Serikali Kagera imeanza kuwapima
watu wanaoingia kutoka nchi jirani kupitia mkoa huu, ili kubaini kama wana
maambukizi ya ugonjwa wa ebola.
Hatua hiyo inafuatia kutangzwa kwa
mlipuko wa ugonjwa huo kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika
Manispaa ya Bukoba jana, Kaimu Ofisa Afya Mkoa wa Kagera, Geraz Ishengoma
alisema kuwa kila mgeni anayeingia nchini anapimwa na anayeonekana ana dalili
zinazofanana na ugonjwa huo, hupelekwa kupimwa zaidi.
Ni mara ya pili katika mwaka mmoja
kwa serikali kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ebola. Mei 29, mwaka
jana Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu,
alisema wageni kutoka nchi hiyo wangesajiliwa na kufuatiliwa hadi wanakoishi
ili kujiridhisha kama hawana virusi vya ebola.
Kaimu Ofisa Afya Mkoa wa Kagera,
Ishengoma alisema jana: “Tumeweka kambi katika maeneo ya mpakani hasa Mutukula,
Murongo, Kabanga na Rusumo, (na) kila mtu anayeingia anapimwa ikiwamo joto la
mwili.
"Tunayekuwa na shaka naye,
tunamtenga na kumchunguza zaidi.”
Alisema kuwa kambi hizo za mpakani
ziliwekwa baada ya serikali kutangaza kuwapo kwa ugonjwa huo DRC Mei 8, mwaka
huu, na kuwa hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyebainika kuwa na maambukizi ya virusi
vya ugonjwa huo.
Alisema virusi vya ugonjwa huo
vinaambukizwa kwa kugusa damu au majimaji, kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa
ugonjwa huo na kugusa wanyama wenye maambukizi, na kuwa dalili zake huanza
kuonekana kuanzia siku mbili hadi 21 tangu mtu anapoambukizwa.
Ishengoma alitaja dalili za ugonjwa
huo kuwa ni homa kali, kulegea mwili, kichwa kuuma kunakoambatana na kutapika
na kutokwa na damu sehemu tofauti za mwili, ikiwamo puani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa
Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu, alisema serikali imechukua kila
tahadhari ili kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini kupitia mkoa wa Kagera.
“Kumbukeni Kagera ni mkoa ambao
unapakana na nchi nyingi, zikiwamo za Rwanda, Burundi na Uganda, lakini pia
unapakana na mkoa wa Kigoma ambao watu kutoka Congo hupitia katika mkoa huo na
kuingia Kagera hasa kupitia eneo la Murusagamba,” alisema.
Kijuu aliwataka wananchi kutoa
taarifa haraka endapo watabaini kuwapo kwa mtu mwenye dalili kama za ebola
katika maeneo yao, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
“Lakini pia wananchi hawapaswi
kugusana na mgonjwa mfano kugusa mate, majimaji na damu, kuepuka kugusa maiti,
kutochelewa kupata huduma na kuzingatia usafi wa mwili,” alisema.
Alisema kuwa serikali inaendelea
kushirikiana na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.
Wageni Wanaoingia Nchini Waanza Kupimwa Ebola
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 16, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment