Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kimesema kinalaani na kupinga ukiukwaji wa Katiba, Sheria na Kanuni mbalimbali
zilizofanywa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Gerson Msigwa Mnamo Mei 21 na
25 mwaka huu kwa kujihusisha na shughuli za chama jambo ambalo ni kinyume na
taratibu -
Hayo yamewekwa bayana na taarifu zilizotolewa
na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje- CHADEMA, John Mrema
mchana wa leo Juni 04, 2018 baada ya kupita siku kadhaa tokea kulipomalizika
vikao vya Halmashauri Kuu Taifa ya CCM vilivyofanyikia ndani ya kumbi za
mikutano zilizopo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
"Tarehe 21 Mei, 2018 ilitolewa
taarifa ya Ofisi ya Rais Ikulu ikiwa imesainiwa na Gerson Msigwa kuhusu tukio
la Mwenyekiti wa CCM Taifa, John Pombe Magufuli kupokea taarifa ya ukaguzi wa
mali za CCM katika Makao Makuu ya Chama hicho Lumumba Jijini Dar es Salaam.
Kwa mara nyingine tena tarehe 25
Mei, 2018 Msigwa kwa kujua au kutojua au kwa kiburi cha malamka alitoa taarifa
kwa vyombo vya habari kwa nafasi yake kama Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu
kuhusu uteuzi wa Wajumbe wawili wa Halmashauri Kuu ya CCM uliofanywa na
Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa John Pombe Magufuli", amesema Mrema.
Aidha, Mrema amesema kwa mujibu wa
Katiba ya nchi Ibara ya 3(1) imetamka wazi kuwa Tanzania ni nchi inayofuata
misingi ya demokrasia na ni nchi ya mfumo wa vyama vingi vya siasa huku Kanuni
maadili ya vyama vya siasa za mwaka 2007, Kanuni ya 5(1) inakataza chama
chochote cha siasa kutumia mamlaka, rasilimali za serikali kwa kujinufaisha
kisiasa.
"Gerson Msigwa kama Mtumishi wa
Umma mwenye wadhfa wa Mkurugenzi kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 anatakiwa na anapaswa
kuzingatia masharti ya Viongozi wa umma. Kifungu cha 21 cha sheria hiyo
kinakataza kiongozi wa umma kutumia mali za serikali isivyoruhusiwa..
Kwa kuwa Msigwa ameendelea
kunukuliwa akisisitiza kuwa yeye ni Msemaji wa Rais na ambaye ni Mwenyekiti wa
CCM huku akijua kufanya hivyo ni kukiuka masharti kama tulivyoeleza, sisi kama
Chama cha siasa tutachukua hatua kwa hilo", amesisitiza Mrema.
Pamoja na hayo, Mrema ameendelea kwa
kusema "tunamtaka Msajili wa Vyama vya Siasa kutumia mamlaka
yake kupitia Kanuni ya 6(1)(d) ya Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa kutoa
tamko dhidi ya ukiukwaji wa Kanuni hizo uliofanywa na CCM kwa kutumia mali za
umma kwa maslahi yao ya kisiasa. Msajili akishindwa kufanya hivyo tutawasilisha
malalamiko rasmi kwake kwa mujibu wa Kanuni ya 6(1)(a) kuhusu ukiukwaji huo.
Tunamtaka Katibu Mkuu Kiongozi au
Tume ya Utumishi wa Umma kama mamlaka za nidhamu kumchukulia hatua Gerson
Msigwa kwa kukiuka masharti ya Utumishi wa Umma kwa kufanya siasa wakati wa
masaa ya kazi na pia kujipa nafasi ya kuwa Msemaji wa CCM huku akijua Chama
hicho kina Msemaji wake".
Kwa upande mwingine, Mrema amesema
endapo hayo yote hayatofanywa na mamlaka husika zilizotajwa basi wao watachukua
hatua zaidi juu ya jambo hilo ambalo linatendwa kinyuma na taratibu.
Msemaji wa Rais Magufuli, kuchukuliwa hatua
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 04, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 04, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment