Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekemea
uharibifu wa makusudi wa miundombinu ya barabara na majengo unaofanywa na
baadhi ya wananchi na kuwataka waache tabia hiyo mara moja.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
asubuhi (Alhamisi, Mei 17, 2018) Bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha
maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa
Magu, Bw. Kiswaga Destery aliyetaka kujua Serikali inachukua hatua gani dhidi
ya wananchi wanaoharibu miundombinu ili wakauze kama vyuma chakavu kwa vile
Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu hiyo.
Waziri Mkuu amesema serikali
inatumia fedha nyingi sana kuboresha miundombinu mbalimbali nchini na kwamba
kila Mtanzania anao wajibu wa kulinda miundombinu hiyo.
"Serikali inatumia fedha nyingi
kujenga miundombinu ya barabara na majengo ili kutolea huduma, watanzania wote
tunao wajibu wa kuilinda na endapo itatokea mtu anaihujumu miundombinu hii,
serikali hatuwezi kukaa kimya, lazima
tutachukua hatua," ameonya
Waziri Mkuu.
Aidha, Waziri Mkuu amesema jukumu la
ulinzi ni la watanzania wote, na kila mtanzania anayo dhamana ya ulinzi na
usalama wa ndani ya nchi ikiwemo kuilinda miundombinu.
"Juzi niliona kwenye
televisheni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mheshimiwa Jaffo akishirikiana
na Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani Shinyanga, wamekamata Fuso lililojazwa
vyuma vilivyong'olewa kwenye barabara, ni vile ambavyo vinawekwa kwenye daraja
na kingo za barabara," amesema.
Pamoja na hayo Waziri Mkuu
ameendelea kwa kusema
"Huu ni uharibifu ambao
hatuwezi kuvumilia, na katika hili Watanzania lazima tuungane pamoja tukemee
tabia hii. Tunatumia fedha nyingi kujenga kingo za barabara, kuashiria maeneo
yenye hatari lakini Watanzania wengine wanakuja kung'oa kwa matumizi yao. Mimi
naamini Mkoa wa Shinyanga utakuwa umechukua hatua kali dhidi yao".
Lazima tutachukua hatua- Majaliwa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 17, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment