Msako wabaini Arusha kuna sukari na mafuta ya kula ya kutosha


Msako wa kamati ya ulinzi na usalama katika maghala ya wafanyabiashara wakubwa umebaini kuwa jijini Arusha kuna mafuta na sukari ya kutosha hivyo ni marufuku kupandisha bei

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 15, 2018 baada ya msako huo jana, Mkuu wa wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro amesema maghala yote ambayo wametembelea licha ya kuwapo uzalishaji mdogo wamebaini bado kuna mafuta na sukari

"Kamati ya ulinzi na usalama wilaya imetembelea maghala na kuona bado kuna bidhaa na kwa sukari bado bei ya jumla mfuko wa kilo 50 ni kati ya Sh102,000 na Sh110,000,” amesema

Amesema kutokana  na bei hizo bei ya kilo moja haipaswi kuuzwa zaidi ya Sh2,600 hivyo ambao watauza zaidi watachukuliwa hatua

Daqarro amesema kuhusiana na sukari iliyofungwa bei pia haipaswi kuzidi Sh2,800 na taratibu zinafanywa kuhakikisha bei haiongezeki

Kuhusiana na mafuta pia amesema yapo ya kutosha ikiwapo ya alizeti licha ya uzalishaji kupungua

Wakizungumza baadhi ya wakazi  wa Arusha waliomba Serikali kuendelea kudhibiti kupanda bei ya mafuta na sukari hasa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan

Jasmin Ally mkazi wa makao mapya amesema katika maduka mengi kati kati ya jiji sukari inauzwa kilo kati ya Sh2,700 na Sh2,800

Hillal Kusena amesema bei ya mafuta na sukari inaendelea kupanda licha ya matamko ya Serikali

"Serikali ingefatilia kujua tatizo ni nini kama ni kodi kubwa basi wapunguze lakini kutoa matamko tu hakutoshi," amesema Kusena

Amesema bei ya mafuta ya kupikia bei ya jumla imepanda kutoka Sh 61,000 hadi Sh 70,000 kwa lita 20 huku lita 10 imepanda kutoka Sh 30,000 hadi Sh35,000

Msako wabaini Arusha kuna sukari na mafuta ya kula ya kutosha Msako wabaini Arusha kuna sukari na mafuta ya kula ya kutosha Reviewed by KUSAGANEWS on May 15, 2018 Rating: 5

No comments: