SIFA zote njema anastahiki Mola Azza
Wajalla mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na nyingine ndogondogo.
Swala na salamu zimwendee kiongozi
wa Umma, si mwingine bali ni Mtume Muhammad Swalla Allahu alayhi wa Sallam, maswahaba
zake kiram na watangu wema hadi siku ya Qiyamah.
Ewe ndugu yangu kila siku unasikia
kama kuna jambo la sadaka, je unafahamu maana yake na faida za ibada hii na
thawabu za mwenye kulifanya jambo hili?
Basi leo ndio nimependa
kulizungumzia jambo hili kwa Tawfiq ya Allah SubuhanaLlah Wataala.
Sadaka ni kile kinachotolewa ili kujikurubisha kwa Allah na hali ya kutarajia malipo kutoka kwake.
Sadaka zipo za aina nyingi kwa mfano kimaneno na
kimatendo. Miongoni mwa mifano ya sadaka ni kama mali, nguo, chakula,tabia
njema, nasaha, kulea mayatima, kujenga msikiti, n.k
Zifuatazo ni Faida au Fadhila za
Kutoa Sadaka :
Itakua ni kuvuli kwa mwenye kuitoa
siku ya Qiyamah siku ambayo haitokua na kivuli ila kivuli ambacho Allah
atawafunika waja wake maalumu. Amesema Mtume Swalla llahu Alayhi wasallam
Kila mtu atakua chini ya kivuli cha sadaka yake mpaka watakapo hukumiwa watu-siku ya kiama (Ahmad)
Kila mtu atakua chini ya kivuli cha sadaka yake mpaka watakapo hukumiwa watu-siku ya kiama (Ahmad)
Huondosha Hasira za Allah.
Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam ((Hakika ya sadaka huzima hasira za Allah))Tirmidhiy.
Huunganisha udugu: Nalo ni jambo
ambalo limesisitizwa sana katika dini kuuchunga na kuunga udugu kwani
amezawadiwa pepo kila mwenye kuunga udugu na amelaaniwa mwenye kuukata.
Na kwa
ajili hio sadaka kwa ndugu wa karibu huandikwa ujira mara mbili wa kutoa sadaka
kuunga udugu.
Huepushwa mbali mwenye kuitoa na
vitimbi vya shetani: Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam ((Hatoi mmoja
wenu chochote katika sadaka isipokuwa huwekwa mbali nae kwa sadaka ile
mashetani sabini)) Imepokelewa na Ahmad na ameisahihisha Albaniy.
Inamsafisha mwenye kuitoa na kumtakasa: Amesema Allah subhanahu wataala Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo, na uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua. 9:103.
Malipo yake huendelea hata baada ya
kufa kwako: Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam. Atakapo kufa
mwanaadamu hukatika matendo yake ILA katika matatu;sadaka yenye kuendelea au
elimu yenye kunufaisha au mtoto mwema mwenye kumuombea mzazi wake (Muslim).
Miongoni mwa sadaka yenye kuendelea ni kujenga au kushiriki katika kujenga
kisima, msikiti au kupanda mti ambao viumbe vitanufaika nao n.k.
Malipo yake huongezwa mara dufu na
Allah Subhanahu Wataala: Kama anavyotuelezea Mfano wa wanao tumia mali zao
katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyo chipuza mashuke
saba. Katika kila shuke zimo punje mia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye,
na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua.]] 2:261.
Pia amesema Mtume wa Allah (swalla
Allahu alayhi wasallam) katika hili ((Mwenye kutoa sadaka kiasi cha tende
kutoka kwenye chumo jema na wala Hakubali Allah ila kilicho chema, basi Allah
anaipokea kwa mkono wa kulia kisha huilea kwa ajili ya alieitoa kama anavyomlea
mmoja wenu farasi wake mpaka iwe kama jabali.)) Bukhari na Muslim.
Sadaka ni Sababu ya Kuponywa
Maradhi: Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam ((Jiponesheni
maradhi yenu kwa kutoa sadaka))Albaniy.
Sadaka hufuta madhambi madogo:
Amesema Mtume Swalla llahu Alayhi Wasallam :.Na sadaka huzima madhambi
madogo kama yanavyozima maji moto. Tirmidhiy.
Humuepusha mwenye kuitoa na kifo
kibaya… Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam, ... Na pia Sadaka
humuepusha na Kifo kibaya. Tirmidhiy.
MAMBO YA KUJIZINGATIA KATIKA KUTOA
SADAKA
a) Jiepushe kuwaudhi watu na
kuwasimanga baada ya kuwapa sadaka.
b) Jiepushe na Ria, Toa kwa ajili ya
Allah.
Allah subhanahu wataala anasema:
[Enyi mlio amini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi, kama
anayetoa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Mwenyezi Mungu wala
Siku ya Mwisho.
Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana
udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uweza
wowote kwa walivyo chuma.
Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.] 2:264
c) Jitahidi kujificha wakati
unapotoa sadaka yako kadri uwezavyo.
Hili linakuepusha na ria na dhana mbaya kutoka kwa watu. Amesema Mtume swalla Allahu alayhi wasallam… (Watu saba watafunikwa na kivuli cha Allah siku ambayo haina kivuli ila kivuli chake…) na miongoni mwao akatajwa ni (Na mtu alietoa sadaka akaificha mpaka mkono wake wa kushoto usijue kilichotolewa na mkono wa kulia)) Bukhari na Muslim.
d) Tambua kuwa Sadaka bora ni ile
unayompa mtu wa karibu yako.
Yaani wazazi,mkeo, wanao na ndugu zako. Amesema Mtume swalla Allahu alayhi wasallam : ((Dinar unayoitoa katika njia ya Allah, na dinar unayoitoa katika mtumwa na Dinar unayoitoa kwa maskini na Dinar unayoitoa kwa watu wako, iliyobora kwa malipo ni ile ulioitoa kwa watu wako)). Imepokelewa na Imam Muslim. na watu wako maana yake ni ndugu zako wa karibu.
Kama tulivyo wataja
hapo juu.
e) Toa kitu kizuri katika
unavyovipenda na sio usichokipenda au ambacho hukitaki.
Amesema Allah Subhanahu Wataala : [[KABISA
HAMTAFIKIA wema mpaka mtoe katika vile mnavyo vipenda. Na kitu chochote mnacho
kitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua.]] 3:92.
f) Pendelea kuwapa sadaka yako watu
wema.
Hili litakusaidia kupata dua zao pia
utakua na uhakika kama wataitumia katika njia nzuri kwani endapo utampa mtu muovu
kama mlevi n.k utakua umemsaidia katia kuyafanya maasi.
g) Tambua ya kwamba Sadaka
haipunguzi mali bali huiongeza.
Amesema Mtume Swalla Allahu Alayhi
wasallam. ((Haipungui mali kutokana na kutoa sadaka)) Muslim.
Tujihimize katika kutoa sadaka ili tuweze
kupata ujira uliotajwa hapo juu. Muhimu zaidi tuyazingatie yote tuliyoelezwa
ili tuweze kupata ujira kamili kutoka kwa Allah. ALLAH ATUTAKABALIE SADAKA
ZETU. AMIN
Tambua Umuhimu wa kutoa Sadaka na fadhila zake katika Uislamu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 09, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment