Deni la Taifa laongezeka kwa Sh12 trilioni ndani ya miezi mitatu


Kwa miezi mitatu ya kwanza mwaka huu, deni la Taifa limeongezeka kwa zaidi ya Sh12 trilioni na jumla kuongezeka mpaka takriban Sh60 trilioni, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeonyesha

Ripoti ya tathmini ya kila mwezi ya BoT inaonyesha kwa mwaka ulioishia Machi, Serikali ilikopa zaidi ya Dola 2.489 bilioni za Marekani kutoka vyanzo vya nje huku iki-chukua zaidi ya Sh2.084 trilioni kutoka nda-ni. Kutokana na ongezeko hilo, deni la nje limefika zaidi ya Dola 20.156 bilioni (zaidi ya Sh45.35 trilioni) wakati la ndani likizidi Sh14.158 trilioni

Kwa miezi mitatu ya kwanza mwaka huu, deni hilo limeongezeka kwa zaidi ya Sh12 trilioni likilinganishwa na Sh47.756 trilioni lililokuwapo mwishoni mwa Desemba mwa-ka jana alilolibainisha waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alipokuwa akiwa-silisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ukomo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19

Wakati huo, Dk Mpango alisema deni la nje lilikuwa Sh34.148 trilioni (sawa na asil-imia 71.5) na la ndani lilikuwa Sh13.607 trilioni (sawa na asilimia 28.5

Hata hivyo, alisema uwiano wa deni hilo na Pato la Taifa kwa mwaka wa fedha 2017/18 ni asilimia 34.4 ikilinganishwa na ukomo ambao ni asilimia 56.“Uwiano wa deni la nje na mauzo ya nje ni asilimia 81.1 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150. Hii inamaanisha kuwa uwezo wetu wa kulipa deni bado ni imara,” alisema Dk Mpango.

Katika kuonyesha umakini uliopo, waziri huyo alisema Serikali inaendelea kuchukua tahadhari kwa kukopa kwenye vyanzo vyenye masharti nafuu ili kuhakikisha kuwa mikopo hiyo inaelekezwa kwenye miradi ya maen-deleo.
Deni la nje

Katika deni lote la nje, ripoti ya Machi ya BoT inaonyesha Serikali ilikopa zaidi kutoka taasisi za kimataifa kama vile Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF). Chanzo hicho kinachangia zaidi ya asilimia 47 ya deni lote la nje

Theluthi moja ya deni hilo (asilimia 31.5) ilitoka benki za biashara za nje, makubaliano na nchi zingine (bilateral agreements) zikiikopesha asilimia 9.3.

Vyanzo hivyo vimechangia asilimia 87.8 ya deni lote na kiasi kilichobaki kikitokana na mikopo ya usafirishaji wa huduma na bidhaa nje ya nchi

Katika deni hilo, Serikali kuu ilikopa zaidi ikiwa na asilimia 77.3 ambalo ni ongezeko la Dola 7.2 milioni kutoka lililokuwapo mwishoni mwa Februari, na Dola 1.81 bilioni la Machi mwaka jana.

Machi pekee, Tanzania ilikopa Dola 132.9 milioni, asilimia 69.1 zikiwa ni za Serikali kuu na kwa mwaka ulioishia mwezi huo ilikopa Dola 1.672 bilioni zikiwamo Dola 1.331 bilioni za Serikali na kiasi kinachobaki kikiwa cha sekta binafsi

Wakati ikikopa kiasi hicho, taarifa zinaonyesha ni Dola 184.6 milioni pekee zililipwa Machi 2018 zinazojumuisha Dola 143.1 milioni ambalo ni deni la msingi na riba yake

Kwa mwaka ulioishia Machi, Serikali ilitoa Dola 1.053 bilioni zilizojumuisha Dola 705.8 milioni za deni la msingi na riba yake.
Kuhusu kuongezeka kwa deni hilo, BoT inasema limechangiwa na mikopo mipya, kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani na malimbikizo ya riba

Hata hivyo, kwenye hotuba yake, Dk Mpango alisema miradi mitano ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa imechangia ongezeko la zaidi ya Dola 26.115 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh57.453 trilioni) kwenye deni la Taifa

“Ongezeko hilo linachangiwa na mikopo mipya iliyochukuliwa ili kugharimia ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), strategic cities, Mradi wa Usafirishaji Dar es Salaam (Dart) na kupanua upatikanaji wa maji safi Dar es Salaam,” alisema

Mikopo ya ndani

 Kwa upande wa deni la ndani, benki za biashara na mifuko ya hifadhi ya jamii imekuwa ndio tegemeo. Benki zimetoa asilimia 39.2 likiongezeka kutoka asilimia 37.9 za mwaka jana.

 Mifuko ya hifadhi ya jamii ilitoa zaidi ya robo ya deni hilo (asilimia 26.9) na BoT ikitoa asilimia 19.9. Kutoka vyanzo hivi vitatu, Serikali imekopa asilimia 86 ya deni lote

Kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2016/17, inaelezwa kuwa mpaka Juni 2017, deni la Taifa lilikuwa zaidi ya Sh46.081 trilioni ambalo halijumuishi Sh4.588 trilioni ambazo ni deni la mifuko ya pensheni

Kwa kutumia hatifungani na amana zake, Serikali ilikopa Sh815.9 bilioni mwezi Machi ili kufanikisha utekelezaji wa bajeti yake huku ikikopa zaidi ya Sh7.536 trilioni ndani ya mwaka huo
Katika mwezi huo, deni lililokuwa tayari kulipwa (lililoiva) lilikuwa Sh692.5 bilioni likilinganishwa na Sh579.4 bilioni la Februari

Kati ya Sh692.5 bilioni zilizopashwa kulipwa Machi, deni la msingi ni Sh560 bilioni ambalo hata hivyo, taarifa inasema halikulipwa kwani Serikali ilikuwa na uwezo wa kulipa riba pekee, Sh132.5 bilioni. Kwa mwaka mzima, deni la Sh5.985 trilioni lilipaswa kulipwa lakini ni Sh1.218 trilioni zilitolewa huku kiasi kilichobaki, Sh4.765 trilioni kikiongezewa muda wa kulipwa (rollover

Taarifa ya CAG

Alipowasilisha ripoti ya mwaka 2016/17, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad alisema mpaka Juni 30 mwaka jana, deni la Taifa lilikuwa Sh46 trilioni

Katika deni hilo, alisema Sh13.3 trilioni ni la ndani na Sh32.7 trilioni la nje. Kwa mwaka mmoja deni lilikuwa limeongezeka kwa Sh5 trilioni kutoka Sh41 trilioni lililokuwapo Juni 2016

Kwenye ripoti yake, Profesa Assad alisema deni la Taifa limeendelea kukua kila mwaka. Ingawa ukopaji wa kibiashara ni muhimu kiuchumi, ukuaji mkubwa wa deni hilo hasa kutoka nje unapaswa kutazamwa kwa umakini na tahadhari ili kupunguza ukuaji na madhara yake

Alisema mapitio ya mpango wa ukopaji wa ndani kwa mwaka husika ilikuwa kukopa Sh6.48 trilioni kwa kuuza hati fungani lakini Serikali ilikopa Sh6.94 kinyume na mpango huo

“Nashauri Serikali ifuate mpango wa ukopaji wa ndani inapokopa ndani ya nchi,” alishauri CAG
Mtafiti mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Repoa, Dk Blandina Kilama alisema suala la msingi kwenye Deni la Taifa ni uhimilivu wake

“Mikopo ya muda mrefu ikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo si vibaya kwa kuwa Serikali inakuwa na nafasi ya kuilipa huku ikiendelea kutoa huduma za jamii kama kawaida. Mikopo ya muda mfupi ndio mibaya kwa kuwa huhitaji fedha nyingi zinazoweza kuathiri uwezo wa Serikali,” alisema mtafiti huyo

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema takwimu zinaonyesha, uwiano wa deni hilo na Pato la Taifa ni asilimia 36 wakati ukomo wake ni asilimia 56, jambo linalomaanisha kuwa bado ni himilivu

Lakini akatoa ushauri. “Uwepo utaratibu mzuri wa kukopa. Wananchi wajue tunakopa ili kufanya nini. Tuendelee kukopa na kuimarisha uchumi wetu,” alisema msomi huyo aliyebobea katika masuala ya sayansi ya siasa

Kwa mtazamo wake, alisema kukopa na kuwekeza kwenye miradi mkubwa kama wa kufua umeme wa Stiegler’s Gorge) na reli ya kisasa (SGR) ni jambo jema kwani itakapokamilika itaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, tofauti na kukopa kwa ajili ya kulipa mishahara ya watumishi.

 Naye mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe alisema mwenendo wa Deni la Taifa si mzuri kwa uchumi.

 “Siku za usoni uwezo wetu wa kugharimia deni utaathiri utoaji wa huduma kwa wananchi. Ni vema sasa Bunge liwe na wajibu wa kuidhinisha madeni,” alisema Zitto, ambaye amekuwa akizungumzia kila mara kuhusu mwenendo wa ukopaji wa Serikali

Deni la Taifa laongezeka kwa Sh12 trilioni ndani ya miezi mitatu Deni la Taifa laongezeka kwa Sh12 trilioni ndani ya miezi mitatu Reviewed by KUSAGANEWS on May 17, 2018 Rating: 5

No comments: