|
|||
Mamlaka ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA),
imeteketeza kilo 48 za nyama kutoka Afrika Kusini baada ya Serikali
kusitisha uingizaji nyama kutoka nchini humo kutokana na mlipuko wa bakteria
wa listeria.
Ilibainika kuwa nyama hizo ziliingizwa nchini kinyume
cha sheria.
Nyama hizo ni mali ya kampuni ya Qamar ya Vingunguti
jijini Dar es Salaam, ilikamatwa Uwanja wa wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid
Karume mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza leo Machi 14 wakati wa zoezi hilo, mkuu wa
kitengo cha uchambuzi wa hatari zinazotokana na chakula wa ZFDA, Aisha
Suleiman amesema kilichosababisha kuteketezwa kwa nyama hiyo ni katazo
lililotolewa na ZFDA baada ya kutokea mlipuko wa ugonjwa wa listeriosis.
Amesema ZFDA ndiyo yenye majukumu ya kuhakikisha
wananchi wanapata chakula salama.
Aisha amesema uamuzi ya katazo hilo umetokana na uwapo
wa maradhi ya Listeriosis nchini Afrika Kusini, hivyo ofisi yao imepiga
marufuku uingizwaji nyama, maziwa na samaki kutoka nchi hiyo.
Bakteria wa listeria, wanaosababisha maradhi ya
listeriosis, wamesababisha vifo vya watu zaidi ya 180 Afrika Kusini.
Amesema katazo hilo si kwa Zanzibar pekee bali na
Tanzania bara na nchi nyingine kutokana na utaratibu wa biashara kimataifa
“Hili katazo siyo sisi tu, ni utaratibu wa kimataifa
kwamba kutokana na maradhi ya listeriosis bidhaa za nyama, samaki, maziwa ni
marufuku kuingizwa nchini sasa hii kampuni ya Qamar LTD ya Dar es Salaam wao
waliamua kuingiza nyama hiyo, tumeikamata na kuiangamiza.” amesema Aisha.
|
ZFDA yateketeza kilo 48 za nyama kutoka Afrika Kusini
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 14, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment