Kampuni
ya uchimbaji madini ya Tanzanite One imekubali kuilipa Serikali fidia pamoja na
kodi watakayokubaliana kutokana na dosari zilizokuwepo hapo awali.
Makubaliano hayo
yametiwa saini Jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Rais
Dkt. John Pombe Magufuli Profesa Palamagamba Kabudi na Mkurugenzi wa
Tanzanite One Bw.Faisal Juma.
Akizungumza mara
baada ya kutia saini makubaliano hayo, Mwenyekiti wa kamati ya majadiliano kwa
upande wa serikali, Prof. Palamagamba Kabudi amesema Tanzanite One imekubali
kulipa fidia serikali kutokana na mambo iliyofanya ambayo yalikuwa kinyume na
utaratibu ulioleta hasara kwa serikali.
"Fidia hiyo
inatakiwa kulipwa kwa awamu ambapo awamu ya kwanza italipwa ndani ya wiki mbili
kuanzia leo na haitahusisha kodi. Pia Kampuni hiyo Tanzanite One italazimika
kulipa kodi kama kawaida inazodaiwa na serikali na tozo nyingine zote
zinazodaiwa na serikali", amesema Kabudi.
Pia serikali
imekubaliana na Kampuni ya Tanzanite One kuwa itafuata masharti yote ya sheria
ya madini ya mwaka 2010 ambayo inaeleza kuwa ni watanzania tu ndio
wanaoruhusiwa kuchimba madini ya vito na pale ambapo watanzania hawana uwezo
huo ndipo wanapoweza kuingia ubia na wageni.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Kampuni ya Tanzanite One Faisal Juma amemshukuru Mhe. Rais
Magufuli kwa kuunda kamati hiyo ya kizalendo katika kufuatilia rasilimali za
madini nchini ambapo wameweza kujadiliana na kufikia muafaka wa kulipa fidia
ikiwa ni mbali na malipo yote yaliyotakiwa kulipwa serikali ikiwemo kodi.
No comments:
Post a Comment