Mwenyekiti wa
CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Ngicho mwishoni mwa wiki iliyopita aliingia katika
mvutano na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alipogoma kuambatana naye kwenda
Kijiji cha Nyanundu kukanusha kauli aliyoitoa kwa wananchi kuhusu mipaka ya
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Ngicho
anadaiwa kuitisha mkutano na kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho akiwataka
wasitii agizo lililotolewa na Malima la kuwataka ndani ya siku 60 wawe wamehama
eneo la hifadhi ambalo liliwekwa alama ya mpaka (bikoni) Aprili 14
Video kuhusu
majibizano kati yao ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa wiki
iliyopita na kuzua mijadala kutoka kwa wananchi
Hali ya kuwapo
mvutano kati ya viongozi wa CCM na wa Serikali wanaotokana na chama hicho
inaonekana kuongezeka baada ya Jumamosi, gazeti hili kuripoti mgogoro
unaofukuta wilayani Mwanga ambako mkuu wa wilaya hiyo, Aaron Mbogho alidaiwa
kumuweka mahabusu mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Jaffary Kandege.
Taarifa
zinasema mwenyekiti huyo aliwekwa mahabusu Kituo cha Polisi Mwanga kabla ya
kudhaminiwa na diwani wa Shighatini (CCM), Enea Mrutu
Kandege
alisema kwa hali ya mgogoro ilipofikia hayupo tayari kufanya kazi na Mbogho
Lakini Mbogho
alisema mwenyekiti huyo hakufikishwa polisi na kuhojiwa kwa wadhifa wake
akitaka aulizwe aliandika maelezo kuhusu tuhuma gani
Kuhusu mvutano
kati ya Malima na Ngicho, mazungumzo kati yao kwenye video iliyosambaa ni kama
ifuatavyo:
Malima: Twende
sasa hiviNgicho: Aah! Nyanundu siendi.
Malima: Aah!
Huwezi kusema hivyo mimi ndiye ninayekwambia tutakwenda. Haki ya Mungu
nakwambia
Ngicho:
Samahani mkuu naumwa sana, naumwa sana, naumwa, naharisha, naharisha.
Malima:
Nakuhakikishia mwenyekiti. Potelea mbali mwenyekiti tunabeba na maji mtoni,
twende ukawaambie wale wananchi kuwa Serikali nchi hii ni moja basi
Ngicho:
Hapana, hapana, hapana. Naomba umchukue na Heche umwambie, hivyo maana mimi ni
kiongozi wa chama
Malima: Nasema
hivi, wewe uliitisha mkutanao kule kwa hiyo leo tutakwenda Nyanundu
Ngicho:
Sijaitisha mkutano mkuu, mimi nilikuta watu wamejaa pale wakanizuia
Malima: Basi
watakukuta leo, twende hata wakitukuta watu wawili
Ngicho: Hapana
kiongozi
Alipoulizwa
kuhusu video hiyo, Malima alisema alimtaka mwenyekiti huyo kuongozana naye
kwenda kijijini kutatua mgogoro uliopo baina ya Serikali na wananchi kuhusu
uwekaji wa mipaka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
“Kiongozi huyo
wa chama alifanya mkutano katika Kijiji cha Nyanundu ambacho kipo ndani ya
hifadhi na kuwataka wananchi wakaidi agizo nililotoa siku chache kabla ya
mkutano wake nikiwataka walio ndani ya bikoni waondoke ndani ya siku 60 naye
alikuwa akikataa,” alisema Malima
Alisema
alikuwa akitaka mwenyekiti huyo akakanushe kauli aliyoitoa kwa wananchi kuwa
wasiondoke eneo hilo
“Serikali ina
sheria na sheria hizo hazina kushoto wala kulia, ukiambiwa na Serikali usifanye
hiki acha.
Sasa unapokaidi agizo lazima uchukuliwe hatua. Yule mwenyekiti
alikwenda mwenyewe kwenye hicho kijiji na kuwataka wananchi wakiuke agizo la
Serikali,” alisema
Kwa upande
wake, Ngicho alisema Malima alimfuata nyumbani kwake Kijiji cha Kariyashanga na
kumlazimisha aende kuwaambia wananchi wa Nyanundu wahame naye alikataa
Ni kweli
nilikataa na hiyo kuharisha nilisema tu kama sehemu ya kujitetea lakini ukweli
ni kwamba, Serikali lazima isikilize chama kinasema nini isifanye tu hata kama
inawaumiza wananchi,” alisema Ngicho.
Alisema yeye ni kiongozi wa chama na ni
mwanasiasa. Ngicho alisema alikwenda katika kijiji hicho na kamati ya siasa
baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi ambao walikuwa wakilia na
kuimba, ‘CCM inatutesa inatunyang’anya ardhi’
“Tulipata
taarifa kwamba wananchi zaidi ya 42 wamekamatwa na wamepigwa. Nilipata taarifa
hizo nikiwa Dar es Salaam, nikampigia simu DC wa Tarime twende tukatembelee
hayo maeneo akaniambia yuko Simiyu ikabidi tuondoke na kamati ya siasa,”
alisema
Mwenyekiti
huyo alisema walipofika aliwakuta wananchi wenye hasira waliowazingira na
kuwataka wazungumze chochote hivyo iliwalazimu kuwatuliza kwa kuwaeleza kuwa
wakae watulie na wasubiri kauli ya naibu waziri mwenye dhamana ambaye atakwenda
kuwasikiliza
“Kwa kuwa ni
mwanasiasa niliwaambia wananchi wawe wavumilivu naibu waziri anakuja. Viongozi
wa Serikali waliposikia, kina Malima likawaudhi. DC akaja kwangu hakunikuta,
siku ya pili akanikuta ndipo Malima akaanza kunilazimisha niende nikawaeleze
wale wananchi kuwa ile mipaka ni halali na wananchi waiheshimu,” alisema.
Mwenyekiti
huyo alisema, “Niliona suala la kwenda kutamka hivyo litaniumiza kisiasa,
nikakataa. Alinilazimisha twende kule jambo ambalo haliwezekani kwangu kwa kuwa
kufanya hivyo ni kukidhalilisha chama changu.”
Ngicho alisema
hawezi kwenda katika kijiji hicho kuwaeleza wananchi wahame eneo hilo kwa kuwa
wamekaa hapo muda mrefu na uwekaji wa bikoni haujawashirikisha
“Mimi mwenyewe
nimejenga, nina hoteli iko ndani ya bikoni lakini kuwa ndani ya bikoni
hakunizuii kuwatetea wananchi,” alisema.
Mkuu wa mkoa, mwenyekiti wa CCM wilaya walivyochuana
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 27, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment