|
Chanzo cha vifo vya pacha
walioungana Maria na Consolata Mwakikuti ni kusinyaa kwa mapafu hivyo
kusababisha kufeli kwa upumuaji wao
Hayo yalielezwa jana na Mkuu wa
Kitengo cha Magonjwa ya Ndani wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Pauline
Chale ambaye alibainisha kwamba madaktari walifahamu kuwa ugonjwa huo
ungekuwa na madhara kwao
“Kiutaalamu tulijua kwamba ipo
siku presha ya mapafu itapanda na kusababisha shinikizo la moyo na mapafu
ambapo hiyo ndiyo iliyosababisha kifo chao,” alisema Dk Chale ambaye ni
daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mapafu.
|
|
|
Alisema walipowapokea Februari 3
katika kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU), Mwaisela walikofikishwa kutokana
na tatizo la kupumua lililoambatana na maambukizi ya bakteria katika mfumo wa
upumuaji, jopo la madaktari lilifanya kazi mbili kubwa; kuchunguza nini
kilichokuwa kinasababisha homa ya mapafu na kwa nini inashindwa kupona,
“Tulianza kuchukua sampuli ya makohozi kutambua aina gani ya bakteria
wanaoleta tatizo la maambukizi na kubaini ni ‘Klebsiella Pneumoniae’.
Ilitusaidia kujua na kuchagua aina sahihi ya dawa, walitibiwa kwa dawa
stahiki na maambukizi ya mapafu tulijiridhisha yamekwisha.”
Sababu ya upumuaji hafifu
Dk Chale alisema ili kubaini kwa
nini pacha hao walikuwa na upumuaji hafifu, waliamua kufanya vipimo vya
mapafu kupitia kipimo cha CT Scan ya kifua iliyoonyesha umbo la nje la kifua
chao na mfumo wa njia za hewa na mapafu yenyewe ambacho kilionyesha wote
wawili walizaliwa pia na ulemavu wa kifua na uti wao wa mgongo
“Hiyo shepu ya kifua ilichangia na
ushindwaji wa kupumua ambao kwao lilikuwa ni tatizo endelevu na kadri
walivyokuwa wanazidi kukua, upumuaji wao ulikuwa unazidi kuwa hafifu,”
alisema
Alisema katika uchunguzi huo
walibaini hata ukubwa wa mapafu ulikuwa mdogo uliobana hasa kwa Maria ambaye
alikuwa chini ya mwenzake
“Maria alikuwa na mapafu madogo
sana na hata kiwango cha oksijeni kilichoingia kwenye kifua chake kilikuwa
kidogo, hivyo vyote vilichangia kuendelea kusinyaa kwa mapafu yao,” alisema
Dk Chale
Alisema kutokana na hali hiyo,
Muhimbili ilizungumza na familia ambayo ilitaja matatizo ambayo walizaliwa
nayo tangu wakiwa wadogo. “Kwa sababu maambukizi ya mapafu yalikwishapona,
tukajiridhisha wanaweza kuwachukua na kuendelea kuwatunza nyumbani, lakini
inabidi wawe na vifaa maalumu vya kuweza kupumua.”
Alisema Aprili 30 waliwaruhusu
lakini kutokana na maandalizi ya jinsi ya kuwafikisha Hospitali ya Mkoa wa
Iringa waliondoka Mei 17 wakiongozana na muuguzi aliyebobea kuhudumia
wagonjwa mahututi na daktari aliyebobea katika magonjwa ya dharura.</p></div><div><p>Dk
Chale alisema kwa kipindi chote walichokuwa Iringa walikuwa wakiwasiliana na
daktari bingwa, Dk Faith Kundy ambaye aliwapatia maendeleo yao. “Daktari
bingwa Dk Faith alishanipigia simu nikamwelekeza jinsi ya kufanya na aliweza
kutatua kila tatizo lililotokea, lakini saa 72 kabla ya kifo chao hakukuwa na
mawasiliano yoyote na kifo cha namna hiyo kinakuwa ni ghafla huwezi kujua
kitakuwaje, tulijua ikifika hatua hiyo ingekuwa ni ghafla,” alisema
Walikuwa wadadisi katika tiba
Moja ya vitu ambavyo viliwafanya
madaktari wawe makini ni jinsi Maria na Consolata walivyokuwa wakifuatilia na
kutaka kujua kila kitu ikiwamo kwa nini walimeza dawa ya aina fulani na kwa
sababu gani
Dk Chale alisema haikuwa kazi
kubwa kuwaelewesha katika matibabu yao kwani wao pia walikuwa na juhudi kujua
kuhusu afya zao. “Kwa kipindi chote walihitaji kujua matibabu yao yanakwendaje,
kabla ya kufanyiwa tiba fulani kutokana na upeo waliokuwa nao walihoji na
hata wakati mwingine kuomba ushauri pia nini wafanye kuepuka madhara zaidi ya
kifua,” alisema
Walichagua pa kuzikwa
Pacha hao ambao walifariki dunia
Jumapili usiku mjini Iringa, watazikwa kesho kwenye makaburi ya Tosamaganga
Akizungumzia mazishi hayo, Mkuu wa
Shirika la Maria Consolata, Jane Nugi alisema uamuzi huo umefikiwa kutokana
na matakwa ya pacha hao ambao katika uhai wao walichagua kuzikwa kwenye eneo
wanalozikwa viongozi wa madhehebu ya Katoliki na kwamba msiba wao upo kwenye
nyumba ya shirika hilo Kihesa, Iringa kwa kuwa ndio nyumbani kwao. “Wakati
wakiumwa walisema wangetamani kuhifadhiwa tunakohifadhiwa sisi hivyo
watazikwa kwenye makaburi ya Tosamaganga,” alisema
Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard
Kasesela alisema jana kuwa pacha hao wanaandaliwa jeneza moja lenye mfumo wa
watu wawili, misalaba miwili na kwamba watazikwa katika kaburi moja
Kuhusu ratiba, Kasesela alisema
wataagwa kesho katika viwanja vya Rucu ambako pia kutakuwa na ibada maalumu
itakayoanza saa nne ikisimamiwa na maaskofu, Tarcisius Ngalalekumtwa wa Jimbo
la Iringa na Alfred Maluma wa Jimbo Katoliki Njombe
Makamu Mkuu wa Rucu, Pius Mgeni
alisema, “Tumeshaanza maandalizi ya ujenzi wa jukwaa kwa ajili ya kuwaaga.”
Mlezi wa wanafunzi wa Ruco, Martha
Magembe alisema walilazimika kuunda zamu za kulala na kushinda hospitali na pacha
hao baada ya walezi waliokuwa nao Muhimbili kutakiwa kupumzika
Walivyokabidhiwa kwa masista
Alisema walikabidhiwa watoto hao
na wazazi wao mara tu walipozaliwa katika hali hiyo. Kuhusu hilo, familia ya
watoto hao jana ilizungumzia ilivyoshiriki kuwalea licha ya kuwa walikuwa
chini ya uangalizi wa masista
Mama mkubwa wa pacha hao, Anna
Mushumbusi alisema tangu walipozaliwa walikuwa karibu nao wakifuatilia
maendeleo yao lakini hawakuweza kuwachukua kulingana na hali waliyokuwa nayo
Kaka yao wa kwanza, David
Mwakikuti alisema baada ya wazazi wao kufariki walichukuliwa na ndugu upande
wa mama na kwenda kulelewa Bukoba. “Tulilelewa vizuri na kwa upendo ndio
maana leo hii wote tumesomeshwa, wajomba na shangazi zetu hawakutuacha
kabisa,” alisema
Maria na Consolata ni wazaliwa
watatu wakiongozwa na kaka yao David, dada yao Editha na mdogo wao wa mwisho
Jackline
David alisema wakati Maria na
Consolata wakisoma Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha (Rucu), Editha anasoma
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut) na Jackline anajiandaa kuanza
masomo ya sekondari
David ambaye alisoma Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) kozi ya takwimu, anafanya kazi katika shirika
linalojishughulisha na masuala ya kijamii la OM lilipo Dar es Salaam
“Hatukuwa na uwezo wa mawasiliano
zaidi lakini tulikuwa tukiwaomba walezi wetu na kuja kuwatembelea ndugu zetu
ambao kwa wakati wote walikuwa wanalelewa na Shirika la Maria Consolata,”
alisema
David alisema mara ya mwisho
kukutana na Maria na Consolata ni wakati wakiwa wamelazwa Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili
“Nakumbuka wakati nilipoonana na
wadogo zangu waliniambia katika maisha yangu nijitahidi kuwasaidia wengine
wasiojiweza hata kama nilichonacho ni kidogo, kiukweli ninayo mengi ya
kujifunza kutoka kwa ndugu zangu,” alisema
Alisema wamemfundisha kupigania
ndoto zake bila kujali vikwazo vinavyoweza kumsimamisha
Mama mkubwa, Anna alisema walikuwa
wakifuatilia malezi na makuzi yao tangu walipozaliwa
“Taarifa ya kuzaliwa kwao
tuliipata siku za saba baadaye, wakati huo hakukuwa na mawasiliano kama haya
ya sasa kwa hiyo niliondoka Dar es Salaam na kwenda Makete.”
Alisema alipofika na kuuliza
mipango, aliambiwa tayari watoto walikuwa wamekabidhiwa kwa masista wa
Shirika la Maria Consolata kulingana na hali zao
“Tuliheshimu ridhaa ya wazazi wao
waliyoitoa kuwa watoto watakuwa chini ya masista, kazi yetu ilikuwa kuja
kuwaona kila tunapopata nafasi,” alisema
Siri ya majina ya Maria na
Consolata
Wengi wamekuwa na maswali kuhusu
majina ya Maria na Consolata yanayofanana na shirika lililowalea. Sista Jane
alisema baada ya kuzaliwa, wazazi wao waliamua kuwakabidhi kwao kulingana na
hali waliyokuwa nayo na hivyo kutakiwa kuwapatia majina
“Baba yao mzazi Mwakikuti
aliposhauriwa kuwabatiza baada ya kuzaliwa kutokana na hali waliyokuwa nayo
aliomba masista watoe majina hivyo yule aliyekuwepo akawaita Maria na
Consolata,” alisema
Sista Jane alisema waliwalea
watoto hao katika mazingira ya kiimani wamjue Mungu na kuwafundisha upendo
Alisema walipomaliza darasa la
saba katika Shule ya Msingi ya Ikonda, wilayani Makete waliwapeka Kilolo
katika shule yao ya Maria Consolata walikohitimu kidato cha nne
Alisema wakiwa huko waliwajengea
nyumba na kuwaandalia mazingira mazuri ya kuishi huku wakiwa chini ya
uangalizi wa viongozi wa Maria Consolata
Alisema hadi wanamaliza kidato cha
sita katika Shule ya Sekondari ya Udzungwa mpaka wanaingia Rucu walikuwa
karibu nao kwa kila hatua
Imeandikwa na Herieth Makwetta,
Tumaini Msowoya na Berdina Majinge
|
Simulizi chungu ya Maria na Consolota kutoka Muhimbili
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 05, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 05, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment