Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema
serikali ipo makini na ajira za wageni na itaendelea kuhakikisha kuwa
watanzania wanapewa fursa kwanza.
Waziri Majaliwa ametoa kauli hiyo
leo Mei 17, 2018 Bungeni Jijini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa
papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Leah
Komanya aliyetaka kupata kauli ya serikali juu ya wageni wanaoingia nchini na
kupata ajira kwenye maeneo nyeti kama vile bandarini au viwanja vya ndege.
"Ajira zote za wageni nchini
Tanzania ni kwa nafasi zile za kitaalam tu ambazo watanzania hawana uwezo nazo
na hatujaacha wazi, tumeweka ukomo kuwa ni wageni watano tu kwa kila taasisi
ndio wanapata fursa ya kuajiriwa ndani ya nchi, kuitumikia taasisi hiyo na ni
kwa nafasi ambazo watanzania hawana uwezo nazo," amesisitiza Majaliwa.
Akifafanua zaidi, Waziri Mkuu
amesema pale ambapo italazimu raia wa nje apate ajira, serikali itaendelea
kusimamia ili kuhakikisha kama kweli nafasi hiyo haina mtu na ni nafasi nyeti
yenye utaalam ambao hakuna mtanzania mwenye uwezo nayo.
Akijibu hoja kuhusu wageni kufanya
kazi kwenye maeneo nyeti, Waziri Mkuu amesema serikali imeendelea kuhakikisha
kwamba hakuna mgeni anayefanya kazi kwenye maeneo ya viwanja vya ndege, bandari
au yale ya mipakani.
"Hii ni kwa sababu ni lazima
tuweke watanzania ambao kweli wanakerwa na nchi yao na wanaweza kulinda nchi
yao kuanzia mipakani ili kuhakikisha kwamba hakuna jambo lolote linaloashiria
kuvunjika kwa amani.", amesisitiza
Majaliwa.
Kwa upande mwingine, Majaliwa
amesema endapo atakutwa mtu yeyote wa Taifa la nje anafanya kazi kwenye maeneo
hayo, basi atakuwa ameajiriwa na kampuni ambayo inafanya shughuli maalum kwenye
eneo hilo na kwa masharti yale yale kwamba watapata nafasi kufanya kazi kwenye
kampuni hiyo kama nafasi hiyo hakuna Mtanzania mwenye uwezo nayo.
Wageni watano tu wanaruhusiwa kuajiriwa - Majaliwa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 17, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment