Mshtakiwa wa tano, Karim Kihundwa jana alijitetea kwa
kuyakana vikali maelezo yake ya ungamo kwa mlinzi wa amani, ambayo yanadaiwa
alikiri ndiye aliyemfyatulia risasi, Erasto Msuya
Mshtakiwa huyo alienda mbali na kudai kuwa alisaini maelezo
hayo baada ya kuteswa na hajui kilichoandikwa na kwamba, hajui kutumia SMG
zaidi ya kujua kutumia panga na shoka
Msuya aliuawa Agosti 7, 2013 saa 6:30 mchana katika eneo
Mijohoroni wilayani Hai, baada ya kushambuliwa kwa risasi 22 za bunduki ya
kivita aina ya SMG na wanaoshukiwa ni washtakiwa
Maelezo hayo ya ungamo (extra judicial statement) ya
mshtakiwa huyo yaliandikwa Septemba 16, 2013 na hakimu mkazi wa Mahakama ya
Mwanzo Moshi, Ponsian Claud aliyekuwa shahidi wa 12
Katika maelezo hayo yaliyosomwa mahakamani, shahidi huyo
alidai mshtakiwa aliyatoa kwa hiari na kwa ridhaa yake, akieleza alifika eneo
la tukio na mshtakiwa wa sita, Sadick Jabir wakiwa na pikipiki
Mshtakiwa anadaiwa kumweleza mlinzi huyo wa amani kuwa,
ndiye aliyefyatua risasi kwa kutumia bunduki aina ya SMG akishirikiana na mtu
aliyemtaja kwa jina moja la Sharifu na kumuua Erasto.
Katika maelezo hayo
ya ungamo, mshtakiwa anadaiwa kueleza kwa hiari yake kuwa kwenye utekelezaji
mauaji hayo, alishirikiana na watu wengine watatu ambao ni Sharifu, Mredii na
Sadik
Ushahidi mahakamani
Hata hivyo, jana akitoa ushahidi wake wa kujitetea,
mshtakiwa alidai alilazimika kutia saini maelezo hayo baada ya kuteswa ikiwamo
kunyimwa chakula na kuunguzwa miguu kwa pasi ya umeme
Akiongozwa na wakili wake, Majura Magafu kutoa utetezi wake,
mshtakiwa huyo alidai kukamatwa wilayani Kaliua mkoani Tabora Septemba 13, 2013
akiwa na mshtakiwa wa sita, Sadick Jabir
Alidai kuwa walikwenda huko kwa ajili ya shughuli za
uchimbaji dhahabu na kwamba, walikamatwa wakiwa kwa mganga aitwaye Sheikh
Khalid Samkamula ambaye ni shahidi wa tano.
Mshtakiwa huyo alidai
kuwa alikwenda kwa mganga huyo kupata baraka na mafanikio ya kimaisha na kukana
kuwa, hawakwenda kutafuta dawa ili wasikamatwe na polisi.</p></div><div><p>
Alieleza kuwa baada ya kukamatwa na shahidi wa tisa,
Inspekta Samwel Maimu akiwa na shahidi wa 10, Seleman Mwaipopo na shahidi wa
11, Sajini Atway Omary, waliwekwa mahabusu kituo cha Kaliua
Ilipofika saa 4:00 usiku, mshtakiwa anadai alitolewa
mahabusu na Inspekta Samwel na kuingizwa katika chumba kimojawapo na kumtaka
amweleze kuhusu tukio la mauaji ya Erasto Msuya
“Nilimwambia hakuna ninachojua na baada ya kumjibu hivyo,
alibadilika na kuniambia nampotezea muda kwani kila kitu anakijua. Alimuagiza
Atway aende kwenye gari na kurudi na pasi ya umeme,” aliiambia Mahakama hiyo
mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo
Alidai kuwa pasi hiyo iliwekwa kwenye umeme na kuwashwa,
Sajin Atway na Koplo Seleman walimshika miguu huku Inspekta Samwel akianza
kumchoma kwenye miguu
Mshtakiwa huyo alidai siku iliyofuata kati ya saa nne na saa
tano asubuhi, waliondoka kurejea Moshi na walifika siku inayofuata, hapo
aliwekwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Moshi
“Ilipofika mchana Samwel alikuja kunitoa lock up (mahabusu)
na kunipeleka kwenye chumba kimojawapo wakati huo akiwa na karatasi akiniambia
hataki utani anataka nizisaini,” alidai mshtakiwa huyo na kuongeza
“Sikuweza kuzisaini. Samwel alitoka nje akaja na kifaa aina
ya “plaizi” alianza kunimega maganda kwenye vile vidonda alivyonichoma wakati
huo vikiwa vimejaa maji na usaha.”
Alidai kuwa Septemba
17, 2013, Inspekta Samwel alimtoa mahabusu na kumweleza kuwa anampeleka kwa
mkuu wake wa kazi na lazima akubaliane na bosi wake, vinginevyo kipigo
kingeanza tena
“Tulifika katika jengo moja hapa Moshi mjini, Samwel aliingia
katika hilo jengo akiwa na bahasha. Baada ya muda alitoka na kuwaamuru polisi
aliokuwa nao waniingize ndani
“Huyo mkuu wake (Hakimu Claud) aliniuliza swali moja tu,
kwamba wewe ni Karim Kihundwa? Nikamwambia ndiyo, akaniambia nataka unisainie
hapa. Sikusomewa hizo karatasi,” alidai shahidi huyo na kuongeza
“Kutokana na hali yangu ya afya nilikuwa nimedhoofu sana kwa
njaa na maumivu ya vidonda, nilisaini hizo karatasi. Huyo mkuu wake ndiyo
ushahidi hapa akisema nilitoa maelezo ya ungamo.”
Akiongozwa na Magafu, mshtakiwa huyo alidai maelezo hayo
hajawahi kuyatoa na siku ya mauaji ya Erasto Msuya Agosti 7, 2013 alikuwa
shambani kwake West Kilimanjaro akivuna karoti
“Siyo kweli kwamba nilimweleza kuwa mimi ndiye
niliyemfyatulia risasi na kumuua Erasto Msuya. Sijawahi kufanya hivyo wala hiyo
tarehe sikuwapo na wala sijawahi kupitia mafunzo ya kijeshi,” alidai
Pia, alikanusha maelezo yaliyomo katika maelezo ya onyo ya
kukiri kosa ya mshtakiwa wa kwanza, Sharifu; wa tatu, Mussa Mangu; na wa saba,
Ally Majeshi kwamba walishiriki kumuua Msuya
“Niliiona hii bunduki ya SMG (kielelezo namba 13) kwa mara
ya kwanza ilipotolewa hapa mahakamani. Sijawahi kumiliki bunduki wala sijawahi
kutumia bunduki,” alidai mshtakiwa
Awali, katika ushahidi wake huo, alidai kuanzia Agosti 7,
2013 alikuwa shambani kwake West Kilimanjaro wilayani Siha na alirejea nyumbani
kwake Bomang’ombe Agosti 10, 2013
Pia, alikanusha ushahidi wa shahidi wa 27 wa mashtaka,
Inspekta Damian Chilumba aliyedai kwamba aliwapeleka yeye na Sadick kwa mkemia
wa Serikali na kuwachukua sampuli za vinasaba (DNA
Akihojiwa na wakili Hudson Ndusyepo anayemtetea mshtakiwa wa
kwanza, Sharifu, mshtakiwa huyo alikana kumfahamu mshtakiwa huyo na wengine
akieleza kuwa amekutana nao katika kesi hiyo
Akihojiwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah
Chavulla alimuuliza mshtakiwa huyo kama alikuwa anafahamu jengo lililopo upande
wa pili wa barabara ni la Mahakama
Mshtakiwa huyo alijibu kuwa kabla ya kupatwa na misukosuko
ya kesi hiyo alifahamu kuwa jengo hilo ni la Mahakama kwa vile wakati akipita
na basi kwenda Moshi, alikuwa akikuta polisi wengi.
Alipoulizwa na wakili Chavulla kama ndilo jengo alilopelekwa
na Inspekta Samwel kwa mtu aliyedai ni mkuu wake wa kazi, mshtakiwa huyo alidai
si kweli kwamba aliwahi kupelekwa katika majengo hayo
Wakili huyo alimuuliza kama alisikia ushahidi wa shahidi wa
12 (mlinzi wa amani), akijitambulisha kuwa ni hakimu mkazi anayefanya kazi
katika Mahakama ya Mwanzo Moshi, alikubali kusikia
Pia, alipotakiwa akubali kwamba alipelekwa katika majengo ya
hakimu huyo na kuandika maelezo ya ungamo, mshtakiwa huyo alidai kama
alipelekwa katika jengo hilo basi alipitishwa njia nyingine
Kuhusu kama alikuwa anafahamiana na hakimu aliyeandika
maelezo yake ya ungamo au kuwa na ugomvi naye, mshtakiwa huyo alidai alikuwa
hamfahamu na wala hakuwa na ugomvi naye
Aliulizwa kama polisi wanaweza kumuonea mtu, mshtakiwa huyo
alidai inawezekana na kutolea mfano kuwa kuna askari Kituo cha Polisi
Bomang’ombe aliwahi kumpeleka bila kuwa na kosa
Chavulla alimtaka aiambie Mahakama kabla ya kukamatwa
alikuwa akifanya shughuli gani, mshtakiwa alidai kwamba alikuwa akimiliki salon
tatu kwa jina la Gorilla zilizokuwa zikimuingizia Sh500,000 kwa mwezi
Kesi hiyo itaendelea leo kwa mshtakiwa wa sita, Sadick Jabir
kuanza kujitetea
KESI MAUAJI YA BILIONEA ERASTO MSUYA: Mshtakiwa akana kukiri kumfyatulia risasi Msuya
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 17, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment