziara yake ya kukagua  miradi inayotekelezwa kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam (Dmdp) chini ya OR TAMISEMI.
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo ameendelea na ziara ya kikazi katika Mkoa wa Dar es Salaam na leo ametembelea  Manispaa ya Temeka kukagua maendeleo ya mradi wa uboreshaji wa miundombinu unaotekelezwa kupitia mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es salaam (DMDP).

Akiwa katika ziara hiyo Mhe. Jafo ametembelea na kukagua ujenzi wa masoko ya kisasa yanayojengwa katika Kata ya Kijichi na  Mbagala Kuu, Kituo cha Mabasi madogo sambamba na  Ujenzi wa barabara za mitaa inazojengwa kwa kiwango cha Lami katika Kata hizo. 

Akitembelea maeneo ya miradi Mhe. Jafo alisisitiza ubora wa miradi hiyo pindi itakapokamilika na kuwataka Wakandarasi wajenzi kukahikisha wanaongeza umakini na kuzingatia ubora katika kila hatua ya ujenzi huku wakijali muda uliowekwa wa ukamilishaji wa miradi hiyo.

“Fedha za miradi hii  zipo zinasubiria kazi tu ikamilike lakini sio kukamilika chini ya kiwango. Kinachotakiwa na nyie wakandarasi mnazingatia Mikataba mliongia mwanzoni kabla hamjaanza kazi na kufikia viwango vile vilivyowekwa ili Fedha itakayolipwa iendane na kazi iliyofanyika” alisema Mhe. Jafo.

Akiwa katika Soko la Kijichi Mhe, Jafo amesema ameridhishwa na ujenzi unaondelea ila pia amewataka uongozi wa Temeke pamoja na Mkandarasi kutoa ajira ndogondogo kwa vijana wa maeneo hayo ili nao waweze kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza katika ziara hiyo Mbunge wa Jimbo la Temeke Mhe. Issa Mangungu amesema hatasubiria tena Mhe. Waziri Jafo aje kukagua miradi hii ndio na yeye afike kwenye maeneo hayo bali ataweka ratiba katika kila wiki kuhakikisha anapitia miradi yote kuona maendeleo ya ujenzi na kuhakiki ubora wa miundombinu hiyo itakayoongeza thamani ya Manispaa ya Temeke kwa ujumla.

Akisoma taarifa ya Utekelezaji wa Miradi Mratibu wa Dmdp Manispaa ya Temeke Edward Haule amesema  kwa sasa wameanza kutekeleza  mradi huu katika Kata 8  kati ya 23 zinazohusika na katika maeneo yote hayo wanaboresha miundombinu msingi  ambayo ni kichocheo cha ustawi wa jamii husika.

Katika Kata ambazo zimetembelewa leo na Mhe. Waziri Jafo hususan ni Kata ya Kijichi kazi zinazoendelea ni ujenzi wa barabara 13 zenye urefu wa Km 18.7, Soko moja lenye uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 200, kituo kimoja cha daladala, mfumo wa maji utakaohudumia wakazi zaidi ya 300,000 na taa za barabarani 700  kwa gharama ya Tsh Bil. 22.

Aliongeza kuwa katika Kata ya Mbagala Kuu kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa barabara 12 zenye urefu wa Km 12, soko moja lenye uwezo wa kubeba wafanyabiashara  zaidi ya 290, kituo cha daladala, mfumo wa maji utakaohudumia wakazi zaidi ya 400,000 na Taa za barabarani 600 kwa gharama ya Tsh Bil. 19.

Miradi hii itakayoleta manufaa makubwa kwa Manispaa ya Temeke na kwa wananchi kwa ujumla  inategemewa kukamilika mapema mwezi Januari mwaka 2019.


JAFO AWATAKA TEMEKE KUKAMILISHA MIRADI YA DMDP KWA UBORA JAFO AWATAKA TEMEKE KUKAMILISHA MIRADI YA DMDP KWA UBORA Reviewed by KUSAGANEWS on July 20, 2018 Rating: 5

No comments: