Wanafunzi wa darasa awali hadi la sita katika Shule ya
Msingi Raha Leo Elimu Maalumu (viziwi) Manispaa ya Mtwara Mikindani wanasoma
katika darasa moja, kutokana na kukosekana kwa vyumba vya madarasa.
Pia, darasa hilo linalotegemewa na wanafunzi 25 linatumika
kama ofisi ya walimu, stoo na bwalo.
Hayo yameelezwa na kiongozi wa
wanafunzi hao, Twaha Salum wakati wa kupokea zawadi kutoka kwa wanawake
wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Tawi la Mtwara, kama sehemu ya
maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa jana.
Twaha amedai kila wanapotembelewa na wageni wamekuwa
wakiwaeleza changamoto zinazowakabili ili kuwatafutia utatuzi lakini
inashindikana
“Darasa hili linatumika na wanafunzi wote wa elimu maalumu,
ndiyo stoo, ofisi ya walimu wetu na tunalitumia kama. Changamoto ni nyingi kila
wakija wageni tunawaambia lakini hakuna kinachofanyika,”amesema Twaha.
Mwalimu wa kitengo hicho, Caroline Chitunda amesema mbali na
changamoto zilizotajwa na mwanafunzi huyo, wanakabiliwa na ukosefu wa bweni
na chumba maalumu kwa ajili ya kupimia usikivu wa wanafunzi licha
ya kupatiwa vifaa vyote
“Kama mnavyoona meza moja wanasomea madarasa mawili mawili.
Pia tuna uhaba wa vyumba vya madarasa na chumba cha upimaji wa masikio kwa
sababu wanaofika kuanza kusoma hapa lazima apimwe usikivu, ni chumba maalumu
hakitoi sauti na hakiingizi sauti lakini vifaa vyote tunapatiwa na Serikali,”
amesema Chitunda.
Mwalimu mkuu msaidizi, Ally Matola amesema wanafunzi wa
madarasa mawili wanatumia mbao moja kwa ajili ya kusoma
“Mbao moja inatumika wa madarasa mawili,hawa watoto wasio na
usikivu kipindi kimoja kinachukua muda mrefu tofauti na wale wenye usikivu
kamilifu, walimu wanapokezana kufundisha unakuta vipindi kwa siku
havikamiliki,” amesema Mwalimu Matola.
Ofisa Habari wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Jamadi Omari
amesema wanatambua changamoto zinazoikabili shule hiyo na kwa sasa wameanza
kutafuta ufumbuzi wa vyoo kwanza
“Tunalifahamu lakini manispaa tuna changamoto nyingi na
katika Shule ya Raha Leo tumeanza na vyoo kwanza kwa sababu ni tatizo na
tunafanya kwa awamu kutatua changamoto zilizopo,”amesema Omari.
Wakina mama wa BoT Tawi la Mtwara wamekabidhi sukari,
unga, mafuta ya kula, majani ya chai, biskuti, shuka, maharagwe, mchele na
juisi ambazo fedha zimetokana na kujichanga kwa wafanyakazi wakiwamo wanaume.
Mwenyekiti wa kamati ya kina mama, BoT Tawi la Mtwara, Zakia
Juma ameiomba jamii kujitokeza na kuwatembelea watoto wenye uhitaji maalumu
kwani na wao wanahitaji upendo.
Wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia wasomea darasa moja
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 09, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment