Sugu: Tunazo ilani, ahadi za CCM

Dodoma. Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu amemweleza Spika wa Bunge Job Ndugai kuwa hawana Ilani za uchaguzi za CCM tu bali hata orodha ya ahadi ambazo zimetolewa na chama hicho wakati wa uchaguzi mwaka 2020.

Akichangia bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2018/19, Sugu amesema wakati yeye akiwa gerezani Ndugai alitaka wabunge wote kupewa ilani ya uchaguzi ya CCM

“Sijui kama walipewa (Ilani) lakini mimi nikuhakikishie mheshimiwa Spika kuwa hatuna ilani ya ccm tu bali hata ahadi ambazo mmetoa wakati wa uchaguzi,”amesema

Akazitaja ahadi hizo ambazo ni pamoja na laptop, Sh milioni 50 katika kila kijiji na elimu bure ambayo ipo lakini ni janga tu

“Kuna watu walikuwa wanasema kuwa elimu bure mmeiga kutoka kwa Chadema jambo ambalo ni zuri, lakini kwa jinsi mnavyotekeleza ni kama kweli mmeichukua tu kutoka Chadema,”amesema

Pia amesema akiwa mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii wametembelea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na kubaini kuwa hosteli zimejengwa kwa zaidi ya Sh54 bilioni si Sh10 bilioni kama ilivyotamkwa

“Sijaona ripoti ya CAG (Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali) kuhusu hili, watu wanang’ang’ana zimejengwa kwa Sh 10 bilioni. Tunamdanganya nani?  Kama fedha ni zetu kama Taifa,”amesema

Amesema namba hazidanganyi kuna tofauti kubwa kati ya Sh 10bilioni na Sh 54bilioni. Pia Sugu amemtaka Waziri wa Fedha atakapojibu hoja za wabunge kueleza ni wapi zimeenda Sh1.5 trilioni zilizohojiwa na CAG

“Hakuna mtu anayesema fedha kuwa zimeibiwa, tunahoji zimekwenda wapi? Taifa hili si sebule ya familia si tunapelekana tu,”amesema



Sugu: Tunazo ilani, ahadi za CCM Sugu: Tunazo ilani, ahadi za CCM Reviewed by KUSAGANEWS on June 05, 2018 Rating: 5

No comments: