Aliyejifanya OCD Igunga mikononi mwa polisi

JESHI la Polisi wilayani hapa limewatia mbaroni watu wawili kwa tuhuma za kujifanya maofisa wa jeshi hilo, huku mtuhumiwa mwingine akijifanya Mkuu wa Polisi Igunga

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Emmanuel Nley, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Issa Juma (44) na Lucas Mwasabu (42), wote wakitokea mkoani Shinyanga

Watuhumiwa hao walikamatwa na makachero wa polisi wakati wakijiandaa kufanya utapeli katikati ya mji wa Igunga

Alisema baada ya kuhojiwa na polisi, watu hao walikiri kufanya utapeli katika mikoa ya Singida, Shinyanga, Dodoma

Kamanda huyo alisema upelelezi utakapo kamilika, watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo huku akitoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Tabora kuwa makini na matapeli kama hao kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pindi wanapowatilia mashaka. 

Katika tukio lingine, mkazi wa Kata ya Nkinga, Zainab Mohamed (24), anashikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani Igunga kwa tuhuma ya kumchoma moto mdogo wake wa miaka saba (jina lake linahifadhiwa) baada ya kumtuhumu kuiba Sh. 700 alizokuwa amezihifadhi kwenye mkoba.Kamanda alithibitisha kushikiliwa kwa mtuhumiwa huyo Zainab Mohamed, aliyekamatwa baada ya polisi kupata taarifa za kumchoma moto mdogo wake baada ya kumtuhumu kumwibia kiasi hicho cha fedha.Alisema mtoto huyo amelazwa katika Hospitali ya Rufani Nkinga kwa ajili ya matibabu kwenye mikono yake iliyoungua vibaya

Alisema upelelezi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hiyo.Kamanda Nley aliwaonya wananchi wanaojichukulia sheria mikononi watoto wao wanapofanya makosa na kuwataka wawaonye kwa kuzingatia sheria za nchi. Alisema kuwa polisi itamkamata mtu yeyote atakayebainika kufanya vitendo vya kikatili.Baadhi ya majirani walioshuhudia tukio hilo, walisema mtuhumiwa alimchoma mdogo wake kwa kutumia neti ya mbu.

Majirani hao Chiku Athumani na Salima Ramadhani, walidai mtuhumiwa aliwasha moto neti ya mbu iliyokwishatumika na kumchoma mdogo wake kwenye mikono huku mtoto huyo akiomba msaada kwa majirani ambao walimuokoa na kutoa taarifa polisi

Aliyejifanya OCD Igunga mikononi mwa polisi Aliyejifanya OCD Igunga mikononi mwa polisi Reviewed by KUSAGANEWS on July 24, 2018 Rating: 5

No comments: