Wakazi,2,500,kuhamishwa,baada,Nyumba,Mungu,kutapika


Athari za Bwawa la Nyumba ya Mungu wilayani Mwanga kujaa maji kupita uwezo wake zimeanza kujitokeza baada ya wakazi zaidi ya 2,500 kutakiwa kuyahama makazi yao wilayani Same mkoani Kilimanjaro

Mbali ya hao, wengine 1,700 huko Ruvu Mferejini na Marwa, nyumba na mashamba yao yameharibiwa hivyo kuhama, huku kitongoji cha Lesirway kikizungukwa na maji.

Akitoa taarifa ya mafuriko katika bonde la Pangani mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule alisema wameanza kuwahamisha wananchi kwa makundi na kuwapeleka vijiji vya jirani

“Kaya 30 za Kijiji cha Marwa na kaya zaidi ya 50 katika Kijiji cha Mferejini hazina makazi. Mashamba ya mahindi, nyanya, vitunguu na mbogamboga yenye ekari 714 yameharibika,” alisema

Alisema shule za msingi Ngama yenye wanafunzi 218 na Mferejini yenye wanafunzi 513 zimefungwa kutokana na kuzingirwa na maji.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira aliwataka wananchi waliohamishiwa kambini eneo la Rolesha na Bagamoyo kujenga makazi ya muda wakati Serikali ikiangalia namna ya kuwasaidia.

 “Nimezungumza na watu wa chama cha Msalaba Mwekundu wameahidi kusaidia mablanketi. Tutaangalia namna ya kupata vyandarua na mahema,” alisema.

 Ofisa mwandamizi wa Bonde la Pangani, Vendelin Basso alisema walishatoa angalizo kwa wananchi kuhusu mafuriko tangu Mei 6 na kwamba, baadhi ya wakazi wa Ruvu Darajani waliondoka lakini wengine walikaidi

“Kama mlivyoona kuna baadhi ya wananchi wanalazimika kuyahama makazi yao kwa kuvushwa kutoka Ruvu Darajani kuja huku Ruvu Muungano kwa kutumia mitumbwi, hao ni wale waliokaidi,” alisema Basso

Alisema maji katika Bwawa la Nyumba ya Mungu yameongezeka hadi kufikia mita 689.8 kutoka usawa wa bahari na yanapungua kidogokidogo kupitia Mto Pangani ambao nao umejaa hivyo kusambaa katika vijiji vya Marwa na Ruvu-Mferejini.

Mkazi wa Kijiji cha Marwa, Ally Lesunguya alisema mashamba na makazi yao yameathiriwa na mafuriko.

 “Miundombinu ya barabara pia imeharibika, tunalazimika kuvushwa kwa gharama ya kati ya Sh1,000 na Sh2,000 kwa kutumia mitumbwi, huku wengine wakivushwa kwa kubebwa mgongoni,” alisema Lesunguya.
Wakazi,2,500,kuhamishwa,baada,Nyumba,Mungu,kutapika Wakazi,2,500,kuhamishwa,baada,Nyumba,Mungu,kutapika Reviewed by KUSAGANEWS on May 27, 2018 Rating: 5

No comments: