Baadhi ya Wakaguzi na Askari
wa vyeo mbalimbali wakimsikiliza Kamanda mpya wa mkoa wa Arusha Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Nga'anzi mara baada ya
kukaribishwa kuongea machache
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP)
Charles Mkumbo leo hii mchana amewaaga Maofisa, Wakaguzi na askari wa vyeo
mbalimbali katika kikao kilichofanyika Bwalo la Maafisa wa Polisi lililopo
jijini hapa.
Akizungumza na askari hao Naibu Kamishna Mkumbo ambaye
amehamishiwa Makao Makuu ya Jeshi hilo, aliwashukuru askari wote wa mkoa huu
kwa kushirikiana naye vizuri katika utendaji wa kazi hali ambayo ilisaidia kwa
kiasi kikubwa kudumisha usalama kwa kipindi chote alichokaa hapa.
Naibu Kamishna Mkumbo ambaye amefanya kazi mkoani hapa kwa
takriba miaka miwili na miezi miwili alisema kwamba mafanikio ya kazi za
kijeshi msingi wake mkubwa ni nidhamu na kufanya kazi kwa weledi.
Aliongeza kwa kusema kwamba, endapo askari wa mkoa wa Arusha
wataendelea kudumisha nidhamu na kutoa huduma iliyo bora kwa wananchi basi ni
wazi wananchi hao wataendelea kuliunga mkono Jeshi hilo kwa hali na mali.
Aliwataka askari hao kuendelea kutoa ushirikiano wa hali ya juu
kwa Kamanda mpya hali ambayo itasaidia kuzidi kuimarisha usalama wa mkoa na
kuendelea kuwa kivutio kwa watalii na wawekezaji wa sekta nyingine.
Kwa upande wake Kamanda mpya wa mkoa huu Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi alisema kwamba, ataendeleza yale
mema yaliyofanywa na mtangulizi wake na kuboresha zaidi pale ambapo panahitajika
kufanya hivyo ili kuweza kuzidi kuimarisha usalama wa mkoa huu.
Alisema ili kufanikisha utendaji bora, askari anatakiwa afanye
kazi kwa weledi, uaminifu na uadilifu, atoe huduma bora kwa mwananchi lakini
pia alilisitiza nidhamu.
“Kama hakuna nidhamu basi hakuna Jeshi na ningependa tuishi kama
familia moja hali ambayo itasaidia kumshinda adui”. Alisisitiza Kamanda
Ng’anzi.
Katika kipindi chake cha uongozi mkoani hapa Naibu Kamishna
Mkumbo kwa kushirikiana na askari aliweza kupunguza matukio ya uhalifu; ambapo
matukio ya uhalifu yaliyoripotiwa kwa mwaka 2016 yalipungua kwa 6.8%
ikilinganishwa na mwaka 2015 na takwimu za matukio ya uhalifu kwa mwaka 2017
yalipungua zaidi kwa 17.9% ambapo kati ya hayo matukio ya uvunjaji yalishuka
toka 604 mwaka 2016 hadi kufikia 294.
Mbali na hayo Naibu Kamishna Mkumbo alikuwa anawaongoza askari
katika mazoezi ya riadha ambapo kila Jumamosi alikuwa akikimbia kilomita 10
hadi 15 hali ambayo ilizidi kuwatia moyo wa kufanya mazoezi binafsi askari wa
mkoa wa Arusha lakini pia aliweza kuwahamasisha askari kushirikia hatua nusu marathoni
mashindano mbalimbali ya riadha kama vile Kili Marathon na kadhalika.
DCP MKUMBO AWAAGA ASKARI, AMKARIBISHA RPC RAMADHANI NG’ANZI KUANZA KAZI RASMI
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 26, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment