Singida United yazichimba mkwara vilabu vya Ligi

Uongozi wa Klabu ya Singida United umefunguka na kuanza kujigamba kuwa utapambana kadri ya uwezo wao katika michuano ya ligi kuu ili historia yao iweze kubaki salama huku wakiwatitishia wapinzani wao Mbeya City kwamba wao sio ngazi ya kuwapandisha wengine daraja
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Singida United Festo Sanga ikiwa yamebakia masaa machache kuelekea mtanange wao dhidi ya Mbeya City leo Aprili 27, 2018 katika dimba la Sokoine mjini Mbeya katika muendelezo wa michezo ya ligi kuu Tanzania Bara.

"Tunaenda kucheza na Mbeya City tukiwa tunawaheshimu kwani wametoka sare na timu kubwa kama Yanga hivyo naamini hata sisi wametupania na pia wanahitaji kujiondoa katika nafasi waliyopo, lakini sisi sio ngazi ya wengine kung'ang'ania kutokushuka daraja. Sisi tunacheza mpira na hatuingii uwanjani kumpa mpinzani wetu pointi tatu bali tunapambana", amesema Sanga.

Pamoja na hayo, Sanga ameendelea kwa kusema "tunapambana kadri ya uwezo wetu ili kwenye Ligi kuu historia yetu iweze kubaki kuwa salama kwa maana tunahitaji kuwa kwenye nafasi ya nne, tatu au mbili na hilo linawezekana kwa sababu mpira unadunda na bado tuna mechi tano kabla ya kumaliza Ligi kwa hiyo hauwezi jua kitakachotokea".

Singida United inashuka dimbani ikiwa nafasi ya tano kwa alama 37 kwa michezo 25 kibindoni katika msimamo wa ligi kuu, Mbeya City akishika nafasi ya 10 kwa alama 26 yenyewe ikiwa na michezo 24 mpaka sasa waliyofanikiwa kuicheza.


Singida United yazichimba mkwara vilabu vya Ligi Singida United yazichimba mkwara vilabu vya Ligi Reviewed by KUSAGANEWS on April 27, 2018 Rating: 5

No comments: