Mbunge wa Mbozi, Paschal Haonga amebainisha ukaribu wake na
Kasuku Bilago, aliyekuwa mbunge wa Buyungu aliyefariki dunia juzi katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
Aghalabu, wawili hao walikuwa wakiongozana, wakikaa jirani
bungeni huku Haonga akisema walifahamiana na kufanya kazi pamoja wilayani Mbozi
wote wakiwa walimu
“Urafiki wetu, uliongezeka baada ya mwaka 2015 wote kushinda
ubunge kwa kuwaangusha waziri na naibu waziri wa wizara moja ya kilimo, chakula
na ushirika,” alisema Haonga
Alisema walifahamiana wakati Bilago akiwa katibu wa Chama
cha Walimu Tanzania (CWT) Mbozi na yeye akiwa mwalimu wilayani hapo
“Tulifanya kazi pamoja na kufahamiana... mwaka 2015 tulikuwa
na malengo ya kugombea ubunge, yeye (Bilago) akasema atakwenda Buyungu na mimi
nitakwenda Mbozi,” alisema Haonga, “Ndoto zetu zilitimia, Bilago akashinda na
mimi nikashinda. Kitu pekee kilichoendelea kuweka historia ni kwamba Bilago
alimshinda (Christopher) Chiza aliyekuwa waziri wa kilimo na mimi nikamshinda
(Godfrey) Zambi aliyekuwa naibu waziri wa kilimo. Yaani tuliwashinda mawaziri
wa wizara moja.”
Alisema hata walipofika Dodoma, walipanga nyumba moja eneo
la Kisasa wakawa wanaishi pamoja hadi mwezi uliopita Haonga alipohama
“Baada ya kuapishwa mwaka 2015, Bunge lilipoahirishwa tu,
Bilago alinisindikiza jimboni Mbozi, ilikuwa Desemba na tulipokewa na umati wa
watu kuanzia Airport ya Songwe na nakumbuka siku ya mkutano wetu, mvua kubwa
ilinyesha lakini tulihutubia hivyohivyo na wananchi hawakutaka tamaa,” alisema
Haonga.
Alisema mwaka jana Bilago alikwenda pia jimboni Mbozi baada
ya kualikwa na Haonga kuangalia miradi aliyoitekeleza ikiwamo ya visima vya
maji na kumpa ushauri wa jinsi ya kuiboresha
“Bilago aliniambia, amekuja jimboni kwangu mara mbili kwa
hiyo imebaki zamu yangu na tulipanga baada ya mkutano wa Bunge hili la Bajeti
kumalizika, tutakwenda lakini ndiyo hivyo, ameondoka kabla sijatekeleza ahadi
ya kutembelea jimbo lake,” alisema
“Bilago hakuwa rafiki pekee, bali mshauri wangu wa masuala
mbalimbali, amenifundisha ujasiri, Bilago alikuwa mtu anayesimamia kile
anachoamini na kukisema bila woga. Kifo cha Bilago kimeniuma sana.”
Shughuli za Bunge kuahirishwa
Kutokana na kifo
hicho, shughuli za Bunge la Bajeti zinazoendelea jijini Dodoma zitaahirishwa
leo
Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai alisema jana kwamba
shughuli hizo zitaahirishwa ili kutoa fursa kwa wabunge kuomboleza msiba huo
Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano wa Bunge la Bajeti, leo
ilikuwa ni zamu ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwasilisha
makadirio yake ya mapato na matumizi
Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi ya mbunge huyo iliyotolewa
jana na Ofisi ya Bunge na Chadema, marehemu Bilago ataagwa leo katika Viwanja
vya Karimjee kabla ya kusafirishwa kwenda Dodoma ambako ataagwa kesho
Baada ya kuagwa na wabunge pamoja na wananchi wengine wa
Dodoma Jumanne, siku hiyohiyo mwili wake utasafirishwa kuelekea Kakonko ambako
utaagwa Jumatano kabla ya kuzikwa Alhamisi kijijini kwake Kasuga umbali wa
kilomita saba kutoka mjini Kakonko.
Jana, viongozi wa ngazi za juu wa Chadema wakiongozwa na
mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe walikutana nyumbani kwa marehemu Kawe,
jijini Dar es Salaam na baadaye mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema
(Bavicha), Patrick ole Sosopi aliwaambia waandishi wa habari kwamba mwili wa
marehemu Bilago utaagwa Karimjee leo kuanzia saa sita mchana akisema uamuzi huo
umefikiwa baada kikao kilichofanyika jana kati ya familia, Bunge na Chadema.
‘Mimi na Bilago tuliwaangusha waziri na naibu wake 2015’
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 27, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment