Mbunge wa jimbo la Ngorongoro Mh William Olenasha amesema
mradi wa bwawa la Mbitin lililopo katika kata ya Enduleni ni msaada mkubwa kwa
wafugaji na litakuwa limemaliza malalamiko yaliyokuwepo kabla ya Bwawa hilo
kujengwa.
Olenasha amesema kuwa bwawa hilo lilijengwa na mamlaka
ya hifadhi ya Ngorongoro kupitia agizo la Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Kasimu Majaliwa wakati
alitembelea Wilayani humo na litatumika hata wakati wa kipindi cha ukame.
Amesema wananchi walikuwa wanatembea umbali wa zaidi ya
kilomita 20 kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya mifugo lakini kwasasa
huduma hiyo imeletwa karibu zaidi ili mifugo iendelee kufaidi.
“Unaweza ukakuta majani yapo lakini kama hakuna maji
bado mifugo inapata tabu lakini kuwepo kwa bwawa hilo kutasaidia wafugaji wetu
kutopata shida ambayo ilikuwepo kwa muda mrefu”Alisema Olenasha
Hata hivyo amewataka wananchi kutunza bwawa hilo ambalo ndiyo
mbadala wa wafugaji na tayari litakuja kuwa kivutio kwa watalii kwasababu
wanyama wameshaanza kuja ikiwemo kiboko na kuwataka wananchi wasiharibu
miundombinu kwasababu bwawa hilo limejengwa kwa garama kubwa.
“Yani hapa umeona tayari kuna viboko hawana shida na
wananchi na huko baadae watalii watakuja na itakua kivutio kikubwa”Alisema
Olenasha
Kwa upande wa Mwenyekiti wa halmashauri ya Ngorongoro
Bwana Mathew Siloma amesema kwasasa wanatafuta utaratibu mzuri wa matumizi ya
bwawa hilo ili kulitunza kwasababu mifugo inayotakiwa kutumia bwawa hilo ni
Mingi zaidi ya 10000 kwa siku.
Amesema kwa Kushirikiana na Mbunge William Olenasha pamoja
na wananchi watatafuta namna ya mifugo kutumia maji ikiwa nje kuliko kuingia
moja kwa moja kwenye bwawa kama ilivyo hivi sasa na kuendelea kutoa elimu kwa
wafugaji juu ya matumizi ya bwawa hilo.
Ameongeza Bwawa hilo mpaka kukamili limetumia zaidi ya
shilingi milioni 200 na litakuwa msaada na limepunguza changamoto ya wafugaji.
Mmoja wa mfugaji ambaye alikuwa ananywesha mifugo yake
kwenye bwawa hilo amesema kuwa walikuwa wanapata adha kubwa sana ambapo mifugo
ilikuwa mingine inakufa kutokana na ukosefu wa maji lakini matatizo yameisha.
Kuhusu kulitunza bwawa hilo kwa ajili ya matumizi sahihi
ili lisiharibike amesema wataweka utaratibu wa wafugaji wa kuwajibishana
wenyewe kwa wenyewe endapo atatokea mtu wa kuharibu miundombinu ambayo
imejengwa kwa garama kubwa.
Bwawa la Mbitin lawa Kielelezo cha maendeleo Wilaya ya Ngorongoro
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 19, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment