Wakati Tundu Lissu akimaliza muda wake wa
uongozi ndani ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na kusema hakufanikiwa
kukamilisha matarajio yake, wagombea wanaowania kumrithi wameahidi kufanya
mabadiliko makubwa ikiwamo kuhamishia ofisi za chama hicho makao makuu ya nchi,
Dodoma.
Lissu, ambaye anaendelea na matibabu nchini
Ubelgiji alichaguliwa kuwa Rais wa TLS Machi 18 mwaka jana lakini alitumikia
nafasi hiyo kwa takriban miezi sita baada ya Septemba 7 kushambuliwa kwa risasi
zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akiwa nje ya makazi yake mjini Dodoma baada
ya kutoka bungeni.
Baada ya shambulio hilo, alipelekwa
Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na usiku wa siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali
ya Nairobi ambako alilazwa hadi Januari 6 alipohamishiwa Ubelgiji kwa matibabu
zaidi
Tayari wanasheria wanne wamejitokeza kawania
nafasi hiyo katika uchaguzi utakaofanyika Aprili 14 jijini Arusha, safari hii
ukifanyika chini ya masharti mapya kwa wagombea tofauti na ilivyokuwa huko
nyuma
Masharti hayo ambayo yapo katika kanuni za
uchaguzi huo kwenye Gazeti la Serikali (GN) namba 116 ya mwaka 2018, kipengele
cha (8) (e) kinaeleza kuwa mwanachama anayetaka kugombea asiwe mtumishi wa
umma, mbunge, diwani au hatakuwa kiongozi wa chama cha siasa kilichosajiliwa.
Wanasheria waliojitokeza kuwania urais ni
Fatma Karume, Godwin Ngwilimi, Godwin Mussa na Godfrey Wasonga. Aliyepitishwa
na kamati ya uchaguzi ya TLS chini ya mwenyekiti wake, Dk Kibuta Ongwamuhana
kuwania umakamu wa rais ni Rugemeleza Nshalla.
Ahadi za wagombea
Akizungumzia sababu za kuwania nafasi hiyo,
Mussa alisema: “TLS kwa sasa inahitaji kiongozi atayeweka wanachama pamoja kwa
kuwaunganisha na kupunguza tofauti ili inapofanya jambo, linakuwa la pamoja na
wanachama wanaishi kuendana na taaluma yao ya sheria na si vinginevyo
“TLS ilipoanzishwa mwaka 1954, ilikuwa na
malengo yake na moja ni kuishauri Serikali katika masuala ya sheria, lakini
hili limepotea kabisa na linahitaji kufanyiwa kazi. Lakini lengo jingine
lilikuwa ni kutoa msaada kwa wanyonge wanaohitaji haki ila kutokana na unyonge
wao hawakuweza, sasa nitahakikisha hili linafanyika.”
Mussa alisema atahakikisha anarejesha
uhusiano kati ya taasisi hiyo na Serikali; “Na Serikali ione TLS ni mdau muhimu
na TLS ione Serikali nayo ni mdau muhimu pia kwani hakuna Serikali yoyote
duniani inayokubali kuona chombo chake kikienda visivyo ikakubali.”
Alisema kukiwa na mazingira mazuri kati ya
TLS na wadau wengine, hata misuguano ya hapa na pale haitakuwapo na Serikali
itapokea ushauri kutoka kwa wanasheria kama lengo lake tofauti na ilivyo sasa
akisema inaweza isiuchukue hata kama ni mzuri
Kuhusu masharti ya mwaka huu ya kuwaengua wanasiasa na watumishi wa umma, Mussa alisema, “Hili linazungumzika, TLS inaendeshwa kwa misingi yake, hata kama mtu ana cheo huko hakiwezi kuathiri na kwa kuwa Baraza la Uongozi lipo, nafikiri hawezi kuathiri kwa hiyo hili nikifanikiwa kushinda nitalifanyia kazi tusiwanyime fursa watu.”
Mgombea mwingine, Fatma Karume alisema, “Uongozi wa Tundu umekatizwa kwa kitendo cha uhalifu. Ukitazama uongozi wa Tundu umekuwa mfupi sana, hajaweza kutimiza yale aliyotaka kutimiza si kwa matakwa yake ila waliotaka kumuua.”
Fatma ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa
Zanzibar, Amani Abeid Karume alisema kuna watu wengi hawajui haki zao na sheria
hivyo ni wajibu wa TLS kuwasaidia na kuhakikisha sheria za nchi zinaheshimiwa
na kila mmoja
“Nitahakikisha TLS tunajali wanachama wetu,
tunawajali wanasheria wetu kwa sababu hiyo ni muhimu sana. Huwezi kumpenda mtu
wa nje kama wewe hujipendi ni muhimu kukaa pamoja, tupendane halafu tuhakikishe
tunawasaidia wananchi,” alisema.
Alisema hategemei ndani ya mwaka mmoja
akamaliza kila kitu lakini, “Nitahakikisha nawasha taa kidogo watu waone na mtu
mwingine atakuja na kuendelea kwani mtu mmoja huwezi kumaliza kila kitu kwa
mwaka mmoja.”
Wakati Fatma akisema hayo, Wasonga alisema:
“Nimejipanga vizuri tu na endapo nikipewa nafasi ya kuwa kiongozi, kuna vitu
naviona haviko sawa hasa huu uchaguzi. Kila mwaka unaendeshwa, ili kupunguza
gharama, kuna haja ya kuishawishi Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria
na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tuibadili Sheria ya TLS ili kiongozi
akae miaka miwili au mitatu.”
Alisema kutokana na ongezeko la mawakili
ambao sasa wako takriban 6,000 anaona hakuna haja kila mwaka kukutana wote katika
mkutano mkuu hivyo atapendekeza kuwapo kwa wawakilishi ili kupunguza gharama.
Wasonga alisema anachokiona sasa, TLS
inahitaji maboresho ya sheria ili kwenda na kasi ya teknolojia akisema,
“Tunakwenda mbali, tumekuwa kama chama cha siasa, sasa turudi katika malengo ya
kuanzishwa kwa TLS na mimi nataka kulifanya hilo. Sisi kazi yetu ni kuisaidia
jamii ya Watanzania katika masuala ya sheria, tuwasemee wananchi katika mambo
ya shida, tuikosoe Serikali pale taratibu zinapovunjwa bila kukiuka maadili ya
taaluma yetu
“Mimi nataka kuondoa ‘tension’ iliyopo kati
ya TLS na Serikali kwa sababu TLS imeanzishwa na sheria kwa hiyo ni mali ya
Serikali. Kwa hiyo nataka kuondoa uadui uliopo ili Serikali iweze kuwa karibu
nasi bila kuathiri nafasi ya mtu yoyote.”
Wasonga alisema wadau wakuu wa TLS ni
Serikali na Mahakama ambazo zote zinahamia Dodoma; “Na mimi kwa kuwa ni
mwenyeji wa Dodoma, kwa hiyo hatuwezi kujitenga na wadau wetu, hivyo wakinipa
nafasi nitaanza utaratibu wa kuihamishia TLS mkoani Dodoma.”
Wakati wagombea wenzake wakijinadi Ngwilimi
ambaye sasa ni makamu wa rais, alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sasa kwani
kampeni hazijaanza na kwamba zikianza atafanya hivyo.
Hata hivyo, baadhi ya wagombea wenzake
walipinga kauli hiyo wakisema kampeni hizo zimeshaanza huku Wasonga
akithibitisha kwa kusema; “kampeni zimeshaanza na mimi Jumatatu nitafanya
mkutano mkubwa sana na waandishi hapa Dodoma.”
Mgombea mwingine aliyezungumzia suala la
kuanza kwa kampeni ni Mussa ambaye alisema, “Kwa kawaida kampeni rasmi huanza
siku moja kabla ya uchaguzi lakini kwa sasa ni zile za kawaida tu kama hizi
ambazo tumeongea
Kauli ya Lissu Jana, Lissu akizungumza na mwandishi wetu
alisema: “Nilipoomba kuchaguliwa na baada ya kuchaguliwa, ile siku
niliyochaguliwa (Machi 18, 2017), katika hotuba yangu baada ya kuchukua mikoba
rasmi, nilielezea changamoto kubwa zinazokaibili nchi na TLS kwa sababu
mawakili ni sehemu ya jamii
“Matatizo ya jamii ni matatizo ya TLS na
nilisema hizo changamoto hazitanyamaziwa katika mwaka wangu mmoja wa kuwa rais,
lakini nimekuwa rais kwa miezi mitano. Katika hiyo miezi mitano nilijaribu kwa
kiasi kikubwa kutimiza kile nilichoahidi.”
Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida
Mashariki alisema: “Hatukunyamaza, TLS yangu haikunyamaza, tulizungumza
palipohitaji kuzungumza, tulipiga kelele tulipohitaji kupiga kelele, kilikuwa
ni kipindi chenye changamoto kubwa sana
“Tuliitisha mkutano wa dharura na kuja wazi
kabisa kuwa hatutakubali TLS kuwa chini ya mamlaka ya Serikali.”
Lissu alisema tofauti na miaka ya nyuma
ambayo mambo yalikuwa yanafanyika na TLS imejificha, “TLS ya miezi mitano
hatukujificha uvunguni.”
Alisema hayo ni miongoni mwa yale anayojivunia.
Warithi wa Lissu wajipanga kuipangua TLS
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 23, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment