Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanznia Dkt. John Pombe Magufuli, leo amefanya ziara ya kushtukiza bandarini
jijini Dar es salaam kukagua matanki ya mafuta ya kula, ambayo yameadimika hapa
nchini.
Baada ya ziara hiyo na kufanya
ukaguzi, Rais Magufuli amebaini kuwa kuna mafuta ambayo yameingizwa nchini huku
kukiwa na taarifa za udanganyifu ili kukwepa kodi, yakiwemo mafuta ambayo
yameshakamilika (refined oil) na kusema kuwa ni mafuta gahfi (crude oil).
Baada ya kugundua hilo Rais Magufuli
amewataka wamiliki wa mafuta hayo kulipa ushuru wake unaostahili, pamoja na
fine kutokana na udanganyifu walioufanya.
"Kwenye bidhaa walizosema ni
crude kumbe ni refined oil walipe 25% pamoja na fine, hatuwezi tukawa tunaibiwa
kila siku tunahitaji kujenga viwanda vetu, haiwezekani crude oil ukachaji sawa
na semi refined, na hii sheria yetu inawezekana kulifanyika mchezo, wabunge
walipitisha kitu kingine, kinachojadiliwa kingine, kilicholetwa huku ni
kingine, kinachokuja kupitishwa kuwa sheria kimebadilishwa kuwa kingine,
"Hii crude oil ichajiwe bei ya juu ili watu wengi wajenge viwanda hapa ili
tujenge nchi yetu ”, amesema Rais Magufuli.
Sambamba na hilo Rais Magufuli
amemtaka mkemia Mkuu wa Serikali kufuata maadili ya kazi, ili kuleta weledi na
kujenga nchi.
"Mkemia Mkuu nataka sampo
zozote mtakazokuwa mnapewa fanyeni kwa utaratibu kwa kuzingatia maadili,
mkiletewa mkono wa albino semeni mkono wa albino msije mkasema mkono wa mbwa.
Mkiletewa madawa ya kulevya semeni haya ni madawa ya kulevya sio unga wa
muhogo, amesema Rais Magufuli.
Magufuli ashtukiza bandarini na kuibua mapya
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 15, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment