Dakika 100 za Zitto na Lowassa mezani Dar


Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe jana alikutana na kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kubainisha kuwa kinachoendelea kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge na madiwani ni ishara ya kitakachojiri katika Uchaguzi Mkuu 2020

Zitto alieleza hayo muda mfupi baada ya ofisi ya Lowassa kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa mgombea urais huyo wa Ukawa katika uchaguzi wa 2015 alikuwa na mazungumzo na kiongozi wa ACT-Wazalendo.

 “Tumezungumza kwa saa moja na dakika 40, tumeshauriana namna ya kukabiliana na siasa za nchi yetu hivi sasa,” alisema Zitto alipoulizwa na Mwananchi kuhusu walichojadili katika mazungumzo hayo.

 Mgombea kutoweka na kuzima simu; muhuri wa chama kufichwa na baadaye mhusika kujivua uanachama; mgombea kutuhumiwa kwa mauaji hadi kupewa mtihani wa kuandika neno “zinjanthropus”, kukosea kujaza fomu na wengine kuelezwa kuchelewa kurejesha fomu ni baadhi ya matukio yaliyotawala uchaguzi mdogo wa madiwani na wabunge safari hii

Hayo yanatokea huku baadhi ya wagombea wakiwa ni waliojivua uanachama na kuhamia chama kingine na kupitishwa tena kutetea viti vyao

Katika maelezo yake, Zitto alitaka wadau wa demokrasia kuungana kuitetea

Na kama taarifa ya ofisi ya Lowassa iliyotumwa na msaidizi wake, Aboubakar Liongo ilivyoeleza, Zitto na mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema walizungumzia mwenendo wa siasa nchini

“Udanganyifu unaotokea katika chaguzi hizi unatia wasiwasi na ni ishara za wazi za hali tutakayokutana nayo mwaka 2020 (wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao),” aliandika Zitto ujumbe wa simu kwa Mwananchi.

 Kwa mujibu wa taarifa ya Liongo, mazungumzo ya wawili hao yaliyofanyika ofisini kwa Lowassa, yalihusu mwenendo wa hali ya kisiasa nchini na mchango wa vyama vya siasa kwenye maendeleo ya nchi

Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza kwa undani kilichozungumzwa

Kuhusu ushirikiano na Chadema katika Jimbo la Buyungu Zitto alisema, “Mazungumzo na Chadema bado yanaendelea na yanaendelea vizuri. Ninaamini tutashirikiana kwenye chaguzi hizi zinazoendelea.”

Hivi sasa, mchakato wa uchaguzi mdogo katika kata 77 na jimbo moja unaendelea na tayari CCM imeshapata madiwani zaidi ya 20 waliopita bila kupingwa baada ya kuwawekea pingamizi wale wa upinzani na wengine kuenguliwa na wasimamizi kwa madai ya kukosa sifa

Pia wapo walioenguliwa kwa madai kuwa si raia na walioenguliwa kwa madai ya kutoa namba ya simu ambazo wasimamizi walidai si sahihi

Maamuzi hayo yameibua rufaa kutoka Chadema ambayo imesema wasimamizi wamekiuka sheria na taratibu za uchaguzi

CCM wamjibu Mchungaji Msigwa
Mkoani Iringa, mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Albert Chalamila alijibu tuhuma zilizotolewa na mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa ikiwemo ya chama hicho tawala kutumia dola kuibuka na ushindi katika chaguzi hizo

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Chalamila alizungumzia madai ya wagombea wa Chadema kuhujumiwa wakati wa kurejesha fomu, akisema kuwa hakuna kiongozi wa CCM aliyemkamata kwa nguvu mgombea wa Chadema na kumtaka asirejeshe fomu.

 “Fomu zilitolewa kwa mujibu wa sheria na waliokidhi vigezo walichukua na kurudisha, suala la kusema tuliwavamia wagombea wao na kuwanyang’anya nina mashaka nalo, kama ni kweli kwa nini wasiende mahakamani kufungua kesi,” alisema Chalamila

Kuhusu hoja ya Mchungaji Msigwa kuwa Serikali inaminya demokrasia, alisema anashangazwa inapotolewa na mtu aliyekaa bungeni miaka saba kwa madai kuwa mbunge huyo anajua wapi pa kwenda kulalamikia suala hilo

Chadema waisubiri mahakama

Chadema wilayani Tarime mkoani Mara imesema inaiachia mahakama kuhusu pingamizi lililowekwa dhidi ya mgombea wao wa udiwani Kata ya Turwa, Charles Mnanka

Ofisa uchaguzi wa chama hicho ambaye pia ni katibu mwenezi, Amos Chilemba alisema mahakama ndiyo iligonga muhuri nyuma ya picha ya Mnanka na ndiyo inayopaswa kujibu kauli ya mkurugenzi wa uchaguzi aliyewaeleza kuwa msimamizi wa uchaguzi ndiye anapaswa kugonga muhuri katika picha hiyo.

 “Mkurugenzi alisema muhuri wa msimamizi wa uchaguzi ndiyo ulipaswa kugongwa nyuma ya picha ya mgombea wangu, na hili kwa sababu ni la kisheria baada ya kutakata rufaa mahakama itamjibu mkurugenzi,” alisema

Chilemba aliongeza kuwa chama hicho kinatarajia kupata majibu ya rufaa yao waliyokata kutokana na mgombea wao kutoteuliwa kugombea nafasi hiyo, baada ya kudaiwa kutokukidhi vigezo

“Leo kikao kinaendelea kujadili na kutoa maamuzi ya rufaa yetu na tunarajia pengine jioni (jana) tutapata majibu ya nini kimeamuliwa, kesho (leo) tutakuwa na majibu sahihi,” alisem

Imeandikwa na Berdina Majinge (Iringa) na Waitara Meng’anyi (Tarime)

Dakika 100 za Zitto na Lowassa mezani Dar Dakika 100 za Zitto na Lowassa mezani Dar Reviewed by KUSAGANEWS on July 20, 2018 Rating: 5

No comments: