Wito umetolewa kwa wafanyabiashara
wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi hususani wamachinga kujisajili na
hatimaye kupatiwa vitambulisho maalum kwa lengo la kusaidia biashara zao
kutambulika, kukopesheka na kurahisisha mawasiliano ya usimamizi wa biashara
hizo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa
usajili na utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo uliofanyika leo
mkoani Arusha, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Fabian Daqqaro amesema ni
muhimu wafanyabiashara kutumia fursa hii ya kujisajili ili kurasimisha biashara
zao.
"Ni matumaini yangu kuwa,
wafanyabiashara wengi wadogo wadogo mkoani hapa, mtatumia fursa hii kujisajili
kwa sababu ninafahamu wengi wenu malengo yenu siyo kuwa wafanyabiashara
wadogo muda wote, bali mtakuza biashara zenu na kuwa wafanyabiashara wakubwa na
hii itawezesha kuchangia mapato ya Serikali," amesema
Daqqaro.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa
Kodi za Ndani kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Abdul Zuberi ameeleza
kuwa, zoezi hili la kuwasajili na kuwapatia vitambulisho wafanyabiashara wadogo
limetokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli.
"Ni ukweli usiopingika
kwamba, Rais wetu kwa nyakati tofauti amekuwa akiwapigania na kutaka
wafanyabiashara wadogo wadogo kutambulika rasmi na kupatiwa vitambulisho ikiwa
ni pamoja na kutafutiwa maeneo rafiki ya kufanyia biashara zao," amesema
Zuberi.
Ameongeza kuwa, kutokana na juhudi
hizo za Rais Magufuli, Serikali kupitia Kikao cha Bunge la Bajeti la Mwaka wa
Fedha 2017/2018, ilifanya marekebisho mbalimbali ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi
ya Mwaka 2015 ambapo moja ya marekebisho hayo ni kuwatambua na kuwapatia
vitambulisho maalum wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi na
jukumu hili limekasimiwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Wamachinga kusajiliwa na vitambulisho juu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 15, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment