Wakati wananchi na viongozi
wakiomboleza kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago kumekuwepo na
mkanganyiko wa taarifa kutoka Ofisi ya Bunge na viongozi wa CHADEMA kuhusu siku
rasmi ya mazishi ya Mbunge huyo.
Katika ibada maalumu ya kuaga mwili
wa Mbunge huyo iliyofanyika leo Mei 28, 2018 katika viwanja vya Karimjee Jijini
Dar es salaam, Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe amesisitiza kuwa siku ya
mazishi ya mbunge ni Alhamisi Mei 31, 2018.
“Siku ya Alhamisi tutampeleka
kanisani kwa ibada maalumu kwajili ya maziko yake, kisha tutakwenda kwenye
shamba la familia kwaajili ya kumlaza, lakini Bunge bado linasisitiza tutamzika
Jumatano, mimi namwambia Spika (Job Ndugai) na timu yake watazika mtu wao
wanayemtaka, Mbunge wetu tutamlaza siku ya Alhamisi” amesema Mbowe.
Mwenekiti huyo ameongeza kuwa
kama Bunge halitaonesha ushirikiano na viongozi wa chama hicho pamoja na
familia basi kama viongozi wa chama watakuwa tayari kugharamia kila kitu pasipo
msaada wa Ofisi ya Bunge.
Mapema leo Mei 28, 2018 Naibu Spika
Dkt. Tulia Ackson akitangaza kuaihirisha kikao cha Bunge Jijini Dodoma ili
kuomboleza kifo cha mbunge huyo, Naibu spika aliweka wazi ratiba ya mazishi
itakua ni Jumatano Mei 30, 2018 katika Kijiji cha kasuga wilaya Kakonko mkoani
Kigoma.
Marehemu Kasuku Bilago alikuwa
Mbunge wa jimbo la Buyungu kupitia CHADEMA alifariki Dunia Mei 26, 2018 katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Bunge, CHADEMA wavutana mazishi ya Bilago
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 28, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment