Kifo kinaleta
huzuni lakini hakizuiliki. Ndivyo unavyoweza kusema ukimshukuru Mungu kwa yote
katika kipindi hiki cha huzuni kufuatia vifo vya pacha wa kipekee wa Tanzania
walioungana, Maria na Consolata Mwakikuti
Pacha hao
walifariki dunia jana Juni 2, 2018 katika hospitali ya mkoa wa Iringa, huku
taarifa zilizothibitishwa na mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela,
zikibainisha kuwa pacha hao wamefariki wakipishana kwa takribani saa 2
Kifo
hakizoeleki na kila kinapotokea watu huwa na huzuni, kukumbuka mengi
yaliyofanywa na aliyetangulia mbele za haki.
Rais John Magufuli ni miongoni mwa wengi
walioshtushwa na vifo vya pacha hao na kutoa salamu za rambirambi kupitia
mtandao wa kijamii wa Twitter, jambo ambalo limefanywa na watu wengine
wengi kupitia mtandao huo na mingine ya Instagram na facebook
Kupitia
akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter, kiongozi mkuu huyo wa nchi
ameandika, “Nimesikitishwa na kifo cha Maria na Consolata. Nilipokwenda
hospitali waliliombea Taifa. Walikuwa na ndoto ya kulitumikia Taifa.”
“Poleni
familia, Masista wa Maria Consolata na wote walioguswa. Pumzikeni mahali
pema wanangu. Bwana alitoa na bwana ametwaa jina la bwana lihimidiwe.”
Katika mtandao
huo wa Twitter, Naibu Spika Dk Tulia Ackson ameambatanisha picha aliyopiga na
pacha hao alipokwenda kuwatembelea hospitali walikokuwa wamelazwa
“Poleni sana
wazazi na walezi wa watoto hawa. Hakika ni watoto ambao waliweza kutufundisha
kutokata tamaa kwenye maisha na kumshukuru Mungu kwa kila jambo, tutawakumbuka
daima Maria na Consolata kwa alama mliyoiacha, Mungu awapumzishe kwa amani,”
amesema
Mbunge wa
Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete huku akiambatanisha picha ya pacha hao
amesema, “Hebu angalia tabasamu lao...ghafla ulimwengu umefunga macho na
wameachwa katika dunia nyengine. Mungu fundi, Mungu mjuzi, Mungu mpangaji,
pumzikeni kwa amani watoto wazuri...R.I.P Mapacha wasomi.”
Naye Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameandika ,
“hakika vita wamepigana, mwendo wameumaliza. Wapumzike kwa amani Maria na
Consolata. Natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki.”
Katika ukurasa
wake wa Twitter, Katibu Mtendaji wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville
Meena amesema, “Nautafakari wasaa wa mwisho wa watoto Maria na Consolata,
nauona uchungu wa yule aliyebaki hai, akitanguliwa na mwenzake.”
“Wamepigania
uhai wao hadi dakika ya mwisho. Mungu awape pumziko la amani. Ni msiba mkubwa
kwa Taifa letu. Poleni wote mlioguswa na msiba huu.”
Mbunge wa
Mikumi (Chadema), Joseph Haule maarufu Profesa Jay ameandika katika Instagram
yake na kuambatanisha picha akisema, “Dah wapendwa wetu mapacha Maria na
Consolata wametangulia mbele za haki. Raha ya milele uwape eeh bwana na mwanga
wa milele uwaangazie, wapumzike kwa amani, amani.”
Mwenyekiti wa
kamati ya uongozi ya CUF, Julius Mtatiro amesema, “nimepokea kwa masikitiko
makubwa sana msiba wa mabinti zetu na wadogo zetu (mapacha walioungana
Consolata na Maria) ambao wamefariki Dunia katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa
walipokuwa wakitibiwa.”
Msanii wa
Bongo Movie, Steven Mengere maarufu kama Steve Nyerere katika Instagram
ameandika, “hatuna budi kusema kazi ya Mola haina makosa. Nichukue nafasi hii
kuwapa pole ndugu jamaa na familia pamoja na Watanzania wote walioguswa na
msiba huu, hakika sisi tuliwapenda kwa namna moja ila Mungu amewapenda zaidi.”
Vifo vya Maria na Consolata vyagusa kila kona
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 03, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 03, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment