Mahakama ya
Afrika ya Haki za Binadamu (AfCHPR), imekubali hoja tatu kati ya nane za
ukiukwaji wa haki za binadamu katika hukumu ya kifungo cha maisha kwa
mwanamuziki Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mtoto wake, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’
baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya ubakaji na ulawiti
Hoja ambazo zimekubaliwa ni pamoja na
mlalamikaji Nguza kutopimwa nguvu za kiume kama alivyokuwa ameomba, kutopata
maelezo ya mashahidi na kutopata fursa ya kuwauliza maswali waliotoa ushahidi
ili kuthibitisha makosa.
Mahakama hiyo
ilitupa hoja tano za walalamikaji hao ambao jana hawakuwapo wakati uamuzi huo
ukitolewa ambazo ni pamoja na kutolewa magereza ikisema haikuwa na mashiko
tena, kutoridhishwa na mwenendo wa kesi katika Mahakama, kutopata fursa ya
kujitetea wakati wa mwenendo wa kesi na kupata msaada wa kisheria; na kukosa
haki ya kuwa na familia zao
Akisoma hukumu
katika kesi hiyo, iliyochukua dakika 55, Jaji Gerard Niyungeko kwa niaba ya
majaji wenzake saba wa Mahakama hiyo, alisema kutokana na hoja hizo nane, zilizowasilishwa
mahakamani hapo katika shauri hilo namba 006/2015, imejiridhisha kwamba tano
hazikuwa na ukiukwaji wa haki hasa kutokana na maelezo ya walalamikaji
Hoja
zilizokubaliwa
Jaji
Niyungeko, ambaye ni raia wa Burundi alisema jopo hilo la majaji limejiridhisha
pasipo shaka kwamba hoja tatu zilizowasilishwa na walalamikaji zilikuwa na
mashiko
Hoja ambazo
Mahakama hiyo imezikubali ni ile iliyowasilishwa na walalamikaji kwamba mtuhumiwa
wa kwanza, Nguza wakati wa mwenendo wa kesi hiyo, alieleza kuwa hana nguvu za
kiume na hivyo asingeweza kufanya vitendo vya ubakaji na alitaka mahakama kutoa
agizo la kupimwa na madaktari hatua ambayo haikukubalika.
Jaji Niyungeko
alisema hoja nyingine ambayo ilibainika kuwa na mashiko ni kuwa walalamikaji
hawakupata maelezo ya mashahidi.
Jaji Niyungeko
alisema wamekubaliana na hoja kuwa watuhumiwa ambao sasa wapo huru kutokana na
msamaha wa Rais, hawakupata fursa ya kuwauliza maswali waliotoa ushahidi ili
kuthibitisha makosa jambo, ambalo ni kosa
Hoja
zilizotupwa
Jaji Niyungeko
alisema, baada ya uchambuzi wa hoja katika shauri hilo, wamebaini ombi la
kwanza lilikuwa ni la kutolewa magereza ambalo hata hivyo, tayari watuhumiwa
walitolewa kutokana na msamaha wa Rais John Magufuli
Wanamuziki hao
walipata msamaha huo Desemba 9, mwaka jana wakati Rais Magufuli alipowasamehe
wafungwa 8,157 wakati akihutubia maadhimisho ya sherehe ya miaka 56 ya Uhuru wa
Tanganyika mjini Dodoma
Pia, Jaji
Niyungeko alisema mahakama hiyo imejiridhisha kuwa mwenendo wa kesi katika
shauri hilo kuanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama Kuu hadi Mahakama
ya Rufaa ulikuwa wa haki tofauti na hoja za walalamikaji kuwa kulikuwa na
ukiukwaji wa haki za binadamu hasa kutokana na ushahidi uliofikishwa mbele yake
Alisema katika
kuthibitisha kuwa mwenendo wa kesi hiyo ulikuwa wa haki, kulikuwa na tuhuma 21,
lakini hadi hukumu ilipotolewa, zilikuwa zimebaki nne tu ambazo ndizo
zilizowatia hatiani
Alisema pia
kitendo cha Mahakama za Tanzania, kuwaachia washtakiwa wengine watatu katika
shauri hilo kinaonyesha kwamba mwenendo wa kesi ulikuwa wa haki na hakukuwa na
ukiukwaji wa haki za binadamu
Jaji Niyungeko
alisema Mahakama hiyo pia imetupa hoja kuwa watuma maombi hawakupata fursa nzuri
za kujitetea wakati wa mwenendo wa kesi hiyo
Jaji
Niyungeko, alisema hoja kuwa Nguza na Johnson hawakupata msaada wa kisheria,
imetupwa kwa kuwa kulikuwa na uwakilishi wa kisheria
Alisema pia
hoja ya kuwa uamuzi wa kesi hiyo, ulikiuka mkataba wa kuanzishwa mahakama hiyo
haikuwa sahihi kutokana na kukosekana ushahidi uliofikishwa mahakamani hapo
Kadhalika,
alisema hoja kwamba wakati wa mwenendo wa kesi hiyo walalamikaji walikosa haki
yao ya kikatiba ya kuwa na familia zao na kuendelea na shughuli zao pia
imeonekana kukosa ushahidi wa athari hizo kutokana na maelezo yaliyofikishwa
mahakamani
Fidia ya
gharama za kesi
Akizungumzia
hoja ya kulipwa fidia kutokana na gharama za kesi hiyo na madai mengine, Jaji
Niyungeko alisema Mahakama imetoa mwezi mmoja kwa walalamikaji, kuwasilisha
mahakamani hapo madai yao ya fidia kama watahitaji na kutoa muda kama huo kwa
Serikali kuyajibu kabla ya kutoa uamuzi juu ya madai hayo ya fidia
Katika kesi
hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alikuwa anawakilishwa na mawakili, Sara
Mwaipopo, Nkasori Sarakikya, Baraka Luguna, Elisha Suka na Aida Kisumo.
Upande wa
walalamikaji uliwakilishwa na mwanasheria na ofisa mtendaji mkuu wa Chama cha
Wanasheria wa Afrika (Palu), Donald Deya.
Akizungumza
baada ya uamuzi huo, Deya alisema ameridhishwa na anasubiri nakala ya hukumu
ili kuteleza maagizo ya mahakama baada ya kushauriana na wateja wake
“Siwezi kusema
lolote kwa sasa, juu ya msimamo wa wateja wangu kwani hawajanipa mamlaka hayo,”
alisema.
Ilivyokuwa
Babu Seya na
wanae watatu walikamatwa Oktoba 12, 2003 na kufikishwa kituo cha Polisi cha
Magomeni jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na tuhuma za ubakaji na ulawiti wa
watoto wa kike wenye umri wa chini ya miaka 10.
Oktoba 16,
2003 wapandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu na kusomewa jumla ya mashtaka 21, kati ya hayo 10 ya ubakaji wa watoto
hao na mengine 11 ya kuwanajisi
Baada ya kuwa
wamesota mahabusu wakati kesi yao ikiendelea kusikilizwa, Juni 25, 2004
Mahakama ya Kisutu iliwahukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela
Kwa nyakati
tofauti walikataa rufani Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa na kugonga mwamba.
Sura mpya kesi ya Babu Seya na mwanae
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 23, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment